Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 23 Disemba 2012 18:24

Uislamu na suala la radi + Sauti

Uislamu na suala la radi + Sauti

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kusikiliza kipindi cha Uliza Ujibiwe. Kipindi hiki kama mnavyokumbuka ni kuwa kilikuwa kikiwajieni hewani kila siku ya Jumanne na kurudiwa siku ya Jumatano lakini kilisimama kwa muda wa zaidi ya mwaka mmoja kutokana na mabadiliko yaliyotokea katika ratiba ya vipindi vyetu. Lakini baada ya kuondoka udhuru uliokuwepo, tumepata tena fursa ya kukipeperusha kipindi hiki kuanzia wiki hii. Aliye na bahati ya kutufungulia kipindi hiki si mwingine  bali ni Bwana Sayinguvu Mzee Alimasi wa Rumonge nchini Burundi. Mzee Alimasi anataka kujua jinsi radi na umeme vinavyotokea na iwapo kuna dalili na mtazamo wowote wa kidini kuhusiana na suala hilo. Karibuni wasikilizaji wapenzi tusikilize kwa pamoja jibu la swali hili.

Huku tukimshukuru Mzee Alimasi kwa swali lake hili tunaanza kulijibu kwa kusema kwamba radi na mwale au kwa ibara nyingine kimulimuli cha radi hutokea pale nguvu tulivu tofauti za umeme, yaani nguvu chanya na hasi zilizoko kwenye mawingu zinapogongana. Hali hiyo huongezeka na kupungua katika misimu mbalimbali ya mwaka kwa kuzingatia hali tofauti ya hewa. Kwa mfano hali hiyo ya radi, ngurumo na vimulimuli vya radi huongezeka katika misimu ya baridi na machipuo katika nchi zilizo na misimu hiyo ya hali ya hewa. Wakati mwingine nguvu za umeme huzalishwa pale nguvu chanya zilizoko kwenye mawingu zinapogongana na nguvu hasi ambazo kwa kawaida hupatikana kwenye ardhi na hivyo kuzalisha mwangaza mkubwa au vimulimuli ardhini. Mwangaza huo ambao kwa kawaida huandamana na nguvu kubwa za umeme mara nyingine husababisha moto na kuteketeza misitu au majengo yanayokumbwa na nguvu hiyo.

Suala la radi na umeme limezungumziwa katika aya tofauti za Qur'ani Tukufu na hata kuna sura nzima ambayo imetajwa kwa jina hilo la radi. Aya ya 13 ya sura hiyo inachukulia radi kuwa aina ya kumsabihi Mwenyezi Mungu. Vilevile Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 24 ya Suratu Rum kama ifuatavyo: Na katika Ishara Zake (za kuonyesha nguvu zake) ni kukuonyesheni umeme kwa (kukutieni) hofu na tamaa (ya kuja mvua) na kuyateremsha (hayo) maji kutoka mawinguni, kwayo huifufua ardhi baada ya kufa kwake. Bila shaka katika haya zimo Ishara kwa watu wanaofahamu.

Aya ya 12 ya Suratu Rad pia inasema kwamba radi na umeme huleta woga na matumaini ambayo hutokana na mawingu mazito. Hii ni kwa sababu wakati wa kutokea radi na umeme, mawingu mazito meusi na upepo hudhihiri hewani na kusababisha mvua kubwa. Hili ndilo suala linalozungumziwa na Mwenyezi Mungu katika aya iliyotajwa ambapo anasema kuwa mvua kubwa ambayo ni rehema Yake na ambayo huwa imebebwa kwenye mawingu mazito hunyesha baada ya kutokea radi na umeme mkali kwenye mawingu hayo. Mbali na hayo joto kali ambalo husababishwa na umeme unaotokana na mgongano wa nguvu chanya na hasi kwenye mawingu ambayo huwa yamebeba maji mazito yaliyo na gesi nyingi ya oksijeni hupelekea mvua nyingi kunyesha kutoka kwenye mawingu hayo. Maji hayo mazito huwa na athari kubwa katika kuua vijidudu na maradhi yanayosibu mimea. Ni kutokana na ukweli huo ndipo wataalamu wakasema kwamba kila mwaka unaoambatana na kiwango kidogo cha radi na umeme, hushuhudia pia kuongezeka kwa maradhi yanayodhuru mimea. Wakati huohuo, matone ya mvua ambayo huchanganyika na gesi ya kaboni ambayo husababishwa na joto kali linalozalishwa na umeme wakati wa kutokea radi, huzalisha asidi ya kaboni ambayo baada ya kuchanganyika na mada nyinginezo kwenye ardhi huunda moja ya mbolea bora zaidi duniani kwa ajili ya ukuzaji wa mimea bora. Jambo hilo limewafanya wataalamu kusema kuwa mbolea inayotokana na radi pamoja na umeme kwenye sayari ya dunia ni tani milioni kumi, kiwango ambacho ni kikubwa sana.

Moja ya athari muhimu zaidi za radi na umeme ni kunyesha mvua kubwa kwa sababu joto linalotokana na umeme huo huchoma hewa iliyo karibu na hivyo kupunguza shinikizo la hewa. Ni wazi kuwa mvua hunyesha katika kiwango hicho cha chini cha shinikizo la hewa na ndio maana ngurumo kali husikika mara tu baada ya kutokea radi na umeme. Katika hali hiyo ya kunyesha mvua, ardhi kavu, yenye joto jingi na iliyokuwa imekauka na kuwa mfano wa kitu kilichokufa, hupata maisha mapya. Maisha hayo mapya hudhihiri kwa sura ya maua ya kupendeza na mimea iliyo na afya, jambo ambalo huwafanya wengi kushangazwa na jinsi hali ya mambo inavyogeuka ghafla kutoka kwenye ardhi kavu iliyokufa na kuwa yenye uhai iliyojaa maua na mimea ya kuvutia. Mbali na hayo, Mwenyezi Mungu anaashiria mwishoni mwa aya hiyo kundi la watu wanaotadabari na kutumia vyema akili zao kuhusu suala hili. Anasema kwamba watu hao hufikia natija hii kwamba bila shaka kuna nguvu kubwa iliyo nyuma ya mambo hayo yanayotokea kwa mpangilio maalumu ardhini kwa manufaa ya mwanadamu. Kwa ibara nyingine ni kuwa watu hao hufikia uamuzi huu kwamba mambo hayo hayawezi kutokea hivihivi bila ya kuwepo nguvu kubwa ambayo huandaa na kuyaongoza mambo hayo ili yapate kutekelezeka kwa utaratibu maalumu.

Ni baada ya kuzingatia matukio hayo muhimu ya kielimu ndipo tunapotambua adhama ya kielimu ya kitabu kitakatifu cha Qur'ani Tukufu ambacho kilizungumzia suala hili muhimu la radi na umeme na faida zake kwa jamii ya binadamu karne nyingi zilizopita, hata kabla ya kuwadia zama za kufanyika ugunduzi wa kielimu na kisayansi wa jambo hilo. Bila shaka jambo hilo mwishowe humfanya mwanadamu kumtambua muumba wake ambaye si mwingine bali ni Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala.

Swali la pili la kipindihiki linatoka kwa msikilizaji wetu Bwana Yaaqubu Saidi Idambira wa Kakamega nchini Kenya ambaye anataka kujua mtu aliyevunja sanamu la Uzza.

Tunalijibu swali hili, ambalo huenda tusifanikiwe kulikamilisha kutokana na mbano wa wakati, kwa kusema kuwa, dini tukufu ya Kiislamu imefanya juhudi kubwa kwa ajili ya kupambana na shirki, fikra potofu pamoja na kuabudiwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu mmoja. Uislamu unapinga miungu mingi kwa sababu iwapo dunia itaongozwa na miungu hiyo ni wazi kuwa mfumo wa uongozi wa dunia utasambaratika. Qur'ani Tukufu daima inamsihi mwanadamu kumuabudu Mwenyezi Mungu mmoja tu. Kwa msingi huo iwapo mwanadamu atadai na kuamini kuwa viumbe na vitu vyote vilivyomo humu duniani vinajiendesha vyenyewe bila ya kumtegemea Mwenyezi Mungu, mtu huyo atakuwa amekufuru na kumshirikisha Mwenyezi Mungu.

Mtume Muhammad (saw) alikuja katika kipindi ambacho mji wa Makka ulikuwa umeghubikwa na ujahili na imani potofu. Kutokana na utamaduni na imani hiyo potofu, Waarabu wa zama hizo waliabudu masanamu waliyojitengenezea kutokana na bao, mawe na tende. Imani na mila hiyo ilikuwa kama mnyororo uliofungwa na kufuli kwenye mikono na miguu yao. Ni katika kipindi hicho ndipo Uislamu ulipodhihiri na kubatilisha imani, shiriki na fikra hizo za kijahili za kuabudu masanamu yasiyosikia, kuona wala kuhisi chochote. Mtume Mtukufu (saw) daima alikuwa akipambana na miungu ya upotofu na shirki. Alikuwa akiwakumbusha watu kwamba miungu na masanamu hayo hayakuwa na uwezo wa kufanya chochote wala kuwakidhia mahitaji yao kwa sababu ni vitu vilivyotengenezwa kwa mikono ya wanadamu. Kila kitu na kiumbe kilichomo humu duniani kimetengenezwa na kuongozwa na Mwenyezi Mungu. Qur'ani Tukufu inasema hivi katika aya ya 23 ya Suratu Najm: Hayakuwa haya (majina ya Lata, mungu mwanamke, na al Uzza, mungu mwanamke mwenye enzi na Manata, mungu mwanamke anayeneemesha) ila ni majina tu mliyowapa nyinyi na baba zenu (masanamu hayo; wala hawana lao jambo). Mwenyezi Mungu hakuteremsha dalili juu ya hayo. Hawafuati ila dhana na zinayoyapenda nafsi (zao). Na kwa yakini uwongofu umewajia kutoka kwa Mola wao (lakini hawataki tu kuufuata).

Wapenzi wasikilizaji, inaonekana wakati hauturuhusu tena kuendelea na kipindi hiki. Hivyo, tunakuombeni mjiunge nasi tena juma lijalo ili tupate kunufaika na majibu ya wasikilizaji wetu wengine, ambapo pia tutamaliza kujibu swali la msikilizaji wetu Yaqubu Saidi Idambira wa Kakamega Kenya. Kwaherini.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)