Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 13 Septemba 2009 22:11

VISA VYA KUELIMISHA (1)

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

******

Huu ni mfululizo wa Visa vya Kuelimisha. Lakini, si vile visa vya ngano za kubuni za alfu lela ulela, wala si vya Hadithi za kutunga, za Paukwa Pakawa au za matukio ya uvumi na tetesi ya sadiki ukipenda. Ni visa vya matukio ya kweli, yaliyotokea katika maisha ya viongozi halisi wa wanaadamu, yaani Manabii wa Mwenyezi Mungu. Visa ambavyo ni kigezo na ruwaza njema, kwa mimi na wewe, ya kuweza kubadilisha maisha yetu, na kutufanya tupate fanaka, na saada, ya leo hapa duniani, na kesho, huko akhera. Ni visa vya matukio yaliyojiri katika maisha ya waja wema wa Allah, ambao kwao wao, Quran, Suna za Bwana Mtume na mafundisho ya Maimamu, vilikuwa ni miongozo ya kufuata kivitendo, katika kila kipengele cha maisha yao, na si mambo ya kuishia kwenye uhodari wa kuyatamka kwa ghibu tu, na kuyasimulia kwa wengine. Ni matumaini yangu kwamba, si mimi na wewe tu mpenzi msikilizaji, bali hata wale wote tutakaowafikishia, ujumbe uliomo ndani ya visa hivi vya kuelimisha, watayachukua mafunzo yake, na kuyatoa katika sura ya nadharia, na kuyafanya kuwa ni somo la amali na vitendo, katika maisha yao ya kila siku.

*******

Siku nyingi zilikuwa zimepita, wakati sahaba huyo alipokaa kitako peke yake akaanza kukumbuka kipindi cha hali ngumu mno ya maisha aliyokabiliana nayo huko nyuma. Maruweruwe ya machungu ya makali ya maisha yaliyomkabili katika kipindi hicho yalikuwa bado yakimpitikia akilini mwake. Hali yake ilikuwa mbaya na ya kusikitisha mno kiasi kwamba alikuwa akishindwa hata kumudu mlo wa siku moja kwa ajili ya mkewe na watoto wake. Ilipofikia hadi ya kushindwa kuvumilia hali hiyo ndipo alipoamua kutoka mguu mosi mguu pili hadi kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu ili kuomba msaada na ushauri wa nini la kufanya. Alifika kwa Mtume; lakini kabla ya kufungua kinywa na kutaaradhia shida yake alimsikia Bwana Mtume akisema: "Yeyote atakayetuomba msaada tutamsaidia, lakini iwapo mtu atajizuilia kunyoosha mkono wake kwa watu kuomba msaada, Mwenyezi Mungu atamfanya mkwasi". Baada ya kusikia maneno hayo, bwana huyo aliamua kutosema chochote mbele ya Bwana Mtume; badala yake akashika njia na kurejea nyumbani kwake. Lakini ndani mulikuwa hamukaliki. Kwani jinamizi la ufukara lilikuwa limeigubika nyumba ya sahaba huyo kiasi kwamba hakuwa na hili wala lile isipokuwa kurudi tena kwa Bwana Mtume kwa nia ile ile ya kushtakia hali yake na kuomba ushauri na msaada. Ama mara hii pia alisikia maneno yale yale ya mara ya kwanza yaliyotoka kinywani mwa Nabii huyo wa rehma. Kinyume na mara ya kwanza, mara hii maneno hayo yalimtia nguvu sahaba huyo na kutoa mtikiso maalumu ndani ya moyo wake kiasi kwamba alipoamua kwa mara ya tatu kurudi tena kwa Bwana Mtume ili kushtakia hali yake alishangaa kusikia tena maneno yale yale kwa sauti yenye kutoa msisimko maalumu kutoka kinywani mwa Mtume wa Allah, akisema:" Ikiwa mtu hatanyoosha mkono wake kuwaomba watu, Mwenyezi Mungu atamfanya mkwasi". Maneno hayo yalipenya kama mshale ndani ya moyo wake na ubongo wake. Alimaizi kuwa utatuzi wa shida yake ya maisha ulikuwa umejificha kwenye maneno yale mazito ya Bwana Mtume. Hapo ndipo alipoamua kuondoka kwa imani thabiti huku akijisemea moyoni: "kuanzia sasa nitatawakal kwa Mwenyezi Mungu tu, nitaomba msaada kwake yeye tu, nitatumia nguvu na uwezo alionijaalia na kumwomba aniwafikishe". Baada ya kutamka hayo, sahaba huyo alikwenda zake nyumbani akachukua tezo yake na kuelekea jangwani ambako alianza kazi ya kukata na kukusanya kuni na kwenda kuziuza ili kupata riziki ya kuendeshea maisha yake, mkewe na watoto wake. Huo ulikuwa mwanzo wa kuonja ladha ya pato lililotokana na jasho lake mwenyewe. Sahaba huyo aliendelea na kazi yake hiyo siku ya pili, ya tatu yake na ya nne, na hivyo taratibu akaanza kupata mtaji uliomwezesha kutatua shida zake za maisha. Mabadiliko hayo yaliyofungua ukurasa mpya katika maisha yake, mkewe na watoto wake yalimpa funzo la kivitendo sahaba huyo kuwa kutawakal kivitendo kwa Mola, ambaye ndiye mtoaji wa riziki kwa viumbe wake wote ndiko kulikoweza kubadilisha hali yake ya maisha; na kwamba kuiendea sababu ya kupatia riziki ya halali, ndio ufunguo wa kushukiwa na baraka za mbinguni za Mola Karima ambaye bila ya rehma zake yeye haingewezekana kwa yeye kuishinda misukosuko na makali ya maisha yaliyokuwa yamemkabili.

Siku na masiku yalipita; mpaka ikasadifu siku moja sahaba huyo mtema kuni akakutana na Bwana Mtume saw. Nabii huyo wa rehma alimtazama bwana huyo huku akitabasamu na kumwambia:"Unakumbuka nilikueleza, yeyote atakayetaka msaada kutoka kwetu tutamsaidia, lakini kama mtu hatoonyoosha mkono wake kwa watu, Mwenyezi Mungu atamfanya mkwasi".

Lakini Bwana Mtume ametupa funzo jingine la matunda ya kutawakal kwa Mwenyezi Mungu na kumtegemea yeye Mola. Nabii huyo wa rehma anasema:"Anayetaka kuwa mtu mwenye nguvu zaidi kuliko yeyote basi na atawakal kwa Mwenyezi Mungu".

***

Tafadhali msimulie na mwenzako

 

Zaidi katika kategoria hii: « VISA VYA KUELIMISHA (2)

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …