Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 14 Septemba 2009 19:57

VISA VYA KUELIMISHA (10)

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

******

Hii ni sehemu nyingine ya Visa vya Kuelimisha. Lakini, kama nilivyotangulia kusema katika kisa kilichopita, si vile visa vya ngano za kubuni za alfu lela ulela, wala si vya Hadithi za kutunga, za Paukwa Pakawa au za matukio ya uvumi na tetesi ya sadiki ukipenda. Ni visa vya matukio ya kweli, yaliyotokea katika maisha ya viongozi halisi wa wanaadamu, yaani Manabii wa Mwenyezi Mungu. Visa ambavyo ni kigezo na ruwaza njema, kwa mimi na wewe, ya kuweza kubadilisha maisha yetu, na kutufanya tupate fanaka, na saada, ya leo hapa duniani, na kesho, huko akhera. Ni visa vya matukio yaliyojiri katika maisha ya waja wema wa Allah, ambao kwao wao, Quran, Suna za Bwana Mtume na mafundisho ya Maimamu, vilikuwa ni miongozo ya kufuata kivitendo, katika kila kipengele cha maisha yao, na si mambo ya kuishia kwenye uhodari wa kuyatamka kwa ghibu tu, na kuyasimulia kwa wengine. Ni matumaini yangu kwamba, si mimi na wewe tu mpenzi msikilizaji, bali hata wale wote tutakaowafikishia, ujumbe uliomo ndani ya visa hivi vya kuelimisha, watayachukua mafunzo yake, na kuyatoa katika sura ya nadharia, na kuyafanya kuwa ni somo la amali na vitendo, katika maisha yao ya kila siku.

*******

Baada ya kimya kirefu na kupita muda mwingi bila kuonana na swahibu wake, bwana mmoja wa makamo hivi aliyekuwa akiishi katika mji mmoja aliamua kufunga safari ya kwenda kumtembelea swahibu na rafiki yake huyo aliyekuwa akiishi katika mji mwingine ulioko mbali. Wakati wa ile lahadha ya kuonana baada ya kupoteana kwa siku nyingi, marafiki wawili walikumbatiana kwa furaha kubwa, na kupitisha saa chungu nzima wakikumbushana mengi yaliyopita katika maisha yao, ikiwa ni pamoja na siku za furaha za enzi za ujana wao. Mwenyeji alimtafadhalisha mgeni wake abaki nyumbani kwa muda wowote atakao. Mgeni naye hakujivunga bali aliipokea kwa mikono miwili ihsani hiyo aliyofanyiwa. Baada ya mwenyeji kutajamali na mgeni wake kama ilivyo ada ya mwenyeji kwa mgeni , anuai za vinywaji na sharubati ziliandaliwa kwenye mkeka wa kupendeza. Na baada ya hapo ikafuatia karamu ya chakula cha mchana, ya nyama ya kuchoma ya kondoo iliyonona, pamoja na mapochopocho ya kila aina. Alhasri mgeni alikirimiwa mno, naye akatoa shukrani zake za dhati kwa mwenyeji wake. Baada ya kumaliza kula, mgeni alijongea hadi kwenye mti wenye kivuli kilichotandawaa, uliokuwepo kwenye ua wa nyumba, ili kupumzika na kupunguza shibe. Na hivyo ndivyo siku ya kwanza ya ugeni ilivyopita; usiku ukaingia, na kufumba na kufumbua kukawa kumepambazuka na siku ya pili ya ugeni ikaanza. Siku hiyo staftahi iliyokamilika iliandaliwa kwa ajili ya mgeni. Na baada ya kufungua kinywa mwenyeji alimgeukia mgeni wake na kumwambia: Rafiki yangu mpenzi, hebu niambie sasa ungependa nikutayarishie nini leo kwa ajili ya chakula cha mchana? Mgeni ambaye alikuwa alipatwa na soni kwa ukarimu mkubwa aliofanyiwa, alimjibu rafiki yake kwa kumwambia:" Wewe umegharamika sana kwa ajili yangu, na kwa kweli hakuna ulichobakisha ambacho hukuniandalia". Ama mwenyeji aliendelea kutajamali na mgeni huku akitoka kwa ajili ya kuelekea sokoni kununua vitu kwa ajili ya chakula cha mchana wa siku ile. Muda haukupita sana mara alirejea mikononi mwake akiwa amebeba kuku na bata mzinga. Wakati mgeni alipomwona mwenyeji wake amebeba aina kwa aina za vitoweo alishangaa mno na kusema:" Kwa nini rafiki yangu unajisumbua kiasi hiki? Kwani mbali na mimi unatazamia kupata mgeni mwingine? Mwenyeji hakujibu kitu na bila kupoteza muda alianza kazi ya kuwasafisha na kuwakataka kuku na bata alionunua. Huku akiendelea na kazi yake sasa alimgeukia rafiki yake na kumwambia:" Hivi rafiki yangu kuna mgeni gani mwingine muhimu zaidi ya wewe. Vyote hivi ninaviandaa kwa heshima yako wewe sahibu yangu wa tangu na tangu." Mgeni alimjibu rafiki yake kwa kumwambia:" Lakini chakula hiki unachotayarisha ni kingi mno na ni sawa na kufanya israfu na ufujaji, wakati ni jana tu nilikula chakula kitamu mno na cha gharama kubwa. Wacha leo tule chakula cha kawaida tu". Hata hivyo mwenyeji alimkatiza mgeni wake na kusema:" Hata chakula hiki ninachokuandalia leo, mimi sioni kama ni chakula cha gharama, nasikitika na unisamehe kwa kushindwa kukutayarishia chakula kizuri zaidi ya hiki." Baada ya maandalizi ya chakula kukamilika, mkeka wa kupendeza ulitandikwa, na vyakula vya kila aina vikawekwa mbele ya mgeni. Mambo yaliendelea hivyo hivyo katika siku ya tatu na ya nne yake, kiasi cha kumfanya mgeni ahisi unyonge kwa kurimiwa kupita kiasi, na hivyo akaamua afunge virago haraka na kurudi mji alikotoka. Wakati wa kuagana ulipowadia mwenyeji alianza tena kumnasihi mgeni wake aendelee kubaki; mgeni kwa upande wake alisema ;"Hakika nimefurahia sana safari yangu na makazi yangu nyumbani kwako. Hata hivyo nitafurahi kama na wewe pia utakuja kunitembelea katika mji wetu na kuwa mgeni wangu nyumbani kwangu, ili nami nijaribu kukukirimu kama ulivyonikirimu".

Baada ya kupita siku na masiku, aliyekuwa mwenyeji, sasa aliamua kwenda kumtembelea rafiki yake aliyemkirimu hapo awali kwa ukarimu mkubwa. Ilikuwa safari ndefu, iliyochanganyika na machovu mengi, hata hivyo mwishowe akafika nyumbani kwa mwenyeji na rafiki yake mpenzi. Baada ya kukaribishwa ndani alianza kujisemea moyoni mwake:" Bila shaka rafiki yangu na yeye atagharamika na kunikirimu pengine zaidi ya vile nilivyomkirimu mimi". Baada ya marafiki wawili kujuliana hali, wakati wa chakula cha mchana uliwadia na mwenyeji akainuka kwa ajili ya kwenda kuandaa chakula. Kwa heshima na taadhima kitanga kilitandikwa, lakini kinyume na alivyofanyiwa na rafiki yake alipokwenda kumtembelea, mwenyeji wa sasa alimuandalia rafiki yake chakula cha kawaida tu. Hilo lilimstaajabisha mno mgeni wake, hata hivyo hakusema kitu. Wakala mpaka wakamaliza. Siku iliyofuata, mambo yakawa yale yale. Ingawa siku hiyo pia mgeni hakutamka chochote, lakini hakuweza kuficha mshangao wake, na hivyo mwenyeji wake akahisi kuwa hiyo ni fursa nzuri ya kumweleza ukweli wa mambo. Kwa upole na heshima alianza kwa kumwambia:" Rafiki yangu mpenzi, uzuri na ubora wa ukarimu ni kutofanya mambo ya fakhari na ya kupindukia. Mimi nilitaka niendelee kubaki nyumbani kwako kwa muda mrefu zaidi, lakini gharama kubwa ulizotumia kwa ajili ya kunikirimu, zilinifanya nione haya na kuhisi kuwa hupendi mimi niwe mgeni wa muda mrefu nyumbani kwako. Lakini mimi kutokana na kukutayarishia chakula cha kawaida kabisa, ninataka kukuonyesha kuwa hata kama utaendelea kuwepo nyumbani kwangu kwa mwaka mzima, basi mimi sitoona tabu hata kidogo, kwa sababu kila nilichonacho humu ndani mwangu nitakitumia kwa ajili ya kukukirimu wewe, na hilo wewe halitokufanya uhisi tabu hata kidog". Mwenyeji alinyamaza kidogo kisha akaendelea kusema:" Kwa maoni yangu nahisi kuwa, kama ambavyo tunashughulika mno kuyafikiria matumbo yetu kwa anuai za vyakula vya kimaada vya kunawirisha miili yetu, tujitutumie walau kidogo kufikiria chakula cha kuzinawirisha pia roho na nafsi zetu. Kwani baadhi ya wakati, sisi hupoteza saa chungu nzima kuandaa vyakula, ili milo yetu isiwe na upungufu au kasoro yoyote ile, hali ya kuwa tungekuwa tumefanya jambo la maana sana, lau tungeutumia nusu tu ya wakati huo, kwa ajili ya kujifunza mengi tusiyoyajua, yatakayozijenga nafsi na roho zetu". Kwa kumalizia nasaha zake mwenyeji alimnukulia mgeni wake maneno ya Imam Hassan Mujtaba as, mjukuu mtoharifu wa Bwana Mtume Muhammad saw pale aliposema:" "Nawastaajabu wale watu wanaofikiria maakuli yao, lakini hawajisumbui hata chembe kufikiria mambo ya kujifunza na kuzikuza akili zao".

********

Mpenzi msomaji sijui wewe uko kwenye kundi gani kati ya mawili haya katika suala la kugharamikia na kutumikia tumbo, mkabala na utumiaji wa walau fursa ndogo kati ya kubwa uipatayo, katika kuinawirisha na kuijenga nafsi yako. Kundi lolote lile utakalokuwemo, natumai kisa hiki kitakuwa kimekuelimisha walau kidogo juu ya suala hilo.

*******

Tafadhali msimulie na mwenzako.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …