Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 13 Januari 2013 16:39

Dini za wachache nchini Iran

Ndani ya moja ya makanisa maarufu ya Tehran, Iran Ndani ya moja ya makanisa maarufu ya Tehran, Iran

Assalaam aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na karibuni kusikiliza kipindi tulichokuandalieni kwa wiki hii cha Uliza Ujibiwe. Kipindi hiki kinafunguliwa na swali la msikilizaji wetu Daudi Omary Luhende wa mjini Dar es Salaam Tanzania ambaye anataka kujua iwapo nchini Iran ambayo ni nchi ya Kiislamu, kuna wafuasi wa dini nyinginezo zisizokuwa  za Kiislamu.

Tunamshukuru Bwana Luhende kwa swali lake hili ambalo tunalijibu kwa kusema kwamba Iran ni nchi ambayo imekuwa na wafuasi wa dini zisizokuwa za Kiislamu kwa karne nyingi wafuasi ambao wamekuwa wakishirikiana kwa karibu na kuishi pamoja kwa amani na wananchi wenzao wa Kiislamu. Wafuasi wa dini za wachache nchini Iran wana haki zote za kiraia na kijamii, bali katika baadhi ya sehemu wana haki nyingi zaidi kuliko zile yanazopaswa kupewa makundi ya wachache. Kwa mfano wanawakilishwa bungeni na wabunge ambao kimsingi hawapasi kuwa nao kutokana na uchache wa idadi yao nchini. Wafuasi hao wa dini za wachache ambao kimsingi ni karibu watu laki mbili hivi wana wabunge watano bungeni wanaolinda na kutetea maslahi yao nchini. Waarmenia wanawakilishwa na wabnge wawili, Waashuri mbunge mmoja Wakalimi mbunge mmoja na Wazartoshti mbunge mmoja.

Kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wafuasi wa dini za wachache nchini wana uhuru kamili wa kutekeleza ibada na shughuli zao za kidini bila kubughudhiwa na yeyote. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Waislamu wote kwa ujumla wana wajibu wa kuwatendea wema na uadilifu wafuasi wa dini nyingine. Wanawajibika kwa mujibu wa mafundisho ya dini yao tukufu ya Kiislamu kulinda na kuheshimu haki za kiutu za wafuasi hao wa dini zisizo za Kiislamu. Wakristo ndio wanaounda idadi kubwa zaidi ya wafuasi wa dini za wachache, nao ni wa jamii ya Waarmenia. Kaumu ya Kiarmenia ilianza kuishi katika milima ya Armenia katika milenia ya pili kabla ya kuzaliwa Nabii Isah Masih (as), na walikuwa watu wa kwanza kuukubali Ukristo kuwa dini yao rasmi. Katika kipindi hicho baadhi ya Waarmenia walihamia katika maeneo na miji mbalimbali ya Iran na kuishi huko. Waarmenia wana karibu makanisa 200 nchini ambapo tatu kati ya hayo yameorodheshwa katika athari za kale za Iran kutokana na ukongwe wa historia yake. Jumuiya 50 za kiutamaduni, michezo na mambo ya heri ni baadhi tu ya suhula zinazomilikiwa na jamii ya Waarmenia nchini Iran. Miongoni mwa taasisi na jumuiya hizo za kiutamaduni na kimechezo ni uwanja wa michezo wa Ararat mjini Tehran ambao ni moja ya viwanja muhimu vya michezo nchini. Jamii ya Waarmenia tokea zamani imekuwa mmiliki mkubwa wa taasisi za kiutamaduni na uchapishaji wa majarida pamoja na magazeti tofauti nchini ambapo mengine huuzwa nje ya nchi kwa ajili ya wasomaji wake. Waarmenia wana shule 50 nchini ambapo Waislamu hawana haki ya kusoma humo lakini wakati huohuo wanafunzi wa Kiarmenia wanaruhusiwa kusoma katika shule za Waislamu.

Waashuri ni jamii nyingine ya Wakristo wa Iran. Idadi ya Waashuri duniani inapata watu milioni moja na laki mbili na wengi wao wanaishi katika nchi za Iran, Iraq na Marekani. Hivi sasa wafuasi 10,000 wa jamii hii wanaishi nchini Iran. Jamii hii ina makanisa 59 mjini Urumia pekee. Kila mwaka kiongozi wa jamii hii huishi Iran kwa muda wa mwezi mmoja hadi miwili. Jamii hii pia kama walivyo Waarmenia, ina shule zake yenyewe licha ya kuwa na haki ya kunufaika na shule za kitaifa za Iran. Mbali na jamii hizi mbili kuna makundi mengine ya Kikristo yanayoishi katika pembe mbalimbali za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.  Kwa mfano kuna Wakristo wa madhehebu ya Katoliki. Wakristo hawa wanagawanyika katika makundi matatu tofauti ya Wakatoliki Waarmenia, Wakatoliki Waashuri Wakaldoni na Wakatoliki Walatini. Jamii ya Wakatoliki nchini inasimamiwa na Baraza la Maaskofu.

Jamii nyingine isiyokuwa ya Waislamu nchini Iran ni ya Mayahudi. Kuwepo nchini Iran makaburi ya manabii na wakuu wa kidini wa Mayahudi, kama vile Nabii Danieli katika eneo la Shush, Habaquq huko Tuweisarkan na wafuasi wake Hanania, Mishail na Uzernia  katika mji wa Qazween, ni dalili ya wazi inayothibitisha kuishi hapa nchini Mayahudi tangu zama za kale. Idadi ya Mayahudi wanaokisiwa kuishi nchini Iran ni kati ya 25,000 hadi 30,000 ambapo 9000 hadi 10,000 wanaishi mjini Tehran. Mayahudi wana vituo na taasisi nyingi za kiutamaduni mjini Tehran na kwingineko ambapo wana uhuru wa kutekelezea humo shughuli zao za kidini na kiutamaduni bila matatizo.

Wazartoshti ni jamii ya tatu isiyo ya Kiislamu nchini Iran. Uzartoshti nchini Iran ulianza baada ya kudhihiri Asho Zartosht. Katika kipindi cha watawala wa Makhamanesh humu nchini yapata miaka 2500 liyopita,  wananchi wengi wa Iran wakiwemo wafalme walikuwa wafuasi wa dini ya Kizartoshti, bila ya dini hiyo kuchukuliwa kuwa dini rasmi. Wasasani watawala waliotawala Iran kabla ya kuingia nchini humu dini tukufu ya Kiislamu, ndio walioifanya dini ya Zartoshti kuwa dini rasmi nchini. Katika karne ya saba Milaadia wakati Uislamu ulipoingia Iran, Wairani wengi walisilimu na dini hii tukufu kutangazwa kuwa dini rasmi kitaifa. Idadi ya Wazartoshti wanaoishi humu nchini ni 20,000 ambapo wametawanyika katika miji tofauti na hasa katika miji ya Tehran, Kerman, Yazd, Shiraz, Isfahan, Zahedan na Ahwaz. Wazartoshti wana shule 9 mjini Tehran na 8 katika mikoa mingine ya Iran. Kuwepo shule hizo maalumu za Wazartoshti nchini hakuna maana kwamba wanafunzi wa dini hiyo wanakatazwa kusoma katika shule nyingine za Iran bali wanaruhusiwa kujiunga na shule nyingine zote za kawaida nchini. Kama zilivyo jamii za wafuasi wa dini nyingine za wachache nchini, Wazartoshti pia wamepewa fursa ya kuwa na vituo na taasisi zao maalumu za kiutamaduni ambapo wanaweza kujumuika humo na kujadili masuala yanayowahusu. Wana majarida na magazeti yapatayo 10 ambayo hujadili na kuchambua masuala tofauti ya Wazartoshti katika nyanja za kijamii, kidini na kiutamaduni.

Licha ya kuwepo dini za wachache nchini Iran, lakini nukta ya kuvutia hapa ni hii kwamba wafausi wa dini hizo hushirikiana bega kwa bega na raia wenzao wa dini ya Kiislamu katika kutekeleza majukumu yao ya kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni kwa maslahi ya taifa zima bila kujali tofauti zao za kidini. Mfano huo mzuri wa ushirikiano kwa maslahi ya taifa huonekana wazi katika nyanja mbalimbali za ujenzi wa taifa, kukabiliana na majanga ya kimaumbile pamoja na kupambana na maadui wanaojaribu kuhatarisha usalama wa nchi. Katika kipindi cha uvamizi na vita vya kulazimishwa vya dikteta Saddam Hussein wa Iraq dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, wafuasi wa dini za wachache nchini walionyesha uzalendo wao mkubwa kwa kutuma vijana, madaktari na wauguzi wao katika medani ya vita ili kalinda ardhi ya Iran dhidi ya hujuma ya adui aliyekuwa akiungwa mkono kwa hali na mali na nchi karibu zote za Maghari na Kiarabu. Wengi wa Waiarani hao wazalendo waliuawa, kujeruhiwa na kutekwa mateka kwa ajili ya kulinda nchi yao. Wafuasia hao wa dini za wachache pia walitoa msaada mkubwa wa kifedha kwa ajili ya kugharamia masuala ya vita. Mchango wao pia umekuwa ukionekana na kuhisika wazi wakati majanga tofauti kama ya mitetemeko ya ardhi na mafuriko yanapotokea nchini. Baada ya kumalizika vita vya kulazimishwa dhidi ya Iran, wafuasi hao wa dini za wachache walionyesha uzalendo wao wa dhati kwa nchi kwa kushiriki katika miradi mbalimbali ya ukarabati na ujenzi wa taifa. Ni kutokana na uzalendo na mchango huo ndipo wafuasi hao wa dini za wachache wakaheshimiwa na serikali na kupewa haki zao zote za kikatiba na kiutu nchini Iran.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)