Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 14 Septemba 2009 20:07

VISA VYA KUELIMISHA (12)

VISA VYA KUELIMISHA (12)

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

******

Hii ni sehemu nyingine ya Visa vya Kuelimisha. Lakini, kama nilivyotangulia kusema katika kisa kilichopita, si vile visa vya ngano za kubuni za alfu lela ulela, wala si vya Hadithi za kutunga, za Paukwa Pakawa au za matukio ya uvumi na tetesi ya sadiki ukipenda. Ni visa vya matukio ya kweli, yaliyotokea katika maisha ya viongozi halisi wa wanaadamu, yaani Manabii wa Mwenyezi Mungu. Visa ambavyo ni kigezo na ruwaza njema, kwa mimi na wewe, ya kuweza kubadilisha maisha yetu, na kutufanya tupate fanaka, na saada, ya leo hapa duniani, na kesho, huko akhera. Ni visa vya matukio yaliyojiri katika maisha ya waja wema wa Allah, ambao kwao wao, Quran, Suna za Bwana Mtume na mafundisho ya Maimamu, vilikuwa ni miongozo ya kufuata kivitendo, katika kila kipengele cha maisha yao, na si mambo ya kuishia kwenye uhodari wa kuyatamka kwa ghibu tu, na kuyasimulia kwa wengine. Ni matumaini yangu kwamba, si mimi na wewe tu mpenzi msikilizaji, bali hata wale wote tutakaowafikishia, ujumbe uliomo ndani ya visa hivi vya kuelimisha, watayachukua mafunzo yake, na kuyatoa katika sura ya nadharia, na kuyafanya kuwa ni somo la amali na vitendo, katika maisha yao ya kila siku.

*******

Soko la mji wa Madina lilikuwa limejaa watu ambao kila mmoja wao alikuwa ameleta bidhaa yake kuuza na wakati huo huo kujinunulia ngano au shayiri. Hata hivyo hakuna duka lolote sokoni hapo ambalo lilikuwa na yoyote kati ya bidhaa mbili hizo. Wakati huo ilisikika sauti ya mtu mmoja aliyekuwa akinadi kwa kusema:"jamani mke wangu na watoto wangu wana njaa, chukueni hii mashk ili munipatie ngano na shairi japo kidogo.

Hata hivyo mtu hakuna yeyote aliyemjali Bwana huyo. Katika lahadha hiyo na katika mazingira kama hayo Imam Jaafar Sadiq (as) mmoja wa wajukuu watoharifu wa Bwana Mtume Muhammad saw, akiwa amefuatana na mtumishi wake aitwaye Hilal alikuwa akipita sokoni hapo. Wakati Hilal aliposhuhudia hali hiyo ya uhaba wa ngano na shairi alipumua kwa nguvu na kujisemea moyoni mwake: Ah mwaka huu tutalivuka salama janga hili la njaa/ukame kwani tuna akiba ya kutosha ya ngano. Akiwa amezama katika mawazo hayo, ghafla Hilal aligundua kuwa Imam alikuwa akikazana kama kwamba alikuwa ameguswa na kushughulishwa na kitu. Alionekana mwenye huzuni na moja kwa moja alifululiza hadi nyumbani kwake.

Hilal naye alimfuata hadi huko huku akijisemea:" Sijawahi kumwona Imam akiwa katika hali kama hii, tuseme ni kutokana na hali hii ya janga la njaa? Afadhali ningemwambia roho yako ikatulia." Baada ya kulitafakari hilo, Hilal alielekea kwenye stoo ya chakula ambako magunia ya ngano yalikuwa yamepangwa kutoka pembe moja hadi nyingine. Aliyabinyabinya magunia hayo na kuzihisi punje za ngano iliyojaa ndani yake, ngano ambayo ilitoka mji wa Taif ikiwa na ubora zaidi kuliko ile ya mji wa Madina. Hilal alikuwa hajijuia hajitambui kwa furaha huku akijipongeza mwenyewe kwa kuwa aliwatangulia wengine kununua ngano hiyo iliyokuwa nzuri mno.

Aliyaweka weka sawa magunia ya ngano stooni alimukuwemo kisha akaegemea kiguzo na kufumba macho huku akitabasamu kutokana na faraja aliyoihisi iko mbele yao kwa kuwa na chakula cha kutosha wakati njaa ilikuwa inaunyemelea mji wa Madina. Lakini ghafla alimkumbuka Imam Jaafar Sadiq na hali ya huzuni aliyokuwa nayo.

Hadi wakati huo Hilal alikuwa ameshindwa kuelewa huzuni ya Imam ilitokana na jambo gani, kiasi kwamba alianza kujishuku yeye mwenyewe na kusema:"Ee Mola wangu, nimeteleza na kufanya gani mie!" Lakini wakati nimekuwa nikijaribu kufanya lile linalomridhisha Imam". Hilal alitoka stoo alikokuwa na kwenda hadi kilipokuwepo kisima cha maji ili kuweza kunawa uso kidogo na kuondoa fikra mbaya zilizokuwa zikimpitikia.

Akiwa anajitayarisha kuteka maji ghafla alimsikia Imam akimwita. Sauti hiyo haikuwa ile ya kawaida ya mtu mwenye bashasha na uchangamfu. Huku akiwa ameyatulizia macho maji yaliyokuwa yametulia tuli kisimani, ghafla Hilal alisikia tena sauti ya Imam Sadiq, na hapo hakuweza kusita tena bali alianza kuvikwea vidaraja vya ngazi ya udongo na kufululiza moja kwa moja hadi chumbani kwa Imam.Baada ya kumsalimia alisimama kando ili kusikiliza wito alioitiwa.

Imam Sadiq alimuuliza:" Tuna akiba ya chakula humu ndani? Suali hilo liliutuliza moyo wa Hilal na kwa furaha akajibu: "Naam, tuna akiba ya ngano kwa matumizi ya mwaka mzima na pengine zaidi." Imam ambaye alikuwa ameketi kwenye busati la ukindu alinuka na kujongea hadi dirishani, akatupia jicho mitende iliyokuwepo kwenye ua wa nyumba yake ambayo majani yake yalikuwa yamepiga umanjano na weusi kwa joto kali. Hapo alimgeukia Hilal na kumwambia:"Akiba yote ya ngano tuliyonayo ichukue wende ukaiuze sokoni".

Hilal alishtuka kiasi kwamba alidhani labda hakusikia vizuri maneno ya Imam. Hivyo akauliza kana kwamba hakusikia vizuri. naye Imam sadiq akakariri maneno yake na kumwambia:"Akiba yote ya ngano tuliyonayo, ichukue wende nayo sokoni ukaiuze." Kwa mshangao Hilal alimuelekea Imam na kumwambia:" Kama tutaiuza ngano tuliyonayo hatutoweza kupata ngano nyingine ya kununua. Maneno hayo ya Hilal yalitokana na hofu kubwa aliyokuwa nayo kuhusiana na hali ya uhaba wa ngano uliokuwepo. Imam Sadiq as alimjibu kwa kumuuliza:" Sasa watu wafanyeje?".

Hilal aliinamisha uso wake chini na kusema:" Wao mahitaji yao kila siku wanayapata kwa kununua huko sokoni. Huko ngano na shairi huchanganywa pamoja na kuuzwa. Lakini baadhi ya watu hulazimika kufanya mikate ya shairi tu." Imam Sadiq alimjongelea karibu Hilal, akamtazama usoni na kumwambia:" Kaiuze ngano, na kuanzia kesho uende huko huko sokoni kununua mikate kwa ajili yetu." Hilal alipumua kwa nguvu na kumwangalia Imam ambaye aliendelea kumwambia:" hivi sasa watu katika hali ya shida na dhiki. ijapokuwa hatuna uwezo wa kuwafanya watu wote wale mkate wa ngano kama sisi, lakini tunaweza kushirikiana nao katika hali waliyonayo". Imam Sadiq as alimkumbusha tena Hilal yale maneno matukufu ya Bwana Mtume yasemayo:" Wapendeleeni watu yale mnayojipendelea nafsi zenu.

 

*******

Tafadhali msimulie na mwenzako.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …