Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 23 Januari 2013 15:06

Salman al Farsi + Sauti

Msikiti maarufu wa Salman al Farsi katika mji wa Madain nchini Iraq. Msikiti maarufu wa Salman al Farsi katika mji wa Madain nchini Iraq.

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kusikiliza kipindi kingine cha Uliza Ujibiwe ambacho kwa leo kitajibu swali la msikilizaji wetu Bwana Onoleka Andre wa Entebbe nchini Uganda. Msikilizaji wetu huyu anaomba kujulishwa kwa ufupi maisha ya swahaba mashuhuri wa Bwana Mtume (SAW) aliyejulikana kwa jina la Salman Farsi.

Huku tukimshukuru Bwana Andre kwa swali lake hili, tunalijibu kwa kusema kwamba Muhyi Deen Arabi mmoja wa Maarif na wanazuoni mashuhuri wa Ahli Sunna anasema hivi kuhusiana na swahaba huyo mtukufu: "Kufungamana kwa Salman Farsi na Ahlu Beit wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) ni uthibitisho wa wazi kutoka kwa Mtume kwamba swahaba huyo alifikia kiwango cha juu cha usafi na usalama wa roho. Hii ni kwa sababu maneno ya Mtume kwamba Salman ni miongoni mwa Ahlu Beit wake hayakuwa na maana ya kubainisha mfungamano wa damu bali yalibainisha sifa zake za hali ya juu za kibinadamu."

Baada ya kudhihiri Uislamu Wairani au kwa ibara nyingine Waajemi waliikumbatia dini hii tukufu kwa moyo mkunjufu na kuihudumia kwa nguvu zao zote. Miongoni mwa watu waliotoa mchango mkubwa kwa madhumuni ya kuihudumia dini hii ni Salman Farsi. Swahaba huyo ni miongoni mwa watu mashuhuri katika historia ya Iran na Uislamu kwa ujumla. Swahaba huyo kabla ya kusilimu alijulikana kwa majina ya Borzuyeh au Ruzbeh Parsi. Alizaliwa katika eneo la Jei mkoani Isfahan nchini Iran na kulelewa katika duru za kielimu na kiutamaduni. Alianza kutafiti na kufuatilia kwa karibu masuala yaliyohusiana na dini tofauti akiwa angali kijana mdogo. Mwanzoni alifuata dini ya Kizartoshti lakini akaachana nayo na kufuata Ukristo baada ya kuona kwamba maswali yake mengi kuhusiana na Mwenyezi Mungu na uumbaji wa ulimwengu na mwandamu hayakujibiwa na dini hiyo. Dini ya Ukristo pia haikuweza kumkinaisha kuhusiana na maswali hayo na kwa hivyo akaamua kuelekea Sham ili kuyatafutia majibu mswali hayo yaliyokuwa yakimsumbua. Aliamua kuelekea Hijaz kwa sababu alisikia kutoka kwa makasisi wa kanisa kwamba wakati ulikuwa umewadia wa kudhihiri mtume mpya. Alifanya safari hiyo akiwa na umri wa miaka 50 na katika mwaka wa kwanza wa hijra ya Mtume kwenda Madina yaani mwaka 622 Miladia. Lakini alipokuwa njiani alitekwa nyara na kabila la Bani Kalb. Hatimaye alinunuliwa na Yahudi mmoja kutoka kabila la Bani Qureidha ambaye alimpeleka Yathrib yaani Madina ya leo. Alipokuwa mjini humo alipata kufahamu kwamba Mtume Mtukufu (SAW) alikuwa amedhihiri na kuamua kuikumbatia kwa mikono miwili dini ya Kiislamu. Alichukua hatua hiyo bila kupoteza wakati kutokana na kuwa sifa zote ambazo makasisi walikuwa wamezitaja kuhusiana na mtume huyo mpya zilionekana wazi kwa Mtume Muhammad (SAW). Kwa msingi huo Salman Farsi alikuwa amepata kitu alichokuwa akikitafuta kwa miaka mingi na hivyo kumfanya asilimu mikononi mwa Mtume Mtukufu (SAW). Mtume alimununua Salman kutoka kwa mmiliki wake huyo wa Kiyahudi na kumuachilia huru. Tokea hapo alikuwa swahaba wa karibu wa Mtume na kupata nafasi ya juu pembeni yake. Baada ya kusilimu Mtume alimpa Ruzbeh Parsi jina la Salman kwa maana ya salama na kusalimu amri. kuchaguliwa kwa jina hilo na Mtume ni ishara ya wazi juu ya usafi na usalama wa roho ya Salman Farsi.

Salman Farsi daima alikuwa akipigana vita pembeni ya Mtume Mtukufu (SAW). Alitoa mchango mkubwa wa ushindi kwa Waislamu katika vita vya Ahzab au kwa jina jingine Khandaq ambavyo vilipiganwa katika mwaka wa Tano Hijiria. Uzoefu na ujuzi wake ulitoa mchango mkubwa kwa manufaa ya Waislamu katika vita hivyo. Alitoa pendekezo la kuchimbwa handaki pambizoni mwa mji wa Madina ili kuzuia hujuma ya jeshi kubwa la maadui dhidi ya mji huo wa Waislamu, pendekezo ambalo lilikubaliwa na Mtume. Siku hiyo Maansar walikuwa wakisema Salman ni miongoni mwao nao Muhajirina wakisema hivyo hivyo. Baada ya kusikia hayo Mtume aliwaita wote na kuwaambia, "Salman Minna Ahlul Bet," kwa maana kwamba Salman alikuwa mmoja wa Ahlu Beit wa Mtume. Mtume aliyasema hayo kutokana na nafasi pamoja na ukuruba mkubwa aliokuwa nao Salman kwa Mtume. Salman pia alikuwa na nafasi muhimu katika ushindi wa Waislamu dhidi ya adui katika vita vya Taif kwa kutengeneza zana ya kurushia mizinga kwa jina la minjaniq.

Kama tulivyosema mwanzoni wapenzi wasikilizaji, Salman Farsi alikuwa karibu sana na Mtume wa Mwenyezi Mungu na akisifika kwa sifa bora za uchaji-Mungu. Daima Mtume alikuwa akimsifu na kumtolea mfano bora wa elimu, akhlaqi na imani thabiti ya dini. Ni kutokana na elimu, ujuzi na maarifa yake makubwa ya kidini ndipo Mtume akamfadhilisha na kumuweka karibu naye. Mtume alikuwa akisema: "Salman ni bahari ya elimu ambayo kina chake hakiwezi kufikiwa." Imam Swaqid (AS) pia amesema: "Mtume Mtukufu (SAW)na Ali (AS) walikuwa wakimwambia Salman siri ambazo watu wengine hawakuwa na uwezo wa kuzidiriki na wakimchukulia kuwa mtu aliyefaa kulinda elimu na siri zilizofichika. Ni kutokana na hali hiyo ndipo akajulikana kwa moja ya lakabu zake, yaani 'Muhadith'.

Salman daima alikuwa akitetea na kumlinda Mtume (SAW). Baada ya kuaga dunia Mtume alikuwa mmoja wa watu wachache walioendelea kuwa na mwamko na kutetea dini kwa nguvu zao zote. Hakusita hata kidogo katika kumtetea imamu wa haki baada ya Mtume. Alikuwa akitumia kila fursa kutetea haki na akiwasihi Waislamu kumfuata Imam Ali (AS) baada ya kuaga dunia Mtume (SAW). Alikuwa akisema mara kwa mara: "Ali (AS) ni mlango uliofunguliwa na Mwenyezi Mungu. Kila anayeingia kwenye mlango huo ni muumini na kila anayetoka humo ni kafiri." Alikuwa na nafasi muhimu mbele ya Imam Ali kwa kadiri kwamba mtukufu huyo alimpa lakabu ya 'Luqman Hakim'. Baada ya kuaga dunia Salman, watu walimuuliza Imam Ali kumuhusu naye akajibu: "Alikuwa miongoni mwetu na mpenzi wa Watu wa Nyumba ya Mtume. Je, mnaweza kumpata mtu mwingine anayefanana na Luqman Hakim? Alikuwa na elimu kubwa na kusoma vitabu vya mitume waliopita. Kwa hakika alikuwa bahari ya elimu na maarifa."

Salman Farsi pia alikuwa na nafasi muhimu katika vita vya Waislamu walivyopigana baada ya kuaga dunia Mtume. Katika vita vya kutekwa Madain, mji mkuu wa wakati huo wa ufalme wa Wasasani, na baada ya kupita miaka mingi, Salman alikutana na Wairani wenzake na kuzungumzia udugu na usawa uliokuwa katika mafundisho ya Uislamu. Jambo hilo lililainisha nyoyo zao na kuwafanya wasimamishe vita. Moja ya malengo ya Salman Farsi katika vita hivyo lilikuwa ni kuondoa dhulma ya kimatabaka iliyokuwa ikitawala katika kipindi hicho nchini Iran. Wanahistoria wanasema kuwa licha ya vita vilivyotajwa, Salman pia alikuwa na nafasi muhimu katika kutoa ushauri wa kijeshi na kuongoza majeshi ya Kiislamu katika vita vya Hums na Damascus katika Syria ya leo.

Salman alipewa na khalifa wa pili madaraka ya kutawala mji wa Madain na alihudumia nafasi hiyo kwa muda wa miaka 19, yaani hadi wakati wa kuaga kwake dunia. Akiwa katika nafasi hiyo, na kinyume kabisa na tunavyowaona watawala waliowengi duniani, hali yake ya kifedha haikubadilika hata kidogo. Alikataa kabisa kutumia hata dinari moja aliyostahiki kutoka kwenye beitulmal na alikuwa akipata pato lake kutokana na kilimo alichokuwa akijishughulisha nacho kwa mikono yake miwili. Licha ya kuwa alikuwa mtawala wa Madain lakini alikuwa akivaa mavazi ya kawaida kabisa na ilikuwa vigumu kumtofautisha na watu wa kawaida mitaani.

Salman Farsi ana nafasi na heshima kubwa mbele ya Mashia na Masuni na kuna riwaya nyingi za Kiislamu zilizopokelewa kumuhusu. Mbali na kauli tuliyotaja mwanzoni mwa kipindi hiki kutoka kwa alim wa Kisuni Muhyi Deen Arabi kumuhusu Salman Farsi, alim mwingine mkubwa wa Kiislamu Sheikh Tusi pia ananukulu riwaya kutoka kwa Mansur bin Rumi katika kitabu chake cha Aamali kama ifuatavyo: "Siku moja nilimuuliza Imam Swadiq (as), 'Ewe Bwana Wangu! Mimi hukusikia ukimtaja sana Salman Farsi katika maneno yako. Nini sababu ya suala hili?' Alijibu, 'Usiseme Salman Farsi, sema Salman Muhammadi. Sababu ya mimi kumtaja kila mara ni kwa sababu alijipamba kwa sifa tatu muhimu: Ya kwanza ni kuwa alikuwa akitanguliza matakwa ya Bwana wake Amirul Mu'minim mbele ya matakwa yake, ya pili ni kuwa alikuwa akiwapenda sana masikini na kuwafadhilisha mbele ya matajiri na tatu ni kuwa alikuwa akipenda sana elimu na maulamaa.'"

Hatimaye Salman Farsi aliaga dunia ima mwaka 33 au 35 Hijiria akiwa na umri wa miaka 83. Imam Ali (AS) aliosha, kuvisha sanda na kisha kuuswalia mwili wake. Kaburi la sahaba huyo mtukufu wa Mtume (SAW) liko Madain yapata kilomita 35 kusini mwa Baghdad, mji mkuu wa Iraq.

Ni matumaini yetu kwamba sote tumenufaika na jibu la swali hili lililoulizwa na msikilizaji wetu Bwana Onoleka Andre wa Entebbe nchini Uganda. Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo panapo majaaliwa, tunakuageni kwa kusema, kwaherini.

 

 

 

Sauti na Video

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)