Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 19 Februari 2013 16:17

Historia ya Wazartoshti

Historia ya Wazartoshti

Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kusikiliza kipindi kingine cha Uliza Ujibiwe. Kipindi hiki kitajibu swali la msikilizaji wetu Bwana Onoleka Andre wa Entebbe nchini Uganda ambaye anaomba kufahamishwa Wazartoshti ni nani.

Tunamshukuru Bwana Andre kwa swali hili ambalo tunalijibu kwa kusema kwamba, kama mnavyojua, Mwenyezi Mungu aliwatuma manabii na mitume wengi kwa jamii ya wanadamu ili wapate kuwaongoza kweye njia nyoofu, ya saada na ukamilifu. Wairani pia ni miongoni mwa mataifa yaliyotumiwa mitume ili wapate kuwaongoza kwenye njia ya wongofu. Miongoni mwa manabii hao ni nabii ajulikanaye kwa jina la Zartosht. Kama inavyodhihiri katika vitabu vya historia ni kwamba, mtume huyo alidhihiri katika moja ya maeneo yanayopakana na Ziwa Urumiyeh lililoko kaskazini magharibi mwa Iran. Wataalamu wa mambo wanasema kwamba kabla ya kuingia Uislamu nchini Iran, wengi wa watu wa nchi hii walikuwa wafuasi wa dini ya Kizartoshti. Katika utamaduni wa Qur'ani, wafuasi wa dini hii wametajwa kuwa majusi. Kuna tofauti za mitazamo kuhusiana na sehemu alikozaliwa au kuishi mtume huyo wa Mwenyezi Mungu. Inasemekana kuwa mtume huyo alifahamika sana kutokana na ujuzi wake mkubwa katika masuala ya hekima na alipofikia umri wa miaka 15  akadhihiri kuwa na kipawa kikubwa katika masuala ya maarifa, ibada, maadili na takwa.

Alipotimu umri wa miaka 20 alijitenga na watu kwa lengo la kujishughulisha na masuala ya zuhdi na uchaji Mungu hadi alipohitimu miaka 30 ambapo aliteuliwa na Mwenyezi Mungu kwa lengo la kuwaongoza watu kwenye masuala ya kidini. Mtume Zartosht alidhihiri katika zama ambazo watu wa Iran walikuwa wamezama katika imani ya uchawi na ibada ya masanamu na wala hawakuwa tayari kukubali wito wowote wa wongofu ulio mbali na ibada hiyo. Katika kipindi hicho ambacho huenda kilikuwa kati ya karne ya 6 na 7 kabla ya kuzaliwa Nbaii Isah Masih (as) Zartosht alidhihiri na kuanza kuwahubiria watu neno la Mungu ambapo aliwataka waachane na ibada ya masanamu na kumuabudu Mwenyezi Mungu mmoja. Baadhi ya watafitii wa historia wanasema kwamba harakati za ulinganiaji za Zartosht zilianza mwaka 660 kabla ya kuzaliwa Nabii Isah (as). Licha ya kuwa Zartosht aliuawa baadaye na wapinzani wake lakini dini na ujumbe wake uliendelea kuenea hadi wengi wa watu walioishi chini ya ufalme wa Makhamanesh walipofuata dini hii. Kitabu cha Wazartoshti kinaitwa Avista na kimeandikwa kwa lugha ya kaumu ya Wamad. Wairani walipoteza kitabu kitakatifu cha Avista katika zama za utawala na udhibiti wa Alexander nchini Iran lakini baadaye wakakichapisha tena katika kipindi cha wafalme wa Wasasani. Licha ya kutoweka sehemu kubwa ya kitabu hicho lakini bado kuna sehemu muhimu ya kitabu hicho ambayo ipo mikononi mwa Wairani nayo kimingi inahusiana na nyimbo za Zartosht. Nyimbo hizo zinahusiana na shakhsia ya Zartosht, waungaji mkono, wafuasia na maadui zake. Moja ya matamshi ya Zartoshi ni haya yafuatayo: "Maisha hayaishii kwenye mauti bali mauti ni wito wa uamuzi utakaofanyika siku ya Kiama. Wale waliofanya matendo mema humu duniani watakaribishwa kwenye enzi ya Mungu na waliotenda maovu watatupwa kwenye hofu na adhabu..."

Dini ya Zartoshti kama zilivyo dini nyingine za mbinguni ilisimama kwenye msingi wa tauhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu. Katika dini hii Ahura Mazda ni Mungu mwenye uwezo, busara na aliye na sifa za ukamilifu. Ahriman ni dhihirisho la kiza nao malaika ni dhihirisho la nuru na mwangaza. Nara na nasaha muhimu katika dini ya Kizartoshti ni "Fikra safi, matamshi safi na matendo safi." Msingi muhimu katika dini hii ni imani kuhusiana na kuwepo dunia nyingine isiyokuwa hii, Siraat na Mizani, Hukumu ya Mwenyezi Mungu kuhusiana na matendo ya wanadamu, Pepo na Jahannam. Katika dini ya Zartoshti ushindi wa mwisho ni wa mwangaza na ukweli na kwa msingi huo mwanadamu anapasa kufanya kila awezalo kufuata njia hiyo.

Ni wazi kwamba baada ya kuaga dunia Zartosht dini yake taratibu ilipotoshwa na wafuasi wake ambao waliingiza humo imani na itikadi mpya potofu. Kwa mfano wafuasi hao walianza kusifu na kumnasibisha Zartosht na mambo yasiyomuhusu kabisa. Miongoni mwa mambo na imani hizo ni kuwa walianza kumpa sifa za kiungu au kunasibisha kwake miujiza isiyo ya kawaida na hivyo kuifanya dini yake kuonekana kuwa dini ya miungu wawili.

Baada ya kudhihiri dini ya Kiislamu nchini Iran, Wairani waliacha dini hiyo iliyopotoshwa ya Kizartoshti na kuingia kwa umati katika dini hii tukufu. Uzartoshi ambao mwanzoni ulikuwa na malengo pamoja na ujumbe mzuri wa mbinguni ulipotoshwa na kuanza kutumiwa vibaya na wafalme na watu wenye ushawishi na madaraka nchini Iran. Mbali na upotovu ulioonekana wazi katika dini hiyo, ufisadi na dhulma ilienea kwa kasi na kwa kiwangio cha juu katika utawala wa wafalme wa Wasasani. Dhulma na uonevu ulioenezwa na wafalme hao ulifanya maisha ya wananchi wa kawaida kuwa magumu sana. Katika kitabu chake cha historia kuhusiana na Wairani, Edward Brawn anasema kuwa Wairani waliuchukulia Uislamu ulioingia nchini kuwa mwokozi wao kutokana na dhulma na uonevu waliokuwa wakifanyiwa na wafalme wao. Si tu kwamba Wairani hawakukabiliana na Uislamu ulioingia nchini bali walifanya juhudi kubwa za kuueneza na kuhakikisha kuwa unafika katika kila pembe ya nchi.

Kwa mujibu wa riwaya za Kiislamu wafuasi wa dini za mbinguni kama vile Ukristo, Uyahudi na Uzartoshti ni Ahlu Kitabu. Msingi muhimu uliofuatiliwa na manabii wote katika mafundisho yao ni upwekeshaji na ibada ya Mwenyezi Mungu mmoja. Kwa maelezo hayo wapenzi wasikilizaji, 'utatu' unaohubiriwa katika dini iliyopotoshwa ya Ukristo na 'uwili' katika dini ya Uzartoshti ni jambo linalopingana moja kwa moja na msingi wa tauhidi na upwekeshaji wa Mwenyezi Mungu, ambao ulihubiriwa na mitume wote wa Mwenyezi Mungu. Hii ni kwa sababu mitume hao wote waliwataka wanadamu kuachana na fikra pamoja na ibada potofu ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kuafuata dini sahihi ya kumuabudu Mwenyezi Mungu mmoja tu. Kwa maelezo hayo dini yoyote inayofundisha wafuasi wake imani potofu ya kuabudu miungu na masanabu na kutozingatia tauhidi katika ibada ni dini potofu na isiyopasa kufuatwa na mja yeyote aliye ni fikra sahihi. Shirki inahesabiwa kuwa dhambi kubwa isiyosamehewa na Mwenyezi Mungu katika mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu na kwa hivyo mwanadamu anapasa kufanya juhudi kubwa za kujiweka mbali na dhambi hiyo.

Wapenzi wasikilizaji muda hauturuhusu kuendelea kujibu maswali ya wasikilizaji wetu wengine. Ni matumaini yetu kwamba sote tumenufaika na jibu la swali hili lililoulizwa na msikilizaji wetu Bwana Oneleka Andre wa mjini Entebbe Uganda. Basi hadi tutakapokutana tena katika kipindi kingine panapo majaaliwa yake Mola, tunakuageni nyote tukikutakieni wakati mwema mnapoendelea kutegea sikio vipindi vilivyosalia vya Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kwaherini

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)