Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 14 Septemba 2009 20:03

VISA VYA KUELIMISHA (11)

VISA VYA KUELIMISHA (11)

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

******

Hii ni sehemu nyingine ya Visa vya Kuelimisha. Lakini, kama nilivyotangulia kusema katika kisa kilichopita, si vile visa vya ngano za kubuni za alfu lela ulela, wala si vya Hadithi za kutunga, za Paukwa Pakawa au za matukio ya uvumi na tetesi ya sadiki ukipenda. Ni visa vya matukio ya kweli, yaliyotokea katika maisha ya viongozi halisi wa wanaadamu, yaani Manabii wa Mwenyezi Mungu. Visa ambavyo ni kigezo na ruwaza njema, kwa mimi na wewe, ya kuweza kubadilisha maisha yetu, na kutufanya tupate fanaka, na saada, ya leo hapa duniani, na kesho, huko akhera. Ni visa vya matukio yaliyojiri katika maisha ya waja wema wa Allah, ambao kwao wao, Quran, Suna za Bwana Mtume na mafundisho ya Maimamu, vilikuwa ni miongozo ya kufuata kivitendo, katika kila kipengele cha maisha yao, na si mambo ya kuishia kwenye uhodari wa kuyatamka kwa ghibu tu, na kuyasimulia kwa wengine. Ni matumaini yangu kwamba, si mimi na wewe tu mpenzi msikilizaji, bali hata wale wote tutakaowafikishia, ujumbe uliomo ndani ya visa hivi vya kuelimisha, watayachukua mafunzo yake, na kuyatoa katika sura ya nadharia, na kuyafanya kuwa ni somo la amali na vitendo, katika maisha yao ya kila siku.

*******

Katika mji mmoja walikuwepo wawindaji wawili ambao kutokana na kazi ya uwindaji waliweza kujipatia riziki ya kuendeshea maisha yao. Siku moja kama ilivyokuwa kawaida yao walifunga safari ya kuelekea maeneo ya majangwani kwa ajili ya shughuli zao za uwindaji. Wakiwa njiani kuelekea huko wakafika sehemu moja ya nyika ambapo walionekana hapo wakiruka huku na huko aina kwa aina za ndege wenye rangi za kupendeza kiasi kwamba mmoja kati ya wawindaji wawili hao ambaye alikuwa mtu wa tamaa sana alisema, "hapa ndipo mahali tulipokuwa tukipasaka kwa muda mrefu, tubaki hapa hapa na kutega ndege hawa kadiri tutakavyoweza kuwanasa".

Ama yule rafiki yake ambaye alikuwa mtu mwenye busara na uzoefu alimwambia:" Sikiza rafiki yangu, tamaa si kitu kizuri, wacha leo tuwinde kiasi ya kile tunachohitaji tu, huenda kesho tukapata mawindo mazuri zaidi". Wawindaji hao wawili waliweka mitego yao kwenye eneo hilo na kutawanya chembe za nafaka, kisha wakaa kitako wakisubiri bahati yao. Baada ya kupita saa kadhaa hatimaye ndege mmoja mzuri sana aliukaribia mtego wa wawindaji, na mara baada ya kuanza kudona dona chembe chembe za nafaka, ghafla alinasa kwenye mtego huo. Wawindaji walifurahi mno.

Walimchukua ndege huyo na kumtia kwenye tundu na kuanza safari yao ya kurudi mjini kwa lengo la kwenda kumuuza. Wakiwa njiani, mara kwa mbali nyuma yao, walisikia sauti ya kwata za farasi aliyekuwa akikata masafa kwa kasi kuelekea lango la kuingilia kwenye mji. Wakati mtu aliyekuwa amempanda farasi huyo alipowakaribia wawindaji hao, aligutuka alipomwona ndege mzuri sana aliyekuwemo tunduni. Alimsimamisha farasi wake, akawaelekea wawindaji na kuwaambia:" Mumemnasa ndege mzuri ajabu, mko tayari kuniuzia?" Hapo wawindaji wale walibaini kuwa bwana mpanda farasi alikuwa Liwali wa mji wao.

Hivyo wote kwa pamoja walimmwamkia na kusimama mbele yake kwa heshima. Liwali aliendelea kwa kuwauliza:" Kiasi gani cha pesa mnataka kama malipo ya ndege huyu?" Wawindaji wawili walitizamana kwa mshangao, na hapo Liwali akashuka farasi wake na kuwaambia: "Ndege huyu ni mzuri sana; mimi niko tayari kukupeni dinari elfu moja". Mwindaji mwenye hekima na busara alifurahi kusikia maneno hayo na akasema:" Tumekubali ewe Liwali muadhamu. Lakini kabla maneno yake hayajamaliza kutoka kinywani, mwenzake aliyekuwa mtu wa tamaa alimdakiza huku akilalamika kwa kusema:" Hapana mheshimiwa Liwali, huyu rafiki yangu hajui chochote kuhusu mambo ya uuzaji na ununuzi wa ndege. Acha kwanza twende tukaulizie bei ya kawaida ya ndege kama huyu. Unajua tumetaabika sana mpaka tumemnasa ndege huyu". Liwali alimwambia: "Vyema, nyinyi nendeni mkaulizie bei yake; bei yoyote mtakayopewa mimi nitamnunua". Baada ya kutamka hayo Liwali alipanda farasi wake na kuendelea na safari yake.

Mwindaji mwenye hekima alimgeukia rafiki yake mwenye tamaa na kumwambia:" Ndo umefanya nini, kwa nini hukuacha tukamuuzia Liwali huyu ndege? Unadhani nani atakubali kutupa dinari elfu moja kwa ajili ya ndege huyu?" Mwindaji mwenye tamaa alijibu:" Thamani ya ndege huyu ni zaidi ya hizo dinari elfu moja. Acha twende tukaulizie bei yake". Bila ya kurefusha mjadala, wawindaji wawili walielekea mjini na kufululiza moja kwa moja hadi kwa wauzaji maarufu wa ndege ili kuulizia bei ya ndege wao. Kila muuzaji waliyemwendea aliwaambia kuwa thamani ya ndege wao huyo haizidi dinari hamsini. Lakini pamoja na hayo mwindaji mwenye tamaa bado hakuridhika, na hivyo siku ya pili akaamkia kwa Liwali na kumwambia:" Liwali muadhamu, ndege huyu thamani yake ni zaidi ya dinari elfu moja". Liwali alimwambia, "kama ni hivyo basi mimi nitakupeni dinari elfu mbili, kwa sababu nimempenda sana huyu ndege, unasemaje?"

Mwindaji huyo ambaye alikuwa akizidi kuingiwa na tamaa hakuridhika pia na pendekezo hilo lililotolewa na Liwali. Bado alihisi ni bora aendelee kupandisha bei yake na kutojali pia hata nasaha alizopewa na rafiki yake yaani mwindaji mwenzake ambaye alimuasa kwa kumwambia: "Acha tamaa hizo rafiki yangu", na zaidi akamtahadharisha kwa kumwambia: "Mimi nina wasiwasi na maneno ya Liwali, nahisi kuna mtego ametutegea katika kadhia hii". Hata hivyo nasaha hizo za rafiki yake zilikuwa kazi bure, chambilecho wahenga, sikio la kufa, halisikii dawa. Mwindaji mwenye tamaa alimwelekea rafiki yake na kumwambia: "We unasema nini bwana!, mimi nakwambia Liwali amemhusudu huyu ndege; na yuko tayari kutupa pesa zozote tunazotaka ili ampate ndege huyu".

Hivyo alimwendea tena Liwali na kumtaka sasa awape dinari elfu kumi ili wamuuzie ndege yule. Wakati aliposikia maneno hayo Liwali aliangua kicheko kikubwa, na papo hapo akamwita mweka hazina wa mamlaka ya mji na kumwambia:" Sasa hivi nenda kalete akiba yote ya fedha iliyopo umpe bwana huyu". Baada ya kutamka hayo alimtoa yule ndege tunduni na kumwachia ende zake. Kisha akasema, "nimekubali uliyotaka kwa sababu ya yule ndege, na kutokana na thamani na gharama kubwa aliyonayo".

Baada ya hapo akaanza kuanguka kicheko tena na kuwafanya wale wawindaji wang'amue kuwa Liwali amekusudia kuwacheza shere hata pale alipomwita mweka hazina na kumtaka akakombe akiba yote ya fedha na kumletea mwindaji mwenye tamaa. Hapo Liwali yule alimgeukia mwindaji mwenye busara na hekima na kumwambia:" Nyinyi mlidhani mimi siijui bei ya ndege yule kwamba thamani yake haizidi dinari hamsini. Wakati nilipojua kuwa huyu mwenzako ni mtu wa tamaa nilitaka nione moto wa tamaa unaofukuta ndani ya nafsi yake utaishia wapi, ili niweze kumpa funzo la kumuelimisha.

Tokea mwanzo mimi nilikuwa tayari kukupeni dinari elfu moja, lakini tamaa ya huyu mwenzako imekufanyeni mukose hata hizo dinari elfu moja". Baada ya kuambiwa hayo wawindaji wawili wale waliondoka taratibu huku mwindaji mwenye tamaa akiwa amepatwa na majuto kwa aliyoyafanya. Rafiki yake alimwambia: "umeona rafiki yangu?, mimi kila nilivyokuasa hukusikia, hata hivyo mkasa huu imekuwa ni tajiriba nzuri ya kukufanya uache tamaa; na inafaa umshukuru Liwali kwa funzo alilokupa".

*******

Mpenzi msomaji hayo basi ndiyo yaliyowapata wawindaji wawili, kutokana na tamaa ya mmoja wao.

*******

Tafadhali msimulie na mwenzako.

 

Zaidi katika kategoria hii: VISA VYA KUELIMISHA (12) »

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …