Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 13 Septemba 2009 22:20

VISA VYA KUELIMISHA (6)

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

******

Hii ni sehemu nyingine ya Visa vya Kuelimisha. Lakini, kama nilivyotangulia kusema katika kisa kilichopita, si vile visa vya ngano za kubuni za alfu lela ulela, wala si vya Hadithi za kutunga, za Paukwa Pakawa au za matukio ya uvumi na tetesi ya sadiki ukipenda. Ni visa vya matukio ya kweli, yaliyotokea katika maisha ya viongozi halisi wa wanaadamu, yaani Manabii wa Mwenyezi Mungu. Visa ambavyo ni kigezo na ruwaza njema, kwa mimi na wewe, ya kuweza kubadilisha maisha yetu, na kutufanya tupate fanaka, na saada, ya leo hapa duniani, na kesho, huko akhera. Ni visa vya matukio yaliyojiri katika maisha ya waja wema wa Allah, ambao kwao wao, Quran, Suna za Bwana Mtume na mafundisho ya Maimamu, vilikuwa ni miongozo ya kufuata kivitendo, katika kila kipengele cha maisha yao, na si mambo ya kuishia kwenye uhodari wa kuyatamka kwa ghibu tu, na kuyasimulia kwa wengine. Ni matumaini yangu kwamba, si mimi na wewe tu mpenzi msikilizaji, bali hata wale wote tutakaowafikishia, ujumbe uliomo ndani ya visa hivi vya kuelimisha, watayachukua mafunzo yake, na kuyatoa katika sura ya nadharia, na kuyafanya kuwa ni somo la amali na vitendo, katika maisha yao ya kila siku.

*******

Ilikuwa ni kati kati ya mchana; na kama ilivyokuwa katika siku zilizopita, soko la mji wa Kufa lilikuwa limefurika umati mkubwa wa watu waliokuwa wakiingia huku na kutokea kule, kwa minajili ya kujinunulia bidhaa mbali mbali za mahitaji yao ya kila siku. Katika umati huo mkubwa wa watu, alionekana mtu mmoja wa tambo mwenye maungo yaliyokakamaa, ambaye maumbile yake yalitoa mvuto kwa watu wengi waliokuwepo sokoni hapo wakati huo.

Huku akitembea kwa hatua za haraka haraka, bwana huyo ambaye uso wake ulikuwa umesawijika kwa kijua kikali kilichokuwa kimempiga, alikuwa ameshaanza kuliacha soko la mji wa Kufa, pale ghafla mmoja wa wafanyabiashara wa soko hilo aliyekuwa ameketi mbele ya kiduka chake, alipomwona bwana huyo; na kwa ajili ya kutaka kuwachekesha maswahibu zake waliokuwa kando yake, akaamua kumfanyia vitimbi mpita njia huyo kwa kumvurumizia vijiwe na vidongo alivyokuwa navyo mkononi mwake. Bwana mpita njia aligeuka na kumtizama mfanya biashara huyo. Lakini bila ya kuonyesha hisia zozote za kuchukizwa na kitendo hicho alishika njia na kuendelea na safari yake.

Ama wale masahibu wa mfanya biashara huyo sio tu hawakuchekeshwa na kitendo kile cha utovu wa adabu, lakini pia walionyesha kutafirishwa na kitendo cha bwana yule, na kwa pamoja wakamtolea macho na kumuuliza: "Unamjua ni nani yule bwana mpita njia uliyemvujia heshima?" Huku akionyesha kutojali kwa kitendo alichofanya, mfanya biashara alijibu:" Simjui asilani, kwani yeye ni nani, si mpita njia tu kama wapita njia wengine chungu nzima, wanaopita mbele yetu hapa kila siku?" Mmoja wa sahibu zake aliyeonekana ameghadhibika mno alimjibu kwa kumwambia:" Ama wewe mpumbavu! Ajabu kuwa humjui mpita njia yule! Ole wako basi kama hujui ni nani yule uliyemvunjia heshima, yule ni Malik Ashtar, jemadari maarufu wa Uislamu, mtu ambaye kutokana na ushujaa wake na kujitolea kwake muhanga katika medani za Jihadi, ndio maana sisi leo tuko na neema hii ya Uislamu. Mfanya biashara yule aligutuka na kushtuka kwa kusikia jina la Malik Ashtar. Rangi ya uso wake ilibadilika ghafla kwa khofu na tahayuri. Alianza kuwaza na kuwazua amtafute nani wa kumwombea, au afanye nini ili aweze ridhaa ya Malik. Alibaki akijisemea mwenyewe:" Ah, ujinga gani huu nlofanya mimi! Nimekwenda kumwudhi jemadari wa Uislamu!? Bila shaka atanipa adhabu kali tu.

Bila kufanya ajizi, mfanya biashara huyo aliamua kumkimbilia Malik, akiwa tayari kufanya lolote lile liwalo alimradi tu Malik amwie radhi kwa aliyomtendea. Alianza kutimua mbio kumtafuta sahaba huyo, akikata kichochoro hiki na kupenyea kwenye kichochoro kingine cha mji wa Kufa hadi mwishowe akamwona Malik Ashtar. Wakati huo Malik alikuwa anamaliza kukata kichochoro cha mwisho kinachoishia kwenye msikiti wa Kufa. Mfanya biashara naye aliamua kumfuata Malik hadi msikitini bila kumshtua.

Moyo ulikuwa ukimdunda kwa kasi mfanyabiashara yule, ambaye katika lahadha hiyo hakuweza kuinua ulimi na kutamka chochote kile. Bila kujua kinachoendelea nyuma yake Malik alianza kusali, naye mfanya biashara akabaki amemkodolea macho akimsubiri amalize sala yake. Baada ya Malik kumaliza kusali na kuvuta uradi, aliinuka pale alipokuwa. Hapo mfanya biashara alimsogelea, akamwangukia miguuni, na kwa sauti ya kitetemeshi alimwambia: "Ee Malik Ashtar, mimi nimefanya ujinga; kwani, kwa sababu ya kutokutambua, nimekuvunjia heshima. Nakuomba kwa hisani yako unisamehe, Wallahi sikujua kama ni wewe, ambaye ni mtu mwenye kuheshimika.

Malik Ashtar aliinama na kumwinua taratibu mfanya biashara yule na kumshika mabegani. Macho ya mfanya biashara yalipogongana na yale ya Malik, bwana yule alishindwa kumtazama usoni jemedari wa Uislamu kwa soni na hali ya aibu iliyompata. Malik alimtuliza na kumpoza mfanya biashara kwa kumwambia:" Wallahi mimi nimekuja msikitini hapa kwa sababu yako wewe tu; kwa sababu nilijua kwamba, ni kutokana na ujinga ndio maana unawafanyia maudhi watu bure.

Nimesikitishwa na hali yako, hivyo nimeamua kuja msikitini ili kukuombea dua, kwa kumwomba Mwenyezi Mungu akuongoze kwenye njia ya sawa na kukusamehe madhambi yako. Aliposikia maneno hayo ya Malik Ashtar, na kujishuhudia kwa macho yake moyo wa usemehevu na upendo wa jemadari huyo wa uislamu, mfanya biashara alizidi kuingiwa na tahayuri; akamshukuru Malik na kurudi dukani kwake. Huko aliwakuta marafiki zake wakimsubiri kwa hamu, kutaka kujua yaliyojiri kati yake na Malik Ashtar. Alipowasimulia yale yote yaliyojiri huko kwenye msikiti wa Kufa, wote kwa umoja wao walimsifu na kumtukuza Malik na kisha mmoja wao akawakumbukusha wenzake hadithi ya Bwana Mtume Muhammad saw pale aliposema: "Wasemeheni wenzenu wanapokukoseeni, kwani kusamehe huzidisha heshima na izza ya mtu. Sameheaneni ili Mwenyezi Mungu akupeni izza.

 

*******

Tafadhali msimulie na mwenzako

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …