Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 13 Septemba 2009 22:14

VISA VYA KUELIMISHA (2)

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

******

Hii ni sehemu nyingine ya Visa vya Kuelimisha. Lakini, kama nilivyotangulia kusema katika kisa kilichopita, si vile visa vya ngano za kubuni za alfu lela ulela, wala si vya Hadithi za kutunga, za Paukwa Pakawa au za matukio ya uvumi na tetesi ya sadiki ukipenda. Ni visa vya matukio ya kweli, yaliyotokea katika maisha ya viongozi halisi wa wanaadamu, yaani Manabii wa Mwenyezi Mungu. Visa ambavyo ni kigezo na ruwaza njema, kwa mimi na wewe, ya kuweza kubadilisha maisha yetu, na kutufanya tupate fanaka, na saada, ya leo hapa duniani, na kesho, huko akhera. Ni visa vya matukio yaliyojiri katika maisha ya waja wema wa Allah, ambao kwao wao, Quran, Suna za Bwana Mtume na mafundisho ya Maimamu, vilikuwa ni miongozo ya kufuata kivitendo, katika kila kipengele cha maisha yao, na si mambo ya kuishia kwenye uhodari wa kuyatamka kwa ghibu tu, na kuyasimulia kwa wengine. Ni matumaini yangu kwamba, si mimi na wewe tu mpenzi msikilizaji, bali hata wale wote tutakaowafikishia, ujumbe uliomo ndani ya visa hivi vya kuelimisha, watayachukua mafunzo yake, na kuyatoa katika sura ya nadharia, na kuyafanya kuwa ni somo la amali na vitendo, katika maisha yao ya kila siku.

********

Bwana huyo alikuwa akipiga hatua taratibu; huku miguu ikimtetemeka, alielekea yalikokuwa makao ya utawala wa Hajjaj Ibni Yusuf. Ijapokuwa mtu huyo alikuwa amekamatwa pamoja na watu wengine kadhaa kwa tuhuma za kufanya uhalifu, lakini ukweli ni kwamba, hana kosa lolote alilokuwa amefanya. Hata hivyo hakujua, ni vipi angeweza kuthibitisha kwamba hakuwa na hatia. Walipofika mbele ya Hajjaj, mtawala huyo alianza kusikiliza kesi ya mtu mmoja mmoja na kuainisha ni adhabu gani apewe kila mtuhumiwa. Ama ilipofika zamu ya mtu huyo ghafla ukatokea udhuru na Hajjaj akalazimika kuondoka. Lakini kabla ya kuakhirisha kesi hadi siku ya pili yake, Hajjaj alimkabidhi mtuhumiwa huyo kwa mmoja wa watu wake, aliyekuwepo kwenye hadhara iliyokuwa ikisikiliza kesi hiyo, aliyekuwa akiitwa Anbasah. Wakati anamkabidhi mtuhumiwa huyo kwa Anbasah, Hajjaj alisema: "Baki naye kwa usiku wa leo; kisha kesho asubuhi uniletee". Anbasah aliitikia na kumchukua mtuhumiwa huyo kwa safari ya kuelekea nyumbani kwake. Wakati wakiwa njiani, mtuhumiwa alimgeukia Anbasah na kumuuliza:" Naweza kuwa na matumaini ya kupata kheri yoyote kutoka kwako? Anbasah akajibu:" Kama una kitu unataka kuniambia, niambie, labda nitaweza kupata taufiki ya kufanya jambo la kheri". Mtuhumiwa akasema:" Nakuapia Mungu, mimi sijafanya kosa lolote, lakini naamini kwamba Mwenyezi Mungu atanirehemu kwa rehma na fadhila zake. Ila ninachokuomba kwa ihsani yako, niruhusu usiku huu wa leo niende kwa mke wangu na watoto wangu, ili nikawaage, niwape wasia wangu, na kulipa haki za watu. Nakuahidi kuwa, kesho asubuhi mapema, nitakuwa nyumbani kwako." Anbasah hakujibu kitu, bali aliangua kicheko tu aliposikia ombi la mtu huyo. Hata hivyo mtu huyo alirudia tena na tena ombi lake hilo, na kumbembeleza Anbasah amkubalie. Hali hiyo iliuathiri moyo wa Anbasah, na hivyo akawa anajisemea mwenyewe:" Wacha nitawakal kwa Mwenyezi Mungu, nimkubalie ombi lake". Baada ya kujisemea hivyo alimgeukia mtu huyo na kumuuliza:" E bwana sawa umenieleza hayo, utatekeleza kweli hayo unayoniahidi? Yule Bwana akamjibu: "Bila shaka; na Mungu ndiye shahidi wangu; nakuahidi kuwa kesho kabla ya kupambazuka, nitakuwa nyumbani kwako." Kwa maelezo hayo Anbasah akakubali kumwachia huru mtuhumiwa huyo, lakini mara baada ya kupita muda si mrefu akaanza kujuta kwa uamuzi aliochukuwa. Khofu na wasiwasi vilitanda moyoni mwake, kiasi kwamba usiku ule hakuweza kupata hata lepe la usingizi. Alibaki akihesabu saa, dakika na sekunde, mpaka kulipopambazuka. Ghafla alisikia mlango wa nyumba yake ukigongwa. Alikurupuka hadi mlangoni na kufungua mlango. Hakuamini macho yake, alipomwona yule mtuhumiwa amesimama mbele yake. Anbasah aliuliza kwa mshangao:" Imekuwaje, mbona umerudi? Yule Bwana alimjibu:" Kila mwenye kuuelewa uwezo wa Mwenyezi Mungu na ukamilifu wake, basi pale anapotoa ahadi na akawa amemfanya yeye Mwenyezi Mungu kuwa shahidi wake, lazima atimize ahadi yake. Ahadi tuliyowekeana mimi na wewe pamoja na kwamba haikuwa rasmi, na wala haina nguvu ya kisheria, lakini kimaadili na kiakhlaqi ni yenye thamani na inastahiki kuheshimiwa. Ewe Anbasah! Tambua kuwa katika Uislamu kutimiza ahadi ni miongoni mwa wajibu wa kila muislamu; na quran tukufu imelitaja suala hilo kuwa ni moja ya masharti ya imani na sifa za waumini wa kweli. Baada ya kutamka hayo, yule Bwana akaanza kuisoma Sura ya 23 ya al Muuminun kuanzia aya yake ya kwanza hadi ya tisa ambazo zinazungumzia sifa za waumini wa kweli, na kuitaja sifa iliyozungumziwa katika aya ya 8 ya sura hiyo ambayo inasema: Na wale ambao wanachunga amana, na kutekeleza ahadi (zao wanazotoa).

*******

Anbasah alimchukua mtuhumiwa huyo na kumfikisha kwa Hajjaj saa ile ile aliyotakiwa kufanya hivyo. Alipofika huko alisimulia kuanzia mwanzo hadi mwisho yale yooote yaliyojiri jana yake, kati yake na mtuhumiwa huyo. Hajjaj alistaajabishwa mno na sifa ya bwana huyo ya kutimiza ahadi aliyotoa, kiasi kwamba kitendo chake hicho kikawa ni ithbati na ushahidi tosha kuwa hakuwa na hatia yoyote. Hivyo kwa upande wake, Hajjaj akaamua kumkabidhi mtu huyo kwa Anbasah ambaye naye aliamua kumwachia huru aende zake. Lakini kabla ya kuagana na Anbasah, bwana yule alimgeukia mfadhili wake aliyemtendea wema akamwambia: "Awali kabla ya yote namhimidi na kumshukuru Mwenyezi Mungu, kisha natoa shukrani zangu kwako". Baada ya hapo akaanza kujikongoja taratibu akielekea nyumbani kwake, huku machozi yakimlengalenga wakati alipoyakumbuka maneno ya Bwana Mtume aliposema: "Watu watakaokuwa karibu nami siku ya Kiyama, ni wale waliokuwa wakweli katika wasemayo, waaminifu katika amana, na watimizaji wa ahadi.

********

Tafadhali msimulie na mwenzako.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …