Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 13 Septemba 2009 22:17

VISA VYA KUELIMISHA (4)

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

******

Hii ni sehemu nyingine ya Visa vya Kuelimisha. Lakini, kama nilivyotangulia kusema katika kisa kilichopita, si vile visa vya ngano za kubuni za alfu lela ulela, wala si vya Hadithi za kutunga, za Paukwa Pakawa au za matukio ya uvumi na tetesi ya sadiki ukipenda. Ni visa vya matukio ya kweli, yaliyotokea katika maisha ya viongozi halisi wa wanaadamu, yaani Manabii wa Mwenyezi Mungu. Visa ambavyo ni kigezo na ruwaza njema, kwa mimi na wewe, ya kuweza kubadilisha maisha yetu, na kutufanya tupate fanaka, na saada, ya leo hapa duniani, na kesho, huko akhera. Ni visa vya matukio yaliyojiri katika maisha ya waja wema wa Allah, ambao kwao wao, Quran, Suna za Bwana Mtume na mafundisho ya Maimamu, vilikuwa ni miongozo ya kufuata kivitendo, katika kila kipengele cha maisha yao, na si mambo ya kuishia kwenye uhodari wa kuyatamka kwa ghibu tu, na kuyasimulia kwa wengine. Ni matumaini yangu kwamba, si mimi na wewe tu mpenzi msikilizaji, bali hata wale wote tutakaowafikishia, ujumbe uliomo ndani ya visa hivi vya kuelimisha, watayachukua mafunzo yake, na kuyatoa katika sura ya nadharia, na kuyafanya kuwa ni somo la amali na vitendo, katika maisha yao ya kila siku.

*******

Kulikuwa tayari kumepambazuka; Siku nyingine mpya ilikuwa imeanza, na hali ya hewa angavu ilikuwa imetanda katika anga ya mji wa Madina. Kama ilivyokuwa ada na kawaida ya kila siku, mji huo ulianza kuchangamka na kushuhudia pirika pirika za nenda huko rudi kule, za misafara ya wafanyabiashara, waliokuwa wakijiandaa kwa safari ya kuelekea Misri, ili kwenda kuuza bidhaa zao huko. Kati ya watu waliokuwemo kwenye misafara hiyo alikuwepo Musadif, aliyekuwa mtumishi na mmoja wa wafuasi wa Imam Jaafar Sadiq (as), ambaye naye pamoja na wenzake alikuwa akikamilisha kufunga funga mizigo yake, tayari kwa safari. Ili kumsaidia Musadif aweze kujipatia chochote, na vile vile kuweza kuuzungusha mtaji uliokuwa umekaa tu kwa biashara itakayoweza kuuongezea pato, Imam Sadiq aliamua kumpa Musadif dinari elfu moja. Musadif alichukua pesa hizo na kwa amri ya Imam akazinunulia bidhaa ili kwenda kuziuza huko Misri na kupata faida maridhawa. Msafara ulianza safari ya kuelekea Misri. Lakini wakati unakaribia kufika huko, njiani ukakutana na msafara wa mfanyabiashara mmoja aliyekuwa akitokea huko Misri. Wafanyabiashara wa misafara miwili wakaanza kusalimiana, na kuulizana mambo yakoje kibiashara huko Misri. Katika mazungumzo hayo ikabainika kuwa, bidhaa alizonunua Musadif zina soko na bei nzuri huko Misri, kwa sababu zilikuwa adimu mno wakati huo. Musadif alikuwa hajijui hajitambui kwa furaha, kwa habari hiyo aliyoisikia. Msafara wa mfanyabiashara aliyetokea Misri aliwaeleza kina Musadif kuwa bidhaa hiyo ilikuwa ikihitajiwa sana na watu, kiasi kwamba walikuwa wako tayari kuinunua kwa bei yoyote ile watakayouziwa. Kwa kusikia habari hiyo, Musadif na wenzake katika msafara wake wakakubaliana kuwa wakailangue bidhaa hiyo na kwamba wasikubali kuuza kwa faida iliyo chini ya bei waliyonunulia. Yaani kama kila bidhaa moja waliinua kwa dinari kumi, basi wahakikishe kwamba wanaiuza kwa dinari zisizopungua ishirini. Misafara ya wafanyabiashara wa Madina iliwasili Misri, na naam iliyoyakuta huko ndiyo yale yale yaliyokuwa yamesimuliwa kabla. Naye Musadif na marafiki zake, wakaazimia kutekeleza yale yale waliyokubaliana kabla ya kuwasili hapo. Hivyo wakaficha bidhaa zao hizo na kuanza kuwalangua watu kwa kuwauzia kwa bei ya juu mno yaani mara mbili ya ile waliyonunulia. Hata jua lilipokuchwa jioni ya siku hiyo hiyo ya kwanza, Musadif na wenzake walikuwa tayari wameshauza bidhaa zao zote. Akiwa na furaha tele Musadif alianza kuhesabu pesa zake na naam kitita cha faida halisi aliyopata kilikuwa sawa na mtaji aliokuwa nao kabla.

Akiwa na faida ya dinari elfu moja, Musadif alirejea zake Madina, na moja kwa moja akafululiza hadi kwa Imam Jaafar Sadiq. Kufika huko alitoa vifuko viwili, kila kimoja kikiwa kimejaa kitita cha dinari elfu moja na kumkabidhi Imam. Imam Sadiq aliuliza:" Ni kitu gani hiki? Musadif alijibu:" Kimoja kati ya vifuko viwili hivi ni cha mtaji uliokuwa umenipa, na kingine ni cha faida niliyopata ambayo ni sawa na mtaji wa asili. Imam Sadiq alimwambia, "Faida hii uliyopata ni kubwa mno kulinganisha na mtaji uliokuwa umenunulia bidhaa na kwenda nazo Misri. Ilikuwaje hata ukaweza kupata faida kubwa kama hii? Hapo Musadif akaanza kusimulia kisa chooote cha safari yao na kusema: "bidhaa za biashara tulizokwenda nazo Misri, zilikuwa adimu huko, hivyo tukakubaliana kuwa tuuze bidhaa zetu kwa faida sawa na gharama ya mtaji tuliokuwa nao. Wakati Musadif anaendelea kusimulia habari zake, uso wa Imam Sadiq ulibadilika ghafla. Kwani kitendo cha Musadif na wenzake cha kutoridhika na kile kilichokuwa haki yao, na kuamua kufanya waliyoyafanya kwa sababu ya tamaa, kilimkasirisha Imam Baada ya Musadif kumaliza kutoa maelezo yake, Imam Sadiq alimaka": Subhanallah! Ndo mambo gani hayo mliyofanya? Nyinyi mumelishana yamini kwamba muwalangue Waislamu wenzenu waliokuwa wakihitajia bidhaa hiyo, ili tu muweze kujipatia faida nono? Mimi katu siwezi kuikubali biashara aya aina hiyo, wala faida kama hiyo. Maneno ya Imam Jaafar Sadiq yalimfanya Musadif ainamishe uso wake chini kwa aibu, na kumfanya ajute mno kwa mambo aliyotenda. Imam Sadiq alikichukua kimoja kati ya vile vifurushi viwili na kusema :" Huu ndiyo mtaji wangu. Ama kile kingine wala hakukigusa bali alisema kuwambia Musadif:" Mimi sina haja na faida hiyo". Baada ya kutamka hayo alimuelekea Musadif na kuanza kumpa nasaha za kumhamasisha afanye juhudi na bidii za kutafuta chumo la halali, jambo ambalo bila shaka lina ugumu na uzito wake maalum. Katika nasaha zake hizo Imam Sadiq (as) alimwambia Musadif: "Ewe Musadif elewa kuwa, kulenga upanga katika uwanja wa vita vya Jihadi ni rahisi zaidi kuliko kujipatia chumo la halali". Nasaha hizo za Imam zilibaki kuwa somo na funzo lisilosahaulika kwa Musadif, hadi mwisho wa uhai wake. Mpenzi msomaji, ikiwa wewe ni mfanyabiashara, uko katika kundi gani kati ya mawili haya! Lile linalofuata nasaha za Imam Sadiq za kuwa na insafu katika kutia faida juu ya bei ya bidhaa au la kina Musadif katika safarai yao ya Misri la kuamua kulangua bidhaa pale inapoadimika ? Tukumbuke mimi na wewe kuwa riziki ya halali hata ikiwa kidogo, ni bora na Mwenyezi Mungu huibariki, kuliko ile nyingi inayopatikana kwa njia ya haramu, ambayo mbali na adhabu ya akhera, Mwenyezi Mungu huiondolea baraka hata hapa duniani. Haya basi ndiyo niliyokuwa nimekuandalia kwa leo. Inshallah tutakuwa pamoja tena wiki ijayo na kisa kingine cha kuelimisha.

*******

Tafadhali msimulie na mwenzako

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …