Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 13 Septemba 2009 22:19

VISA VYA KUELIMISHA (5)

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

******

Hii ni sehemu nyingine ya Visa vya Kuelimisha. Lakini, kama nilivyotangulia kusema katika kisa kilichopita, si vile visa vya ngano za kubuni za alfu lela ulela, wala si vya Hadithi za kutunga, za Paukwa Pakawa au za matukio ya uvumi na tetesi ya sadiki ukipenda. Ni visa vya matukio ya kweli, yaliyotokea katika maisha ya viongozi halisi wa wanaadamu, yaani Manabii wa Mwenyezi Mungu. Visa ambavyo ni kigezo na ruwaza njema, kwa mimi na wewe, ya kuweza kubadilisha maisha yetu, na kutufanya tupate fanaka, na saada, ya leo hapa duniani, na kesho, huko akhera. Ni visa vya matukio yaliyojiri katika maisha ya waja wema wa Allah, ambao kwao wao, Quran, Suna za Bwana Mtume na mafundisho ya Maimamu, vilikuwa ni miongozo ya kufuata kivitendo, katika kila kipengele cha maisha yao, na si mambo ya kuishia kwenye uhodari wa kuyatamka kwa ghibu tu, na kuyasimulia kwa wengine. Ni matumaini yangu kwamba, si mimi na wewe tu mpenzi msikilizaji, bali hata wale wote tutakaowafikishia, ujumbe uliomo ndani ya visa hivi vya kuelimisha, watayachukua mafunzo yake, na kuyatoa katika sura ya nadharia, na kuyafanya kuwa ni somo la amali na vitendo, katika maisha yao ya kila siku.

*******

Yalikuwa ni majira ya mchana, ya siku moja ya msimu wa joto, ambapo joto la jua kali lenye kuunguza lilikuwa likifukuta kwenye mashamba na konde zilizokuweko kwenye viunga vya mji wa Madina. Ilisadifu kuwa siku hiyo Muhammad bin Munkadir, aliamua kwenda kutembelea viunga hivyo. Muhammad bin Munkadir alikuwa ni mtu mkithirishaji wa ibada aliyeamua pia kwa namna alivyoamini yeye mwenyewe kuipa mgongo dunia. Akiwa katika pitapita zake hizo katika viunga vya mji wa Madina huku akimdhikiri na kumsabihi Mwenyezi Mungu, ghafla kwa mbali alimwona mtu mmoja katika moja ya mashamba hayo aliyekuwa ameshughulika na kazi ya kung'oa na kusafisha magugu katika shamba lake. Wakati Muhammad bin Munkadir alipomwona mtu huyo akimiminikwa na jasho kutokana na kazi na joto la jua kali lililokuwa likiwaka, aliwaza na kujisemea rohoni mwake: "Ah ajabu hii, nani huyu anayejitesa nafsi yake kwa kazi za kidunia katika joto kali kama hili. Kwa sababu tu ya kutaka mali ameamua kujianika kwenye jua kali linalounguza kama hili, tena basi, katika wakati wa mchana kama huu! Muhammad bin Munakadir alionelea ni bora akampe nasaha mtu huyo. Lakini wakati alipozidi kujongea na kumkarabia mtu huyo, Munkadir alipigwa na butwaa alipotambua kuwa mtu huyo alikuwa ni Imam Muhammad ibn Ali, Baqir (as) mmoja wa watu wa kizazi cha nyumba ya Bwana Mtume Muhammad (saw). Akiwa bado ameduwaa, Muhammad bin Munkadir alijisemea tena rohoni mwake: "Kitu gani kimemfanya mtu mtukufu kama huyu kuja hapa kujishughulisha na mambo ya dunia? Kwa hali hii inanilazimu nimpe nasaha ili awache mwenendo huu". Baada ya kumfikia Imam Baqir pale alipokuwa, Munkadir alimsalimia, naye Imam Baqir kwa sauti ya kuhema aliitikia salamu iliyotolewa na Muhammad bin Munkadir. Munkadir alianza kwa kusema:" Hivi kweli inalaiki kwa mtu mtukufu kama wewe uje hapa kwa sababu ya kuhangaikia dunia? Tena basi katika hali kama hii ya jua linalounguza na joto kali linalofukuta? Ndiyo kusema dunia imekuwa muhimu na yenye thamani kiasi hiki mpaka wewe ulazimike kwa ajili yake kuvumilia mateso na machungu chungu nzima? Wakati Muhammad Munkadir anatoa nasaha zake hizo, Imam Baqir alitulia tuli na kusikiliza yale yaliyokuwa yakitoka kinywani mwa Bwana huyo. Wakati Munkadir alipotambua kuwa Imam Baqir ametulia na kusikiliza anayoyasema, alizidi kupata ujasiri wa kuendelea na nasaha zake. Hapo alihoji kwa kusema:" Ni nani aliye na habari ya mauti yake? Nani ajuaye atakufa wakati gani? Pengine hivi sasa hivi inaweza ikawa ndiyo saa yako ya mauti. Mungu aepushie mbali; lakini kama imeshaandikwa kuwa hivyo, na ukafa ukiwa katika hali hiyo, utakuwa na hali gani? Waislamu watasema nini? Kiongozi wao ameaga dunia, akiwa ameshughulika na kazi ya ukulima shambani? Hapana! Hailaki asilani kwa mtu kama wewe, kuja kujishugulisha na dunia katika siku ya joto kama hili, ukajitia wewe mwenyewe na kuwatia na wengine kwenye tabu na usumbufu". Muhammad bin Munkadir alikuwa akiongea kwa ghururi; pamoja na hayo Imam Baqir aliendelea kusikiliza maneno yake kwa makini. Imam alimwacha Munkadir aseme yote atakayo, mpaka alipomaliza na kunyamaza kimya, hapo alimuelekea na kuanza kumjibu kwa kumwambia:" Kama nitafikwa na mauti katika hali hii niliyonayo, elewa kuwa nitakuwa nimeaga dunia, nikiwa katika hali ya kufanya ibada, na kutimiza wajibu wangu; kwa sababu, kufanya kazi ni sehemu ya taa na kudhihirisha uja wangu kwa Mola Mwenyezi. Hivi wewe unadhani ibada inaishia kwenye dhikri, dua na sala tu? Ikiwa mimi nitajishughulisha na dhikri na dua tu, bila kufanya kazi kwa ajili ya kukidhi mahitaji yangu na kuendesha maisha yangu, nitalazimika kukuonyooshea mkono wewe na mfano wa wewe. Mimi ninakwenda kuhangaika kutafuta riziki yangu ya halali, ili nisiwe mhitaji kwa wengine. Hofu yangu mimi, ni pale yataponikuta mauti, nikiwa katika hali ya kumwasi Mwenyezi Mungu na kukhalifu amri zake. Lakini mimi ninapokuwa nikifanya kazi, huwa nimo katika hali ya kutii amri ya Mola wangu, ambaye ameniwajibishia kufanya kazi na kujituma, kwa ajili ya kutafuta riziki yangu. Maneno ya Imam Muhammad Baqir yalimtia tahayuri kubwa Muhammad bin Munkadir, ambaye alibaki akijisemea: "Ah kumbe nilikuwa nikifanya makosa! Mwenyewe nilikuwa nikijihisi ni mtu wa kutoa nasaha kwa wengine, sasa nimetambua kuwa mimi ndiye ninayehitaji kupewa nasaha. Kwa kweli muda wote huu nimekuwa na mtazamo usio sahihi kuhusiana na maisha. Baada ya kuwaza hayo na kuihukumu mwenyewe nafsi yake, Munkadir alimjongelea Imam Baqir na kumwomba radhi kwa maneno aliyomwambia. Kisha akaanza kuondoka taratibu na kuendelea na safari yake. Akiwa njiani yalikuwa yakimpitikia akilini mwake maneno ya Imam Muhammad Baqir (as) pale alipomwambia:" Endapo mauti yatanifika nikiwa nimo katika kufanya kazi, sina khofu kwa hilo, kwani nitakufa nikiwa nimo katika kumuwabudu Mwenyezi Mungu."

Mpenzi msomaji, kisa ulichokisikia kilitokea zaidi ya miaka elfu moja iliyopita. Lakini ajabu ni kuwa katika dunia yetu hii ya leo, kungali kuna akina Munkadir wengi, ambao kwa mtazamo wao, mswalihina ni yule akithirishaye kufanya ibada za kiroho tu na kupitisha muda mwingi katika ibada hizo bila kujishughulisha na kazi kwa ajili kutafuta riziki ya halali. Si ajabu kukuta watu wa aina hiyo wakiishi maisha ya ombaomba kwa sababu ya kukaa bila ya kufanya kazi kwa kisingizio cha kuipa mgongo dunia, na kujiweka mbali na tamaa ya kutafuta mali. Kama wewe mpenzi msikilizaji ni mmoja wa watu wa aina hiyo, natumai kisa hiki kitakuwa kimeuondoa akilini mwako mtazamo huo usio sahihi.

*******

Tafadhali msimulie na mwenzako.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …