Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 13 Septemba 2009 22:26

VISA VYA KUELIMISHA (8)

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

******

Hii ni sehemu nyingine ya Visa vya Kuelimisha. Lakini, kama nilivyotangulia kusema katika kisa kilichopita, si vile visa vya ngano za kubuni za alfu lela ulela, wala si vya Hadithi za kutunga, za Paukwa Pakawa au za matukio ya uvumi na tetesi ya sadiki ukipenda. Ni visa vya matukio ya kweli, yaliyotokea katika maisha ya viongozi halisi wa wanaadamu, yaani Manabii wa Mwenyezi Mungu. Visa ambavyo ni kigezo na ruwaza njema, kwa mimi na wewe, ya kuweza kubadilisha maisha yetu, na kutufanya tupate fanaka, na saada, ya leo hapa duniani, na kesho, huko akhera. Ni visa vya matukio yaliyojiri katika maisha ya waja wema wa Allah, ambao kwao wao, Quran, Suna za Bwana Mtume na mafundisho ya Maimamu, vilikuwa ni miongozo ya kufuata kivitendo, katika kila kipengele cha maisha yao, na si mambo ya kuishia kwenye uhodari wa kuyatamka kwa ghibu tu, na kuyasimulia kwa wengine. Ni matumaini yangu kwamba, si mimi na wewe tu mpenzi msikilizaji, bali hata wale wote tutakaowafikishia, ujumbe uliomo ndani ya visa hivi vya kuelimisha, watayachukua mafunzo yake, na kuyatoa katika sura ya nadharia, na kuyafanya kuwa ni somo la amali na vitendo, katika maisha yao ya kila siku.

*******

Kitanga kidogo cha chakula cha watoto mafakiri kilikuwa kimetandikwa chini ya kivuli cha mitende ya mji wa Madina. Watoto hao waliokuwa wamechangamka na wenye furaha walikizunguka kitanga chao hicho, na mkono kwa mkono wakawa wanakula chao cha kinyonge cha vipande vya mikate mikavu na maganda ya mbatata yaliyokaushwa. Sauti ya upepo mwanana uliokuwa ukivuma na kuyasukuma matawi na majani ya mitende huku na huko, ikichanganyika na sauti za vicheko za watoto hao pamoja na zile za ndege waliokuwa wakizunguka huku na kule angani zilitoa mandhari yenye haiba na uzuri wa aina yake, uliomfanya kila aliyekuwa akipita njia kando ya watoto hao masikini, aihusudu na kuionea choyo dunia ya watoto hao ambao hawakuonyesha hata chembe ya ghamu na huzuni kwa sababu ya umasikini wao. Hata hivyo hakuna hata mmoja kati ya wapita njia hao aliyekuwa tayari kukaribia kitanga cha watoto hao na kula chakula pamoja nao. Hata hivyo watoto hao hasa yule aliyekuwa mdogo kabisa kati yao aliyekuwa akiitwa Said hakuacha utaratibu wao huo wa kumwalika kwenda kula pamoja nao kila aliyekuwa akipita njia hiyo. Siku moja walipokuwa wameshatandika kitanga chao tayari kujumuika pamoja kwa ajili ya chakula cha mchana, Said na wenzake walimwona kwa mbali mtu aliyepanda farasi akielekea upande wao. Wakati alipowakaribia, mmoja kati ya watoto alisema: "Mie namjua Bwana huyu! Baba yangu amesema hakuna mtu yeyote Madina aliye mfano wake. Yeye ni mwana wa Mtume". Mtoto mwingine alidakia na kusema: "Mimi nna hakika kama tutamkaribisha hatokubali kula nasi". Wote walinyamaza kimya. Said aliwatizama wenzake kisha akamsogelea yule bwana, na kwa sauti nzuri ya kitoto akamwambia:" Sayidi yangu! Sisi tutafurahi kama utakuja kula na sisi". Bwana mpanda farasi hakuwa mtu mwingine bali ni Imam Hassan Mujtaba as, mjukuu mpenzi wa Bwana Mtume Muhammad saw. Alijibu ombi la Said kwa tabasamu. Alimshika hatamu farasi wake na kwenda kumfunga kwenye kiguzo cha mtende. Wale watoto ambao walikuwa wameduwaa wakiwa hawaamini macho yao kwa kukubaliwa mwaliko waliotoa, walikimbilia kwenye kitanga chao cha chakula na wakaanza kuvikusanya haraka haraka vipande vikavu vya mikate na maganda ya mbatata na kuvitupilia mbali. Wakati Imam Hassan aliporudi kwenye mjumuiko wa watoto hao, wote kwa pamoja walitaka kuinuka. Said alikitupia jicho kitanga cha chakula kilichokuwa takriban kitupu vikiwa vimesalia vipindi viwili vitatu tu vya mikate mikavu. Aliinamisha uso chini kwa aibu. Imam Hassan aliwataka watoto wakae. Kisha yeye mwenyewe akapinda goti na kuketi kando ya Said. Alichukua kipande kimoja cha mkate, na wakati yeye anaendelea kula, Said alisema: "Ingekuwa vizuri zaidi kama ungekuja mapema". Imam alimtazama mtoto mmoja mmoja kwa jicho la huruma kisha akainuka na kuwaambia: "Sasa nyote inukeni na twendeni kwangu ili muwe wageni wangu". Watoto hawakuyaamini masikio yao, kusikia kwamba shakhsiya mtukufu wa Madina anawaalika nyumbani kwake. Wakati Imam Hassan alipoinuka na kumshika mkono Said ili waanze safari yao mtoto huyo alijaribu kuificha sehemu iliyoraruka ya nguo aliyokuwa amevaa. Imam na Said walitangulia mbele na watoto waliobakia walifuata nyuma. Wakati Imam Hassan na wageni wake walipowasili nyumbani, watoto hao walichukuliwa hadi kwenye chumba kimoja ambacho dirisha lake lilikuwa linafungukia uani. Walimsikia Imam Hassan akiwaambia wajakazi wake wapike kile chakula kitamu kabisa kwa ajili ya wageni wake. Watoto hawakuweza kutulia chumbani kwa furaha, kwani muda si muda harufu nzuri ya chakula kilichokuwa kikiandaliwa ilihanikiza kwenye anga ya chumba kizima. Muda si mrefu baadaye kitanga cha rangi mbali mbali kilitandikwa chumbani, na watoto wakakusanyika pamoja kula shibe yao chakula kitamu walichotayarishiwa. Baada ya kula walikaa kitako kumsubiri Imam Hassan. Baada ya kupita kama saa moja hivi Imam alirejea akiwa amefuatana na mtu aliyekuwa ameshika kikapu kikubwa mkononi. Walipomwona Imam Hassan watoto waliinuka kwa heshima na kumwamkia kwa pamoja yeye na mgeni aliyekuja naye. Yule mtu ambaye alikuwa ni fundi mshoni alianza kutoa nguo za kupendeza za rangi mbali mbali zilizokuwemo ndani ya kikapu chake. Imam Hassan alitabasamu, kisha akamwita Said aliyekuwa mdogo zaidi kati ya watoto wote. Fundi mshoni alitoa nguo moja ya rangi ya samawati na kumgeza nayo Said. Alipoona kuwa inamfaa alimtaka aende kwenye kona ya chumba na kubadilisha na ile ya mararu aliyokuwa amevaa. Alifanya vivyo hivyo kwa watoto waliobakia. Kwa hakika watoto wote walifurahi sana. Kwa moyo wa upendo na huruma Imam Hassan aliagana nao na kuwataka wasiache kwenda kumtembelea tena siku nyingine. Watoto walianza kuondoka mmoja mmoja na Said akawa ndiye wa mwisho kufanya hivyo. Imam Hassan alimwekea mkono kichwani na kuzipuna nywele zake kwa upendo kisha akaagana naye. Ama yule fundi mshoni ambaye alikuwa akiwaangalia kwa dirishani watoto wale waliokuwa wakienda zao huku wakiwa na furaha tele, alimgeukia Imam Hassan na kumwambia:" Ee Sayyid yangu hakika umewafanyia wema mkubwa watoto hawa. Imam ambaye kwa uso wa bashasha alikuwa akiendelea kuwapungia mkono watoto wale kuwaaga alimwambia fundi mshoni:" Ukarimu wa watoto hawa kwangu ulikuwa mkubwa zaidi, kwani wao walinipa kile chote walichokuwa nacho, hali ya kuwa mimi nina zaidi ya kile nilichowapa wao". Mshoni alitikisa kichwa tu kuajabia ukarimu wa Imam Hassan. Alibeba kikapu chake, akapokea malipo ya nguo alizouza, na kuagana na Imam Hassan.

*******

Tafadhali msimulie na mwenzako.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …