Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 13 Septemba 2009 22:22

VISA VYA KUELIMISHA (7)

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

******

Hii ni sehemu nyingine ya Visa vya Kuelimisha. Lakini, kama nilivyotangulia kusema katika kisa kilichopita, si vile visa vya ngano za kubuni za alfu lela ulela, wala si vya Hadithi za kutunga, za Paukwa Pakawa au za matukio ya uvumi na tetesi ya sadiki ukipenda. Ni visa vya matukio ya kweli, yaliyotokea katika maisha ya viongozi halisi wa wanaadamu, yaani Manabii wa Mwenyezi Mungu. Visa ambavyo ni kigezo na ruwaza njema, kwa mimi na wewe, ya kuweza kubadilisha maisha yetu, na kutufanya tupate fanaka, na saada, ya leo hapa duniani, na kesho, huko akhera. Ni visa vya matukio yaliyojiri katika maisha ya waja wema wa Allah, ambao kwao wao, Quran, Suna za Bwana Mtume na mafundisho ya Maimamu, vilikuwa ni miongozo ya kufuata kivitendo, katika kila kipengele cha maisha yao, na si mambo ya kuishia kwenye uhodari wa kuyatamka kwa ghibu tu, na kuyasimulia kwa wengine. Ni matumaini yangu kwamba, si mimi na wewe tu mpenzi msikilizaji, bali hata wale wote tutakaowafikishia, ujumbe uliomo ndani ya visa hivi vya kuelimisha, watayachukua mafunzo yake, na kuyatoa katika sura ya nadharia, na kuyafanya kuwa ni somo la amali na vitendo, katika maisha yao ya kila siku.

*******

Kama ilivyo kila siku, sauti za kelele za watoto waliokuwepo kwenye chuo cha quran zilikuwa zikivuma na kusikika kutokea chuoni hapo. Na kama ilivyokuwa kawaida yao watoto hao wote walinyamaza kimya na kutulia tuli mara tu walipomwona mwalimu wao anaingia chuoni hapo. Kuwepo kwa mwalimu huyo kulikuwa kukiipa anga ya chuo mandhari ya kimaanawi ya aina yake. Upole na moyo wake wa upendo na huruma, viliwapa uchangamfu maalumu watoto. Mapenzi yake kwa wanafunzi wake yaliziteka nyoyo zao na kutoa mvuto mkubwa kwao; kiasi kwamba shauku na hamu ya kujifunza ilimu na maarifa ya wanafunzi, ilikuwa haina kifani.

Siku moja wakati mwalimu huyo aliporudi nyumbani kwake akiwa amechoka taabani, alikuta amepata ugeni wa kaka yake aliyekwenda kumtembelea. Kaka wa mwalimu alikuwa mtu tajiri na mwenye kipato, lakini alikuwa hakusoma, naye kila mara alikuwa akimlaumu ndugu yake kwa nini ameamua kufanya kazi ya ualimu wa chuo. Mwalimu alimsalimia kaka yake, lakini badala ya kujibu salamu aliyotolewa, kaka mtu kama ilivyokuwa kawaida ya kila anapokutana na ndugu yake, alianza kukariri lawama zake, ambazo mwenyewe alizipa jina la nasaha za kumwonea uchungu nduguye akasema:" Hebu niambie ndugu yangu, mpaka lini utaendelea kufanya kazi hii isiyo na faida? Hebu fanya kuitupia jicho kidoogo tu hali yako ya maisha. Hutaki wewe kuboresha hali yako kwa kuwa na pesa na mtaji utakaowezesha aila yako iishi maisha ya raha mustarehe! Mimi sina ilimu yoyote, lakini kila safari ninayokwenda napata pesa na kitita cha mtaji kinachoniwezesha kuishi maisha mazuri na ya raha, bukheri wa afya.

Mwalimu ambaye masikio yake yalikuwa yameshazoea kusikia kauli hizo za lawama kutoka kwenye kinywa cha kaka yake, aliamua kunyamaza kimya kwa heshima ya kaka yake na ili lisije likamponyoka neno ambalo halitomfurahisha kaka mtu. Baada ya kutamka aliyoyataka, mgeni wa mwalimu aliondoka akaenda zake. Hapo mwalimu aligutuka kugundua kuwa machozi njia mbili mbili yalikuwa yakimbubujika mkewe. Kwa kushuhudia hali ya huzuni na majonzi aliyokuwa nayo mkewe mwalimu alijaribu kumtuliza kwa kumwambia: "Mola mwenye rehma na huruma katu hawasahau waja wake; mimi naona fakhari kwa kazi ninayofanya na ninaipenda mno. Ni kweli maisha yetu ni ya kawaida na ya kinyonge lakini elewa kuwa moyo na kifua changu kimehifadhi hazina na dafina ya elimu yenye thamani kubwa ambayo ikilinganishwa na utajiri alionao kaka yangu, utajiri huo si lolote si chochote. Mimi ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa rehma zake za kuniwezesha kukifunza kile nikijuacho." Mke mtu kwa upande wake alijibu: Mimi kwa kweli nimechoshwa na lawama zisizokwisha za kaka yako. Yeye kila siku kazi yake ni kujifakharisha kwa mali na utajiri wake, lakini wewe humjibu chochote.

Mwalimu alimtazama mkewe kwa jicho la huruma na kumwambia: Mke wangu la azizi, chochote nitakachomweleza kaka yangu hakimwathiri kitu, kwani akili yake yote imeshughulishwa na mali na utajiri, wala hafikiri chochote ghairi ya pesa na mambo ya kimaada tu. Hata hivyo ukweli bado unabaki kuwa matunda ya kazi ninayoifanya mimi hayawezi kulingana hata chembe na yale aliyonayo yeye. Kwani kila neno moja ninalowafunza wanafunzi wangu, huwa mithili ya kurunzi inayotoa nuru na kuwaangazia kwenye dunia yao ya giza la ujinga." Maneno hayo ya mwalimu yaliweza kupoza kidogo machungu yaliyokuwa yakifukuta ndani ya moyo wa mkewe.

Kama ilivyokuwa desturi yake, siku iliyofuatia mwalimu aliondoka nyumbani kwake kwa hamu na uchangamfu wake ule ule wa kawaida na kuelekea chuoni kwa ajili ya kwenda kuwasomesha watoto quran na mambo mengine ya dini. Ilisadifu siku hiyo mmoja wa wanafunzi wake alisoma quran kwa sauti ya kuvutia mno, na wakati huo alimu mmoja akawa anapita karibu na chuoni hapo. Alimu alivutiwa mno na kisomo hicho cha quran, hivyo akawauliza aliofuatana nao:" Sauti hii inatokea wapi?". Akajibiwa kuwa, mahali hapa kuna mwalimu anayesomesha watoto wadogo elimu mbali mbali za dini pamoja na quran tukufu. Aliisifia mno kazi inayofanywa na mwalimu yule na kuamua kwenda nyumbani kwake ambako alichukua zawadi yenye thamani kubwa kwa lengo la kwenda kumtunukia mwalimu yule. Baada ya saa chache alifika chuoni hapo naye mwalimu akaenda kumlaki kwa heshima na kuamkiana naye. Alim alimwambia mwalimu: "Tambua kuwa kazi unayoifanya ni yenye kheri kubwa mno. Mimi nimeamua kukutunukia zawadi hii kutokana na juhudi zako unazozifanya kwa ikhlasi. Kisha akaendelea kumuusia kwa kumwambia:" Waelimishe wanafunzi wako kuwa elimu huweza kumfikisha mwanadamu kwenye saada, pale inapoweza kumjenga pia mwanadamu kimaadili na kiakhlaqi. Baada ya kumuusia hayo, Alim alimnukulia mwalimu hadithi ya Bwana Mtume saw aliposema: "Mwalimu anayewafunza waja wa Mwenyezi Mungu njia za kheri na saada, viumbe wa ardhini na walioko angani wanamtakia mtu huyo maghufira kwa Mwenyezi Mungu. Tambueni kuwa hakuna hidaya yenye thamani kubwa zaidi, kama mtu kumfunza ndugu yake hikma itakayomuongoza kuifikia njia ya Mwenyezi Mungu na kuokoka na upotofu". Machozi ya furaha yalimbubujika mwalimu, akamshukuru Mwenyezi Mungu, na kwa furaha akaichukua tunu yenye thamani kubwa aliyopewa na Alim hadi nyumbani kwenda kumtunukia mkewe.

*******

Tafadhali msimulie na mwenzako.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …