Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 15 Januari 2013 17:07

Kuhusiana na Sahaba Tha'laba + Sauti

Eneo la Badr, Saudi Arabia Eneo la Badr, Saudi Arabia

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kusikiliza kipindi kingine cha Uliza Ujibiwe. Kipindi cha wiki hii kinafunguliwa na swali kutoka kwa msikilizaji wetu Bwana Sayinguvu Mzee Alimasi wa Rumonge nchini Burundi. Mzee Alimasi anataka kujua iwapo sahaba wa Mtume Muhammad SAW anayejulikana kwa jina la Tha'laba aliaga dunia katika kipindi cha uhai wa Mtume SAW au la. Pia anata kufahamishwa kwa ufupi maisha ya sahaba huyu.

Tunajibu swali la smikilizaji wetu huyu kwa kusema kuwa kulikuwa na masahaba wengi wa Mtume waliojulikana kwa jina hili la Tha'laba na kwa hivyo ni vigumu kujua hasa ni sahaba gani anayekusudiwa hapa. Hata hivyo tutajaribu kuelezea kwa ufupi maisha ya baadhi ya masahaba wa Mtume waliojulikana kwa jina hili.

Mmoja wa masahaba hao ni Tha'laba bin Ghanama bin Uday bin Sinan, mkazi wa Madina. Alishiriki katika mapatano ya pili ya Aqaba. Baada ya kusilimu Tha'laba alivunja masanamu yote ya kabila la Bani Salama. Alishiriki na Mtume SAW katika vita vya Badr na Uhud na kuuawa shahidi katika vita vya Khandaq katika mwaka wa tano hijiria. Sahaba mwingine aliyekuwa na jina la Tha'laba ni Tha'laba bin Zeid bin Harith kutoka mjini Madina pia. Sahaba huyu ambaye alikuwa mwaminifu sana kwa Mtume SAW aliuawa shahidi katika vita vya Taif katika mwaka wa 8 Hijiria.

Tha'laba bin Sad ni sahaba mwingine wa Mtume aliyejulikana kwa jina hilo. Alikuwa mwana wa Sad bin Malik bin Khalid. Alipigana jihadi pembeni ya Mtume SAW katika vita vya Badr. Vita vya Uhud vilipowadia katika mwaka wa 3 Hijiria alipigana kwa ushujaa mkubwa na kuuawa shahidi na makafiri wa Qureish katika vita hivyo.

Sahaba mwingine wa Mtume aliyejulikana kwa jina la Tha'alaba ni Tha'laba bin Hatib Ansari ambaye alishiriki katika vita vya Badr na Uhud. Tarehe ya kuzaliwa na kuuawa kwake haijulikani. Baadhi ya wanahistoria wanasema kuwa aliaga dunia katika kipindi cha ukhalifa wa Omar alihali wengine wanasema aliuawa katika zana za ukhalifa wa Othman.

Wafasiri wa Qur'ani Tukufu wanasema kwamba aya za 75 na 76 za Sura at- Tauba ziliteremshwa kuhusiana naye. Inasemekana kuwa siku moja Mtume Mtukufu SAW alikuwa ameketi msikitini na wafuasi wake alipoingia Tha'laba bin Hatib na kujiunga nao. Alimwomba Mtume ombi moja kwa kusema: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Niombee dua ili Mwenyezi Mungu anipe mali nyingi."

Mtume alimtazama na kunyamaza. Tha'alaba alidhani kwamba angejibiwa kama angeendelea kusisitiza na kukariri ombi lake kwa Mtume. Kwa hivyo alirudia tena ombi lake hilo na mara hii akionyesha unyenyekevu wa kiwango fulani. Alisema: "Ewe Mtume! Sijui ni kwa nini nina hamu ya kuwa tajiri. Kila mara ninapofanya juhudi za kuufikia utajiri huo siupati!" Hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa Mtume kusikia ombi hilo kutoka kwa sahaba wake huyo bali alikuwa amelisikia mara kadhaa na kukaa kimya. Ama mara hii alimwambia: "Mali chache ambayo unaweza kuitumia vyema ni bora kuliko mali nyingi ambayo huwezi kuitumia vyema." Tha'laba alitaka kuzungumza lakini Mtume baada ya kunyamaza kidogo aliendelea kusema: "Ewe Tha'laba! Si ni vyema uyatazame maisha ya Mtume wako na kukinai?"

Baada ya kimya kifupi Mtume alisema: "Watu wengi huwa hawatekelezimajukumu ya Mwenyezi Mungu mara wanapopata mali nyingi." Baada ya kuyasikia maneno hayo ya Mtume Tha'laba alisema: "Naapa kwa jila la Mwenyezi Mungu ambaye alikuteuwa wewe kuwa Mtume kwamba, kama nitajaaliwa kuwa na utajiri mkubwa nitatekeleza majukumu na faradhi zote ninazotakiwa kutekeleza na Mwenyezi Mungu." Mtume ambaye aliona Tha'laba anaendelea kusisitiza juu ya msimamo wake na kutaka aombewe dua ya utajiri alimwombea hivi: "Ewe Mwenyezi Mungu! Mtekelezee Tha'alaba kile anachokiomba!" Haukupita muda mrefu kabla ya dua ya Mtume kujibiwa na Mwenyezi Mungu. Mtoto wa ami yake Tha'laba ambaye alikuwa mzee na tajiri mkubwa aliugua kwa muda na kisha kuaga dunia ambapo Tha'laba alirithi mali yake yote. Tha'laba alitumia utajiri huo kununua kondoo wengi na kujishughulisha na ufugaji mifugo. Baada ya muda, alifanikiwa sana katika shughuli hiyo ambapo idadi ya mifugo wake iliongezeka kwa haraka kwa kadiri kwamba hakupata tena malisho ya kutosha mjini Madina. Kwa hivyo aliamua kuhama Madina na kwenda kuishi katika kijiji kimoja kilichokuwa nje kidogo ya mji huo ili apate fursa ya kulisha mifugo wake kwa urahisi. Kijiji hicho kilimtosheleza vyema Tha'laba kwa ajili ya malisho ya mifugo wake wengi. Licha ya kuridhishwa na wingi wa mifugo hiyo na mafanilkio makubwa aliyoyapata katika uwanja huo lakini shughuli hiyo ilimzuia kushiriki katika swala za jamaa na kuamua kushiriki swala za Ijumaa tu jambo ambalo pia taratibu alizembea kulidumisha na mwishowe kutoshiriki kabisa katika swala hizo.

Baada ya kuteremka aya ya 103 ya Sura at-Tauba ambayo iliwawajibisha Waislamu kutoa zaka, Waislamu wote waliokuwa mjini Madina na ambao walikuwa na uwezo wa kutoa kodi hiyo ya Kiislamu walilazimishwa kuilipa. Baada ya hapo zamu iliwafikia wale waliokuwa wakiishi nje ya mji, hivyo Mtume akawatuma watu wawili ili wachukue zaka kutoka kwa Tha'laba. Idadi ya mifugo ya Tha'laba ilikuwa kubwa kiasi kwamba ilimwezesha kutoa zaka bila matatizo yoyote, lakini alikataa kufanya hivyo mara tu wajumbe wa Mtume walipomjia na kumuomba atoe zaka. Alisema: "Aah, mashaka ya maisha! Mwambieni Mtume kwamba maisha ya Tha'laba ni mabaya sana na kwa hivyo hawezi kutoa zaka ya mifugo wake!"

Wakusanyaji zaka ambao walikuwa wakijua vyema utajiri wa Tha'laba, na wakifahamu kwamba mamia ya kondoo waliowaona njiani walikuwa ni wake walishangaa na msimamo huo na kumuuliza: "Tha'laba unawezaje kutamka maneno hayo ilihali unafahamu vyema kwamba wewe ni mmoja wa wamiliki wakubwa wa kondoo pambizoni mwa mji wa Madina?!" Huku akiwa na uso uliojaa huzuni alisema: "Mliona kondoo njiani na kudhani kwamba ni wa Tha'laba. Hata kama itakuwa ni hivyo, lakini jueni kwamba kandoo wanene na walio salama wanatokana na malisho mazuri na uchungaji mkubwa, jambo ambalo humletea mtu matatizo na machungu mengi. Ni vipi Tha'laba anaweza kuvumilia machungu haya yote?!"

Mmoja wa wakusanyaji zaka alisema: "Tha'laba! Sisi tumetumwa hapa na Mtume wa Mwenyezi Mungu ili tuchukue haki unazopaswa kutoa kwa ajili ya wanaozistahiki. Elewa kwamba kutoa haki za kisheria kutakuwa na baraka za kuongezeka mifugo wako humu duniani na kupata thawabu za Mwenyezi Mungu huko Akhera."

Tha'laba alicheka kwa kejeli na kusema: "Nina swali: Ninataka kujua iwapo kuna tofauti kati ya zaka na jizia." Afisa yule wa ukusanyaji zaka ambaye hakuwa amefahamu vyema kusudio la swali la Tha'laba alimuuliza: "Yaani wewe haufahamu tofauti ya mambo haya mawili?" Tha'laba akajibu: "Watu wasiokuwa Waislamu wanaoishi chini ya himaya na ulinzi wa Waislamu huwa wanatozwa kodi inayoitwa jizia, ni kweli au si kweli? Zaka pia ni aina ya jizia ambayo sisi Waislamu tunapasa kuitoa. Sasa niambieni, je, Waislamu na wasiokuwa Waislamu wanapasa kutoa jizia au la?

Afisa mwingine wa ukusanyaji zaka akamjibu Tha'laba kwa kusema, "Zaka ni haki ya wanyonge na wahitaji wa Kiislamu ambayo Mwenyezi Mungu amewatengea kutoka kwa matajiri na inatofautiana na jizia." Tha'laba aliinamisha chini kichwa chake ikiwa ni alama ya kupinga maneno ya afisa huyo na kusema: "Hakuna tofauti yoyote kati ya zaka na jizia; hii ni fikra na imani yangu ambayo nimewaza sana juu yake." Maafisa hao wa ukusanyaji zaka ambao walishuhudia ujanja, ukorofi na inadi kutoka kwa Tha'laba waliinamisha chini vichwa vyao huku wakiwa wamekata tamaa. Ilifahamika wazi kwamba kwa kutoa dalili hizo batili na zisizo na msingi Tha'laba alitaka kukwepa kutoa zaka. Mmoja wa maafisa hao alitaka kutoa hoja ya mwisho kwa kusema: "Tutakaporejea Madina tumwambie nini Mtume wa Mwenyezi Mungu...?' Hata kabla hajamaliza kuuliza swali hilo, Tha'laba alimkatiza kwa makelele na kumwambia: "Hakuna! Tusijisumbue. Mwambieni Mtume kwamba Tha'laba ima hataki au hana uwezo wa kutoa zaka..." Baada ya hapo aliwapa mgongo wajumbe wawili hao wa Mtume na kwenda zake bila kusema neno jingine lolote.

Wakusanyi kodi hao walirejea mjini Madina na kumueleza Mtume SAW mambo yalivyokwenda walipokutana na Tha'laba. Mtume alisikitika sana aliposikia maneno aliyonukuliwa kutoka kwa Tha'laba na kusema: "Ole wake Tha'laba! Ole wake Tha'laba!

Muda si mrefu Malaika Jibril alimteremshia Mtume aya za 75 na 76 za Suratu Tauba zinazosema: Na miongoni mwao (hao wanafiki) wako waliomuahidi Mwenyezi Mungu kuwa: "Akitupa katika fadhila zake tutatoa sadaka na tutakuwa miongoni mwa wanaotenda mema." Lakini alipowapa hizo fadhila zake, walizifanyia ubakhili na wakakengeuka, nao (mpaka hivi sasa) wanakengeuka.

Inasemekana kuwa baada ya Tha'laba kusikia kwamba aya hizo ziliteremka kwa ajili yake alimwendea Mtume kwa madhumuni ya kutaka kutoa zaka lakini Mtume SAW aliikataa na kusema kuwa Mwenyezi Mungu alikuwa amemkaza kupokea zaka kutoka kwake. Baada ya kuaga dunia Mtume Tha'laba aliwapelekea makhalifa waliotawala baada yake sadaka hiyo lakini nao pia waliikataa kwa kumfuata Mtume SAW. Ni kutokana na hali hiyo ndipo Qatada bin Diama, mwanahadithi mashuhuri wa karne ya pili na Said bin Jubair fakihi aliyeishi mwishoni mwa karne ya kwanza hijiria wakamtaja Tha'laba kuwa mzuiaji sadaka. Naye Maqrizi, mmoja wa wanahistoria mashuhuri wa Misri aliyeishi katika karne ya nane na tisa hijiria alimtaja Tha'laba kuwa miongoni mwa wanafiki.

Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji........

 

 

 

 

Sauti na Video

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)