Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 30 Januari 2013 20:57

Sababu za Imam Khomeini (MA) kuelekea Ufaransa

Sababu za Imam Khomeini (MA) kuelekea Ufaransa

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kusikiliza kipindi cha juma hili cha Uliza Ujibiwe. Kipindi hiki kitajibu swali la msikilizaji wetu Bwana Bakari Hamisi Dagama wa Songea Tanzania ambaye anaomba kujua iwapo Imam Khomeini (MA) alizaliwa nchini Iran au kwingineko na pia shue alizosomea masomo ya kidini na kiakademia. Bwana Dagama pia anataka kufahamishwa lengo la safari ya Imam Khomeini nchini Ufaransa na kama alielekea huko kwa ajili ya kuhubiri dini au kufanya biashara.

Tunalijibu swali la msikilizaji huyu mpendwa kwa kusema kwamba Imam Khomeini ni miongoni mwa watu mashuhuri katika historia ya mwanadamu wa leo, ambaye amefanya juhudi kubwa kwa ajili ya kuhuisha mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu. Imam Khomeini (MA) huku akifuata mafundisho ya Mtume Muhammad (saw) na Maimamu waliokuja baada yake, alianzisha harakati kubwa ya kupigania haki na kupambana na dhulma iliyokuwa imeenezwa nchini Iran na wafalme wa wakati huo. Kufuatia harakati hiyo wananchi wa Iran walianza kushuhudia mwanga mpya wa matumaini na kunufaika na matunda ya Mapinduzi ya Kiislamu kutokana na uongozi wake wa busara. Ayatullahil Udhma Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu anasema hivi kuhusiana na shakhisa huyo: "Ama kwa kweli hakuna shakhsia mwingine yeyote anayeweza kulinganishwa na shakhsia adhimu, kiongozi mkubwa na Imam wetu mpendwa baada ya mitume wa Mwenyezi Mungu na mawalii wake watakasifu."

Imam Sayyid Ruhullah Musawi Khomeini alizaliwa tarehe 21 Septemba 1902 katika familia moja ya kielimu na kidini huko katika mji wa Khomein katika Mkoa wa Kati wa Iran. Baba yake alikuwa mwanazuoni mashuhuri, mwaminifu, shujaa na aliyependwa sana na watu wa mji huo. Alifahamika kwa kupambana na magenge ya wezi na majangili waliokuwa wakipora mali, kuua na kuwatatiza wakazi wa mji huo. Aliuawa na magenge hayohayo Imam alipokuwa na umri wa miezi mitano tu. Baada ya kuachwa bila baba mzazi Imam Khomeini alilelewa katika kipindi cha utotoni na mama yake. Kipindi hicho kiliandamana na kipindi cha kuongezeka harakati za mabadiliko ya kisiasa na kijamii nchini ambayo yalilenga kubana madaraka ya ufalme mutlaki nchini. Baadhi ya mutukio hayo yaliathiri moja kwa moja maisha ya Imam Khomeini. Kwa bahati mbaya, msiba mwingine mkubwa ulimfika Imam akiwa na umri wa miaka 15 ambapo alimpoteza mama yake mpendwa. Hata hivyo Imam Khomeini alionyesha subira kubwa mbele ya msiba na machungu ya kuwapoteza wazazi wake angali mdogo na kuamua kufuatilia kwa bidii masomo yake ya msingi. Akiwa na umri huo mdogo alijifunza masomo ya msingi ya zama hizo yakiwemo ya lugha ya Kiarabu, mantiki, fikhi na usuul. Aliamua kwenda kusoma masomo ya juu katika chuo cha kidini cha Arak mnamo mwaka 1918. Baada ya hapo Imam alielekea katika mji mtakatifu wa Qum kwa lengo la kunufaika zaidi na masomo ya kidini kutoka kwa wanazuoni wakubwa na mashuhuri wa wakati huo kama vile Ayatullahil Udhma Hairi. Imam alipiga hatua kubwa ya masomo kwa haraka kutokana na kipawa pamoja na ufahamu wake mkubwa wa masomo. Mbali na masomo ya fakhi, usuul na falsafa Imam Khomeini pia alisomo na kufikia kiwango cha juu cha somo la irfani kutoka kwa mwanazuoni mashuhuri zaidi wa zama hizo yaani Ayatullah Agha Mirza Muhammad Ali Shah Abadi. Imam alijaaliwa kumuoa Bibi Khadija Thaqafi mnamo mwaka 1929 akiwa na umri wa miaka 27.

Mwaka 1937 akiwa na umri wa miaka 35 tu alidhihiri kuwa mmoja wa wahadhiri na walimu mashuhuri wa kidini katika taasisi ya kidini ya Qum. Katika kipindi hicho wanafunzi vijana wa mji huo mtakatifu walikuwa na hamu kubwa ya kuhudhuria masomo yake. Hadi kufikia mwaka 1941 mbali na kujishughulisha na masuala ya kielimu, kuandika vitabu na kufundisha katika chuo hicho cha kidini, Imam Ruhullah Khomeini alikuwa akishughulishwa sana na masuala ya kupambana na dhulma na udikteta uliokuwa ukifanywa na watawala wa nchi. Dukuduku lake kuu lilikuwa ni kuona kwamba kituo cha kidini cha Qum kinaendeshwa kwa njia inayofaa na bila ya uingiliaji wa watawala wa zama hizo. Alipigana na kufanya juhudi kubwa za kuinua kiwango cha umaanawi katika taasisi hiyo ya kidini kwa lengo la kukabiliana na dhulma ya ndani na uingiliaji wa kigeni. Licha ya kushughulikia masuala ya ndani Imam Khomeini pia alifuatilia kwa karibu masuala ya kisiasa na kijamii yaliyokuwa yakiendelea katika mataifa mengine ya dunia.

Mwaka 1961 Ayatullahil Udma Burujerdi, marja na mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu aliaga dunia na watu wengi wakiwemo wanafunzi na wataalamu wa masuala ya kidini kumtaka Imam awe marja wao kwa kuzingatia kiwango chake cha juu cha masomo, akhlaki na uelewa wake mkubwa wa masuala ya kisiasa na kijamii. Hicho kilikuwa kipindi ambapo ushawishi na uingiliaji wa Marekani nchini ulikuwa umefikia kilele. Serikali ya Washington ilimshinikiza kibarake wake Shah Pahlavi atekeleze baadhi ya mambo yaliyokwenda kinyume kabisa na mafundisho ya dini ya Kiislamu. Baada ya kuona hatari ya njama hizo za Wamarekani dhidi ya Uislamu Imam aliamua kusimama imara dhidi ya njama hizo mwaka 1962 ambapo aliandaa maandamano makubwa ya kulalamikia jambo hilo kwa ushirikiano wa baadhi ya wanazuoni wa mjini Qum na Tehran.

Shah alikuwa na lengo la kufanya marekebisho ya sheria zilizokuwa zikitawala nchini kwa kuitisha kura ya maoni ya kidhahiri ali kuwaridhisha mabwana zake wa Marekani, jambo ambalo lilikabiliwa na upinzani mkubwa wa wanazuoni waliokuwa wakiongozwa na Imam Khomeini (MA), ambapo waliharamisha kura hiyo ya maoni. Ili kukandamiza upinzani wa wanazuoni hao waliokuwa wakiungwa mkono na wananchi, Shah aliamuru askari wawafyatulie risasi wananchi waliokuwa wamekusanyika kulalamikia jambo hilo ambapo idadi kubwa kati yao waliuawa na kujeruhiwa. Mwaka 1963 askari wa Shah walivamia chuo cha kidini cha Feidhiyya mjini Qum na kuwaua kinyama wanafunzi waliokuwa humo. Hujuma kama hiyo ilifanywa pia katika shule za kidini katika mji wa Tabriz. Kinyume na alivyotarajia Shah, maandamano na upinzani wa wanazuoni ulizidi kuongezeka nchini dhidi ya utawala wake licha ya kuzidisha hatua za usalama na ukandamizaji dhidi ya wapinzani. Wanazuoni na watu wa matabaka mbalimbali walikuwa wakikusanyika kila siku mbele ya nyumba ya Imam Khomeini mjini Qum ili kutangaza uungaji mkono wao kwa harakati za wanazuoni dhidi ya utawala wa Shah. Bila ya kusita wala woga wowote Imam Khomeini (MA) alikuwa akiuhutubia umati mkubwa uliokuwa ukikusanyika nymbani kwake kila suku na kumshambulia kwa maneno makali Shah pamoja na kumtaja kuwa chanzo halisi cha mauaji ya kinyama dhidi ya wananchi, mauji ambayo yalikuwa yakitekelezwa kwa ushirikiano wa moja kwa moja wa Marekani na utawala haramu wa Israel. Aliwataka wananchi kusimama dhidi ya njama hizo za wageni na kuwashajiisha waendeleze mapambano yao dhidi ya utawala wa kibaraka wa Shah. Baada ya kuhisi hatari utawala wa Shah uliamua kumtia nguvuni Imam mnamo tarehe 5 Juni 1963, jambo lililowasha moto wa maandamano na migomo katika miji mingi ya Iran.

Utawala wa Shah ambao haukutaka kuonekana na mabwana wake wa Magharibi kuwa dhaifu mbele ya waandamanaji, uliamuru waandamanaji waliokuwa wakiandamana katika miji tofauti ya Iran wauawe bila huruma. Hata hivyo miezi kadhaa baadaye Shah alilazimika kumuachilia huru Imam. Hata baada ya kuachiliwa huru, Imam hakuogopa vitisho vya Shah bali kwa kuzingatia uungaji mkono mkubwa aliokuwa nao kutoka kwa wananachi aliendelea kukosoa siasa zake mbovu na kuwasihi watu waendelee kusimama dhidi ya siasa hizo. Shah ambaye wakati huo alikuwa ameingiwa na wasiwasi mkubwa kutokana na uwezekano wa kuanguka utawala wake, alifanya njama ya kumbaidisha Imam nje ya nchi. Mwaka 1965 alimbaidishia Uturuki na mwaka mmoja baadaye katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq ambapo kipindi rasmi cha miaka 14 ya kubaidishwa Imam nje ya nchi kilianza.

Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji hatuna budi kusimamia hapa kwa leo kutokana na kumalizika muda uliotengewa kipindi hiki. Tutaendelea kuzungumzia maisha ya Imam Khomeini (MA) katika kipindi kijacho panapo majaaliwa. Kwaherini.

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)