Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 14 Septemba 2009 19:37

VISA VYA KUELIMISHA (9)

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

******

Hii ni sehemu nyingine ya Visa vya Kuelimisha. Lakini, kama nilivyotangulia kusema katika kisa kilichopita, si vile visa vya ngano za kubuni za alfu lela ulela, wala si vya Hadithi za kutunga, za Paukwa Pakawa au za matukio ya uvumi na tetesi ya sadiki ukipenda. Ni visa vya matukio ya kweli, yaliyotokea katika maisha ya viongozi halisi wa wanaadamu, yaani Manabii wa Mwenyezi Mungu. Visa ambavyo ni kigezo na ruwaza njema, kwa mimi na wewe, ya kuweza kubadilisha maisha yetu, na kutufanya tupate fanaka, na saada, ya leo hapa duniani, na kesho, huko akhera. Ni visa vya matukio yaliyojiri katika maisha ya waja wema wa Allah, ambao kwao wao, Quran, Suna za Bwana Mtume na mafundisho ya Maimamu, vilikuwa ni miongozo ya kufuata kivitendo, katika kila kipengele cha maisha yao, na si mambo ya kuishia kwenye uhodari wa kuyatamka kwa ghibu tu, na kuyasimulia kwa wengine. Ni matumaini yangu kwamba, si mimi na wewe tu mpenzi msikilizaji, bali hata wale wote tutakaowafikishia, ujumbe uliomo ndani ya visa hivi vya kuelimisha, watayachukua mafunzo yake, na kuyatoa katika sura ya nadharia, na kuyafanya kuwa ni somo la amali na vitendo, katika maisha yao ya kila siku.

*******

Miaka mingi mno iliyopita na katika mji mmoja alikuwepo mfua dhahabu aliyekuwa na jirani aliyekuwa mfinyanzi. Mfua dhahabu alikuwa mtu mpenda dunia na mali na kwa sababu hiyo alikuwa tayari kutumia njia yoyote ile ili kujizidishia na kujilimbikizia zaidi mali yake. Kila mtu alimjua mfua dhahabu kuwa ni mtu asiye na murua wala kujali watu; lakini kinyume chake mfinyanzi alikuwa mtu mchamungu, mpenda watu na mwenye kujituma, kiasi kwamba kila mtu aliyekuwa na shida hakusita kumwendea ili kumwomba msaada. Hali hiyo ilimkosesha raha mfua dhahabu na kumfanya akae peke yake na kujiuliza: "Hivi ni kitu gani hasa kinachomfanya mfinyanzi apendwe na watu kiasi hiki pamoja na kwamba hana mali wala utajiri kama wangu". Hilo lilimfanya mfua dhahabu awe na kinyongo na kuwasha moto wa husuda dhidi ya mfinyanzi ndani ya moyo wake. Siku na masiku yalipita, hata ikatokea siku moja zikasikika habari mjini kuwa kuna mwizi anasakwa kwa uvumba na udi. Mfua dhahabu akaona kuwa hiyo ni fursa nzuri ya kumkomoa mfinyanzi na kumaliza kinyongo alichonacho dhidi yake. Hivyo akawaambia askari wa mji kuwa yeye amemwona mwizi anayetafutwa akiingia kwenye nyumba ya mfinyanzi. Askari wakaivamia nyumba ya mfinyanzi, na baada ya kufanya upekuzi bila mafanikio wakaamua kumchukua mfinyanzi hadi korokoroni. Huko walimtikisa wakimtaka awaeleze alikompeleka mwizi. Licha ya kumaliza viapo vyote ili kuthibitisha kuwa hajui chochote kuhusu habari ya mwizi huyo, askari hawakuyaamini waliyoelezwa na mfinyanzi. Hivyo wakatumpa korokoroni. Lakini hazikupita siku nyingi ila mwizi aliyekuwa akisakwa alitiwa mbaroni na kubainika kuwa masikini mfinyanzi hakuwa na hatia yoyote. Hivyo yeye akaachiwa huru na badala yake mfua dhahabu mzushi akatoleshwa faini. Ingawa siku nyingi zilipita lakini sio tu moto wa husuda, uadui na chuki wa mfua dhahabu dhidi ya mfinyanzi haukuzimika, bali ulizidi kuwaka na kukolea ndani ya moyo wake hasa baada ya kuona kuwa imani na mapenzi ya watu kwa mfinyanzi yanaongezeka zaidi na zaidi. Moto huo wa husuda na uadui ulikuwa ukizidi kuiharibu roho na akili ya mfua dhahabu, mpaka ukamfanya ajiwe na wazo baya la kutaka kumwua mfinyanzi. Hivyo akatayarisha sumu na kumtafuta kijana mmoja, akamshawishi na kumpa sarafu mia moja za dhahabu ili ahakikishe anamuua mfinyanzi kwa sumu. Siku ya kutekeleza njama hiyo ikawadia, na mfua dhahabu akawa amekaa akisubiri kwa hamu kubwa kusikia sauti za vilio na maombolezo kutoka kwenye nyumba ya jirani yake mfinyanzi. Lakini hilo alilotarajia halikutokea, na badala yake muda si muda akamwona mfinyanzi akitoka nyumbani kwake mzima wa afya na kuelekea kibaruani kwake. Mfua dhahabu alipigwa na butwaa, na hivyo bila kupoteza muda akaanza kumsaka yule kijana ili kutaka kujua kulikoni. Hata hivyo baada ya kuuliza uliza alibaini kwamba sio tu kijana yule hakumpa sumu yoyote mfinyanzi lakini pia ametoroka na sarafu zote mia moja alizompa kama ujira wa kazi yake. Habari hiyo ilimtibua mno mfua dhahabu, kiasi cha kumtia maradhi ambayo waganga na waganguzi walishindwa kuyapatia dawa ya kuyaponya. Na sababu ni kuwa chanzo cha maradhi hayo hakikuwa kirusi wala kimelea chochote, bali ni moto wa husuda na uadui ndio uliokuwa ukiiteketeza nafsi yake. Dunia ilimpa kisogo mfua dhahabu kiasi kwamba hata mke na watoto wake walimkimbia akabaki peke yake. Habari za kuumwa kwake zilimfikia jirani yake mafinyanzi, ambaye kinyume na matarajio ya mfua dhahabu, aliamua kutayarisha chakula kizuri na kwenda kumjulia hali jirani yake huyo.

Wakati mfua dhahabu alipomwona mfinyanzi alipatwa na tahayuri isiyoelezeka. Hakuweza hata kutikisa ulimi wake kutamka chochote au mkono wake kuashiria kitu. Ama mfinyanzi, yeye alimjongelea jirani yake, na kwa huruma na upendo akamjulia hali na kumwambia:" Haki ya ujirani imenifanya nije kukujuilia hali". Kisha akaendelea kusema:" Mimi nina habari ya yoote yaliyopita; hata yule kijana uliyempa sumu, alipokuja na kunieleza kila kitu alinishauri niuhame huu mji kwa kuwa maisha yangu yatakuwa hatarini. Lakini kwa kuwa nilikuwa sijakata tamaa na rehma za Mwenyezi Mungu, kila siku nilikuwa nikikuombea dua, kwa matumaini kwamba asaa moyo wako utabadilika ,na kufuta uadui na husuda uliyokuwa nayo dhidi yangu. Mfua dhahabu alianza kutokwa na machozi. Ama mfinyanzi aliendelea na kumwasa jirani yake kwa kumwambia:" Tambua ewe ndugu yangu kuwa, uhasidi na uadui ni moto unaoanza kumwakia mtu mwenyewe. Kama ni hivyo, si bora tuishi kwa kupendana katika kipindi hiki kifupi cha maisha ya kupita ya dunia, ili tuweze kutajwa kwa wema baada ya kuondoka hapa duniani. Unajua sababu ya mimi kupendwa na watu? Acha nikunukulie hadithi moja ili uitambue siri ya jambo hilo. Siku moja Imam Sajjad as, mmoja wa wajukuu watoharifu wa Bwana Mtume Muhammad saw alimwelekea mmoja wa masahaba zake aliyekuwa akiitwa Zuhri, ambaye alionekana amejiinamia sana kutokana na hisia kuwa kila mtu anamtazama yeye kwa jicho la husuda. Imam Sajjad alimwambia sahaba wake huyo kuwa: "Ewe Zuhri, kuna ubaya gani ikiwa utawachukulia watu wengine kuwa ni watu wa aila yako na jamaa zako. Wale ambao ni wazee ukawachukulia kuwa ni kama baba zako, wa chini ya rika lako ukawafanya kuwa ni sawa na wadogo zako, na wale wa rika lako ukawachukulia kuwa ni ndugu zako. Katika hali hiyo utakuwa tayari kumfanyia dhulma yeyote kati yao? Usisahau kuwa watu humpenda zaidi yule mtu ambaye kheri zake huwafikia zaidi watu, bila ya yeye kutaka kitu kwao. Kama utafuata njia hii maishani mwako, dunia itakuwa ya raha kwako, na utapata marafiki wengi." Maneno ya mfinyanzi yalimwathiri mno mfua dhahabu . Uso wake ulionyesha wazi kuwa amejuta kwa yote aliyomtendea jirani yake. Alimwomba radhi na kutoa ahadi kwa Mwenyezi Mungu, kuwa kuanzia hapo ataishi na wenzake kwa upendo na huruma, badala ya chuki, husuda, uadui na hasama.

*******

Tafadhali msimulie na mwenzako

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …