Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 13 Septemba 2009 22:15

VISA VYA KUELIMISHA (3)

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

******

Hii ni sehemu nyingine ya Visa vya Kuelimisha. Lakini, kama nilivyotangulia kusema katika kisa kilichopita, si vile visa vya ngano za kubuni za alfu lela ulela, wala si vya Hadithi za kutunga, za Paukwa Pakawa au za matukio ya uvumi na tetesi ya sadiki ukipenda. Ni visa vya matukio ya kweli, yaliyotokea katika maisha ya viongozi halisi wa wanaadamu, yaani Manabii wa Mwenyezi Mungu. Visa ambavyo ni kigezo na ruwaza njema, kwa mimi na wewe, ya kuweza kubadilisha maisha yetu, na kutufanya tupate fanaka, na saada, ya leo hapa duniani, na kesho, huko akhera. Ni visa vya matukio yaliyojiri katika maisha ya waja wema wa Allah, ambao kwao wao, Quran, Suna za Bwana Mtume na mafundisho ya Maimamu, vilikuwa ni miongozo ya kufuata kivitendo, katika kila kipengele cha maisha yao, na si mambo ya kuishia kwenye uhodari wa kuyatamka kwa ghibu tu, na kuyasimulia kwa wengine. Ni matumaini yangu kwamba, si mimi na wewe tu mpenzi msikilizaji, bali hata wale wote tutakaowafikishia, ujumbe uliomo ndani ya visa hivi vya kuelimisha, watayachukua mafunzo yake, na kuyatoa katika sura ya nadharia, na kuyafanya kuwa ni somo la amali na vitendo, katika maisha yao ya kila siku.

*******

Zakariya alikuwa ni kijana wa kikristo aliyekuwa akiishi katika zama za Imam Jaafar Sadiq (AS), mmoja wa wajukuu wa nyumba tukufu ya Bwana Mtume Muhammad saw. Zakariya na familia yake walikuwa wakiishi katika mji wa Kufa ulioko katika Iraq ya leo. Kwa muda mrefu, Zakariya alikuwa akifatilia habari za yale yaliyokuwa yakijiri huko Madina, na hasa harakati za kielimu za Imam Sadiq. Wakati huo sauti ya wito wa haki ilikuwa ikinong'ona ndani ya moyo wa Zakariya na kumtaka afanye hima ya kutafuta uongofu; hatimaye baada ya kufanya utafiti na udadisi, kijana huyo wa Kikristo akaamua kusilimu. Kusilimu kwa Zakariya kulisadifiana na kuwadia kwa msimu wa Hija. Hivyo kijana huyo aliyedhihirikiwa na uongofu, akaamua kuitumia safari hiyo tukufu kwa ajili ya kwenda kumzuru pia Imam Jaafar Sadiq huko Madina. Haiba ya kimaanwi ya Imam iliuteka moyo wa Zakariya. Lakini kabla ya kuagana na Imam na kurejea zake Kufa, kijana huyo alisimulia habari za kusilimu kwake. Hapo Imam Sadiq alimuuliza:" Kitu gani kilikufanya ukavutiwa na Uislamu?". Zakariya alijibu, kwa kusema: "Ndani ya quran nilisoma aya ya 52 ya suratu shura, ambapo Mwenyezi Mungu anamhutubu Mtume wake kwa kumwambia: "Na namna hivi tumekufunulia Wahyi (ewe Mtume) kwa amri yetu. Ulikuwa hujui kitabu ni nini, wala imani; lakini tumefanya kitabu hiki (Quran) ni nuru, ambayo kwayo tunamwongoza tumtakaye katika waja wetu." Baada ya kuisoma aya hiyo Zakariya aliongezea kusema: "Nahisi kuwa ni nuru hii, ndiyo iliyoniongoza mimi". Imam Sadiq alimgeukia Zakariya na kumwambia:" Nasadikisha kuwa Mwenyezi Mungu amekuongoa. Sikiliza sasa ewe mwanangu; kama una suali lolote lile, niulize tu". Kijana yule alisema: "Wazazi wangu ni wakristo, ambapo mama yangu yeye ni kipofu pia. Nifanye nini? ". Imam Sadiq alimwambia:" Jitahidi sana kumtunza mama yako; ijapokuwa hafuati dini unayofuata wewe, ama muda wa kwamba yu hai, hakikisha unamtendea wema". Baada ya kupokea wasia huo wa Imam, Zakariya alifunga safari ya kurejea kwao Kufa. Hakika wasia huo aliopewa aliuzingatia sana, na akaazimia kwamba asipoteze fursa yoyote ile aipatayo, isipokuwa aitumie kwa ajili ya kumtendea wema mama yake. Alikuwa akimlisha chakula kwa mkono wake mwenyewe, akimfulia na kumpangia nguo zake, na hata kumchana nywele zake. Mabadiliko hayo ya tabia ya Zakariya kwa mama yake, yaliyoshuhudiwa zaidi hasa baada ya yeye kurejea kutoka Makka, yalimstaajabisha mno mama yake, kiasi kwamba alishindwa kuvumilia na hivyo akaamua kumuuliza: " Ewe mwanangu, imekuwaje siku hizi unanienzi na kunitunza, kuliko ulivyokuwa huko nyuma, pamoja na kwamba sasa umekuwa mfuasi wa dini nyingine?". Zakariya alimjibu mama yake kwa kumwambia: "Mpenzi mama, haya ninayokufanyia, yanatokana na wasia niliopewa na bwana mmoja katika kizazi cha Bwana Mtume. Kwani dini niliyoingia ya Uislamu ina mafundisho mazuri mno kuhusu kuwafanyia wema wazazi wawili. Bwana Mtume saw amesema, kuutizama mtu kwa mapenzi, uso wa baba au mama yake, ni ibada; na Mwenyezi Mungu ameusia ndani ya Quran tukufu juu ya kuwatendea wema wazazi wawili, mara baada ya kuamuru waja wake wasimwabudu yeyote ghairi ya yeye.". Kusikia maneno hayo, mama mtu alitamka kwa furaha" Maamrisho na mafundisho haya mwanangu, hayawezi kutoka kwa yeyote ghairi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu; kwa kweli dini yako ni dini nzuri mno, hebu nieleze zaidi kuhusu mafundisho yake." Zakariya alitumia fursa hiyo kumfikishia mama yake wito wa Uislamu wa La ilaha illa llah, Muhammadun rasulullah, na hatimaye mama huyo naye akaamua kusilimu. Hakika mama wa Zakariya alifurahi mno, kupata taufiki ya kuutambua uongofu na kuufuata.

********

Siku na masiku yakapita, mwishowe uzee na maradhi vikamzidi nguvu mama wa Zakariya akawa mgonjwa taabani. Hata hivyo katika lahadha za mwisho za uhai wake, hakuacha kumwomba tena mwanawe amfunze na kumuelimisha, juu ya misingi ya mafundisho matukufu ya Uislamu. Zakariya aliitumia tena fursa hiyo kumkumbusha tena mama yake juu ya misingi mikuu ya Uislamu, ambayo ni tauhidi ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu, kumwamni Mtume wake, vitabu vyake vya mbinguni na siku ya malipo. Muda si muda mama wa Zakariya alifumba jicho, na kuaga dunia.

Zakariya alipatwa na huzuni na majonzi makubwa kwa kuondokewa na mama yake. Machozi yalimbubujika njia mbili mbili, na moyo wake uliingiwa na simanzi kubwa mno. Hata hivyo kilichomliwaza na kumfariji kijana huyo, ni kule kuona kwamba alijitahidi kadiri ya uwezo wake kutekeleza mafundisho ya dini yake tukufu ya Kiislamu kuhusiana na kuwatendea wema wazazi wake wawili. Utekelezaji ambao moja ya malipo yake madogo kabisa ya kheri aliyopata hapa duniani, ilikuwa ni kupata mama yake pia taufiki ya kuufuata uongofu. Zakariya aliyakumbuka maneno mengine ya Imam Sadiq pale aliposema: "Kuwatendea wema wazazi, ni sababu ya kumfanya mtu amtambue Mwenyezi Mungu, kwani hakuna ibada inayomfurahisha Mwenyezi Mungu kama kuwaheshimu wazazi". Mpenzi Msikilizaji, baada ya kuyasikia haya yaliyojiri katika maisha ya Zakariya ni mahala pake kujiuliza mimi na wewe, je tunajitahidi kwa kiwango gani kuwatendea wema wazazi wetu.

*******

 

Tafadhali msimulie na mwenzako.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …