Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 30 Disemba 2012 19:43

Muda aliokaa Mtume Muhammad SAW katika pango la Thaur

Muda aliokaa Mtume Muhammad SAW katika pango la Thaur

Hamjambo  wapenzi wasikilizaji na karibuni kusikiliza kipindi tulichokuandalieni kwa juma hili cha Uliza Ujibiwe. Kipindi hiki kitaanza kwa kujibu swali la msikilizaji wetu  Bwana Yaaqubu Saidi Idambira wa Kakamega nchini Kenya ambaye anataka kujua muda aliotumia Mtume Muhammad (saw) na Abu Bakr katika pango la Thaur huko Hijaz.

Huku tukimshukuru msikilizaji wetu huyo kwa swali hili, tunalijibu kwa kusema kwamba makafiri na maadui wa Mtume mjini Makka walikuwa na njama ya kumuua kabla ya kuhajiri kwake kwenda Madina. Lakini Mwenyezi Mungu alibatilisha njama hiyo na kumuepusha mtume wake na hatari hiyo kubwa kwa njia ya muujiza. Katika mwaka wa 13 wa kubaathiwa Mtume (saw) na kufuatia mkataba wa pili wa Aqabah uliotiwa saini kati ya Mtume na watu wa Yathrib yaani Madina, watu hao walimwalika mtume aelekee katika mji wao na kuahidi kumlinda dhidi ya hujuma ya kabila la Qureish lililopanga kumuua na kuvuruga juhudi zake za kuwalingania watu na kuwatoa kwenye ujahili. Siku ya pili baada ya kutiwa saini mkataba huo, Waislamu wa Makka walianza kuhama taratibu kutoka mji huo kuelekea Madina. Wakuu wa Qureish ambao waligundua mpango huo na kuhisi hatari, walianza kupanga njama ya kuuvuruga. Walikutana katika Dar an-Nad'wa ambayo ilikuwa majlisi ya mashauriano mjini Makaa ili kupanga mikakati ya kukabiliana na dini tukufu ya Kiislamu na kusimamisha ujumbe wa Mtume (SAW).

Kila mmoja katika majlisi hiyo alitoa maoni na mawazo yake hadi fursa ilipomfikia Abu Jahl ambaye alisimama na kusema: "Mimi nina fikra sahihi kuhusua suala hili na wala siiamini fikra nyingine isiyokuwa hii. Tutamchagua kijana mmoja shujaa na mpiganaji hodari kutoka kila kabila na kisha kuwapa mapanga makali ambayo watayatumia katika kumshambulia kwa pamoja Muhammad. Kwa njia hii umwagaji damu yake utalihusu kila kabila lililoshiriki katika mauaji hayo, na sidhani kama ukoo wa Bani Hashim utaweza kukabiliana na koo nyinginezo zote za Qureish. Kwa hivyo utakubali kulipwa fidia na sisi kwa upande wa pili tutakuwa tumeondokana na Muhammad."

Mwenyezi Mungu alimfahamisha mtume wake njama hiyo ya mushrikina kama tunavyosama katika aya ya 30 ya Surat al-Anfal: "Na (kumbuka Ee Nabii Muhammad) walipokufanyia hila wale waliokufuru ili wakufunge au wakuue au wakutoe (kwa hali mbaya katika Makka); na wakafanya hila (zao barabara); Na Mwenyezi Mungu akazipindua hila hizo. Na Mwenyezi Mungu ni mbora wa kupindua hila (za watu wabaya)."

Mtume alitumia mbinu ya kupoteza nyayo na alama na kwa msingi huo katika usiku ambao makafiri walikuwa wamepanga kumuu, alishauriana na Imam Ali (as) na kumuomba alale kwenye kitanda chake badala yake. Katika usiku huo unaojulikana kwa jina la Leilatul Mabit, Imam Ali (as) alilala kwenye kitanda cha Mtume ili kuwahadaa maadui na hivyo kuokoa roho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu. Imam Ali alichukua hatua ya kuhatarisha roho yake mwenyewe kwa kukubali kulala katika kitanda cha Mtume huku akifahamu vyema kwamba makafiri wa Makka walipanga kumshambulia na kumuua Mtume kwenye kitanda hicho. Alifanya hivyo ili kumpa Mtume fursa ya kukimbia na kwenda kwenye pango la Thaur lililoko kusini mwa Makka. Baadhi ya wanahistoria na wafasiri wa Qur'ani Tukufu kama vile Imam Muhammad Ghazali katika kitabu chake cha Ih'yaul Ulum, Tabari katika kitabu cha Tarikh al-Tabari, Ibn Hisham katika kitabu chake cha  Siratu Ibn Hisham na Ahmad Yaaqubi katika kitabu chake cha Taarikh Yaaqubi wanasema kwamba aya ya 207 katika Surat al-Baqarah inayosema: "Na kuna katika watu, wauzao nafsi zao kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu ni mpole kwa watumwa wake", iliteremka kusifu kujitolea kwa Imam Ali katika usiku ule wa Leilatul Mabit. Historia ya Kiislamu inasema kwamba Abu Bakr aliandamana na Mtume katika safari hiyo.

Asubuhi ilipofika maadui walielekea katika nyumba ya Mtume na kuanza kumtafuta ili wamuue lakini walimkuta Imam Ali (as) akiwa amelala kwenye kitanda chake. Kwa msingi huo Mwenyezi Mungu alivunja njama za maadui wa Makka dhidi ya Mtume wake. Bila kupoteza wakati waliamua kufuata nyayo za Mtume hadi mbele ya pango alimokuwa amejificha Mtume na Abu Bakr. Lakini walipofika mbele ya pango hilo walikuta utando wa buibui ukiwa umetanda mlangoni jambo lililowafanya watilie shaka kuwepo mtu ndani yake. Walijadiliana na kuhoji kwamba kama Mtume angekuwa kwenye pango hilo utando wa buibui haungekuwa mlangoni na kwa hivyo wakaamua kutoingia humo kumtafuta Mtume.

Inasemekana kwamba Mtume alikaa kwenye pango la Thaur kwa muda wa siku tatu na hatimaye kutoka humo na kuelekea Madina baada ya maadui kumsaka katika pori zote za Makka na kukata tamaa ya kumpata. Historia ya Kiislamu inasema kuwa katika usiku wa nne na kwa amri ya Mtume Mtukufu (saw), Imam Ali (as) alimtuma mfuasi mwaminifu kwenye pango hilo  ili ampelekee Mtume ngamia watatu ambao waliwatumia kwenda Yathrib.

Tunajifunza kutokana na kisa hiki kwamba Mwenyezi Mungu ni muweza wa kila jambo na kwamba huwanusuru mitume, mawalii na waja wake wema katika mazingira magumu zaidi yanayowakabili na kuvunja njama za maadui wao.

Swali la pili linatoka kwa msikilizaji Hussein Haffani wa mjini Jeddah Saudi Arabia ambaye anauliza swali lake hivi; nchini Sudia ada imekuwa kwamba madereva wa malori ya mizigo wanaofanya makosa barabarani, kwa mfano kupindukia kasi iliyoainishwa wamekuwa wakitozwa faini ya kati ya riale 150 hadi 300. Wahalifu wanapokosa uwezo wa kulipa faini mara moja wamekuwa wakipewa fursa ya hadi miaka miwili kuweza kulipa faini hiyo kwa sharti kwamba wasisafiri nje ya nchi. Lakini hivi karibuni sharia hiyo imebadilishwa na kuwa kwamba kama dereva atafanya kosa barabarani na kutolipa faini katika wakati ulioainishwa faini hiyo itaongezeka taratibu na hata kufikia mara mbili zaidi ya kile kiwango alichotakiwa kulipa mwanzoni. Sasa Bwana Haffani anataka kujua kama fedha hizo zinazoongezeka taratibu na hata kuwa mara mbili zaidi ya kiasi cha awali ni riba au la.

Tunamjibu msikilizaji wetu huyu kwa kumwambia kwamba fedha hizi za ziada si riba. Malipo ya fedha hizo za ziada ni faini ya kifedha anayoahidi mtu kulipa iwapo atavunja sheria zilizowekwa. Fedha za ziada zinazochukuliwa kutokana na mhalifu kuchelewa kulipa faini pia hujulikana kama faini ya kuchelewa kutekeleza jukumu. Riba katika sharia za Kiislamu ni fedha za ziada zinazotozwa juu ya mkopo wa fedha. Kwa maana kwamba wakati wa kutolewa mkopo, mkopeshaji humshurutisha mkopaji arudidhe mkopo ule ukiwa na  fedha za ziada juu. Riba ina mifano mingine mingi ambayo wakati hauturuhusu kuizungumzia hapa.

Kuhusu faini ya makosa ya madereva barabarani, wahalifu wanapasa kuepuka kulipa fedha za ziada kwa kulipa kwa wakati  faini wanazopaswa kulipa. Hii ni pamoja na kuwa nyongeza ya faini huenda ikapunguza makosa na ajali barabarani. Wataalamu wanasema kwamba ongezeko la faini ni jambo linalodhamini utekelezwaji sahihi wa sharia. Ni wazi kuwa hakuna fedha zinazobadilishanwa hapa ili isemekane kuwa riba imefanyika kwa kutolewa fedha za ziada juu ya zile za awali. Kwa msingi huo wanazuoni wanasema kuwa nyongeza ya fedha za faini si riba.

Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji ndio tumefikia mwisho wa kipindi chetu cha Uliza Ujibiwe kwa juma hili. Jiungeni nasi tena juma lijalo ili tuweze kunufaika zaidi na majibu ya wasikilizaji wetu wengine. Kwaherini.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)