Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 16 Februari 2016 14:24

Ufeministi, itikadi na misingi yake (20)

Ufeministi, itikadi na misingi yake (20)

Karibuni kuwa nasi tena katika sehemu nyingine ya kipindi cha Ufeministi, Itikadi na Misingi Yake. Katika baadhi ya vipindi vilivyotangulia tuliashiria kwamba katika kuzungumzia masuala mengi ya kijamii, mafeministi walikumbwa na hali ya kuchupa mipaka kulia au kushoto. Miongoni mwa mijadala na mambo ambayo mafeministi walifeli na kushindwa kutokana na misimamo yao ya kuchupa mipaka na kupuuza uhakika wa masuala ya kijamii, ni suala la mitindo, uzuri au urembo. Kipindi chetu leo kitazungumzia mtazamo wa mafemenisti, jamii ya mabepari na mtazamo wa dini ya Uislamu kuhusu mitindo, fesheni na urembo.

Miongoni mwa masuala ya kijamii yaliyokuwepo katika zama zote za historia ya mwanadamu ni mtindo na uzuri na hamu ya wanadamu ya kuwa na mtindo. Neno “Mtindo” yaani mode au fashion katika lugha lina maana ya jinsi ya kufanya kitu kwa kufuata taratibu fulani, fesheni au staili, na katika istilahi lina maana ya mbinu ya muda ambayo huelekeza na kupanga dhuku na silika za watu wa jamii husika kwa kipindi fulani. Kufuata mtindo kuna maana ya mtu kutayarisha mavazi yake, mtindo wa maisha yake, aina ya mila na desturi za kukaribisha watu, kuamiliana na watu, kujiremba na kwa ujumla mwenendo wake kulingana na vigezo na fesheni mpya, na pale inapotokea fesheni na staili nyingine katika jamii, basi mtu huyo hufuata na kuiga fesheni na mtindo huo mpya. Wataalamu wa masuala ya jamii wanasema kuwa, mwenendo mpya wa jamii ambao bado haujakita mizizi na kuwa ada na desturi ya kijamii huwa ni “fesheni na staili ya kijamii”.

Mwenyezi Mungu SW amemuumba mwanadamu kwa namna ambayo daima hukimbia kuwa na hali moja na ya kutuama na kutaka mabadiliko na upya. Sifa hii ya mwanadamu ndiyo inayomuongoza kuelekea daraja za juu za ukamilifu na kwenye elimu mbalimbali na kuzidisha ubunifu na uvumbuzi mpya siku baada ya siku. Sifa hii huyaondoa maisha ya mwanadamu katika kuwa katika hali moja na ya kuchosha na kuyapa taharuki, utanashati na mvuto. Hapa ndipo tunapoweza kupata siri ya kwa nini mwanadamu anapenda kufuata fesheni na mtindo mpya akiwa katika jitihada za kutafuta ukamilifu zaidi, kujiondoa katika kuwa katika hali moja na kutafuta ukamilifu zaidi ambako daima huambatana na ujudi na uwepo wa kiumbe huyo. Kwa msingi huo fesheni na mtindo unaweza kuwa mzuri au mbaya. Ni wazi kuwa mtindo na fesheni nzuri ni matokeo ya kuchagua, ubunifu, kutafakari na uvumbuzi wa watu wa nchi au jamii moja, na pale uvumbuzi na ubunifu huo unapokuwa na misingi na mizizi katika itikadi za kidini na thamani za kitaifa na kibinadamu basi huwa sababu ya utanashati na hushibisha hisi ya mwanadamu ya kupenda upya, kuzidisha hali ya kujiamini, kustawisha vipawa na muawana na kuimarisha hisi ya kuheshimu na kuthamini mila na desturi na mahusiano ya kibinadamu na kifamilia.

Hata hivyo inatupasa kuelewa kuwa, fesheni na mtindo daima huwa haitokani na kutafakari au haitegemei utamaduni, mila na itikadi za taifa au watu wa jamii na nchi. Kwani wakati mwingine fesheni na mtindo huenezwa na kusambazwa na upande mmoja kwa njia hatari na kuja kama hujuma inayolenga watu wa taifa, kaumu na utamaduni mwingine. Watu hao hulazimishwa na kutwishwa fesheni na mtindo fulani kupitia njia mbalimbali zinazohisika na zisizo hisika. Inasikitisha kuwa, hii leo jamii ya kibepari inatumia nyenzo mbalimbali kama masoko na vyombo vya habari na vya mawasiliano ya umma kwa ajili ya kubadili mtindo wa maisha wa watu wengine duniani kwa maslahi yake kwa kutumia sekta hii ya fesheni na mitindo. Wanawake ni miongoni mwa malengo makuu ya mabepari kwa ajili ya kueneza na kusambaza fesheni na mitindo makhsusi inayokwenda sambamba na malengo na maslahi ya mabepari na masoko yao.   

Mafemenisti, wamekumbwa na hali ya kuchupa mipaka na kufurutu ada katika suala hili la mitindo na fesheni. Watu wa kundi hili wanaamini kwamba, juhudi za wanawake za kuremba sura na dhahiri zao zimewafanya kuwa wahanga wa sekta ya mitindo na fesheni na kuwa wanasesere na vibonzo vya wanaume. Mafeministi daima wamekuwa wakikosoa propaganda, filamu na fesheni za kisasa na wanaamini kuwa wanawake wanadhalilishwa katika filamu hizo na kufanywa chambo cha kushibisha matamanio ya wanaume.

Miongoni mwa mambo yanayokosolewa na mafeministi ni kuwa, fesheni na mitindo vinatwishwa kwa watu wa jamii kupitia viwanda vya mitindo na  vipodozi vinavyodhibitiwa na wanaume. Hata hivyo tunapotazama historia ya miaka mia na khamsini iliyopita ya sekta ya fesheni na mitindo, tunaona kuwa, sekta hiyo imekuwa mikononi mwa wanawake na matangazo mengi yanayohusiana na masuala ya urembo yamekuwa yakiandikwa au kutayarishwa na wanawake wenyewe.

Vita vya mafemenisti dhidi ya haja ya kimaumbile ya wanawake ikiwa ni pamoja na hamu yao ya kujiremba na kupendeza, vilizusha wimbi la upinzani na malalamiko ya wanawake. 

Katika upande mwingine unaokabiliana na mtazamo huu wa mafeministi, kuna mtazamo unaochupa mipaka katika kupigia debe kwa nguvu zote masuala ya fesheni na mitindo na kuwafanya wanawake kuwa watumiaji wa kudumu wa bidhaa za fesheni na mitindo. Kundi hili limeathiriwa zaidi na mtazamo wa Magharibi na utamaduni wa mfumo wa kibepari unaoeneza fesheni na mitindo kupita kiasi ukiwa na lengo la kubadilisha mtindo wa maisha wa watu wa dunia. Jamii ya mabepari inatumia fesheni, mitindo na vipodozi kuathiri masoko kwa ajili ya maslahi yao na kuwatumia vibaya wanawake. Hii leo sekta ya fesheni, urembo na vipodozi imekuwa sekta ya kudumu katika mfumo wa ubepari kwenye jamii za Magharibi hususan Marekani. Matangazo ya kuvutia watu, kutafuta na kushawishi masoko na wanunuzi hufanya mikakati ya kuzusha mahitaji bandia katika jamii kwa kubadili dhuku na silika za watu au kwa uchache kuzusha hali ya dukuduku ya kubadilisha mwenendo wa matumizi katika nafsi za watu wa jamii husika.

Mtazamo huu wa Magharibi kuhusu fesheni na mitindo umekuwa na taathira mbaya kwa thamani za kibinadamu za mwanamke, jamii na familia. Hii leo mfumo wa ubepari unaeneza baadhi ya mitindo na fesheni zenye hatari na madhara makubwa kupitia televisheni za satalaiti ambazo zinadunisha nafasi na hadhi ya mwanamke, kama fesheni za taratibu za kujikondesha zilizochini ya viwango, kutoboa pua, uchoraji au nakshi za tatoo, kubadilisha rangi ya ngozi (kujichubua au kujibabua) na kadhalika ambavyo mbali na madhara yake ya kijamii, husababisha hatari kwa mwili wa mwanadamu. Kwa mfano tu takwimu zinaonesha kuwa, nchini Marekani watu zaidi ya milioni 30 huingia katika chombo maalumu cha kubadilisha rangi ya ngozi zao kila mwaka, suala mabalo huzidisha kwa asilimia 70 hatari ya kupatwa na saratani ya Melanoma. Ni wazi kuwa, kutangaza na kupigia propaganda mitindo kama hii ni kueneza fesheni na mitindo yenye madhara kwa usalama wa mwili na roho ya mwanadamu.

Dini ya Uislamu imekuja na njia ya kati na kati na ya kiadilifu kuhusu masuala ya mitindo na fesheni. Dini hiyo inapinga mitizamo yote miwili iliyochupa mipaka ya uadilifu ya mafemenisti na mfumo wa ubepari na kutenganisha baina ya mitindo na fesheni nzuri na mbaya na hivyo kuwaokoa watu hususan vijana kutoka kwenye kinamasi cha mitindo isiyofaa.

Katika suala la kuchagua mitindo na fesheni, Uislamu ambao unakidhi mahitaji asili na ya kimaumbile ya mwanadamu, unaweka mbele maslahi ya mtu binafsi na jamii na umezuia na kuharamisha kila kitu chenye madhara na hatari kwa uzima na usalama wa mwili na roho ya mwanadamu. Uislamu umewahimiza sana wafuasi wake kuchagua mitindo mizuri na ya kupendeza ikiwa ni pamoja na kujipamba kwa nguo na mavazi safi, kuchana nywele na kuzifanya maridadi, usafi wa mwili, kuwa na harufu nzuri na kujitia uturi na marashi na kujiepusha na mambo yanayodunisha shani na hadhi ya mwanadamu. Pamoja na hayo yote dini ya Uislamu inasisitiza kuwa, vazi zuri na pambo maridadi zaidi la mwanadamu na linalomkurubisha zaidi kwenye ukamilifu ni pambo na vazi la takwa na uchamungu. Aya ya 26 ya Suratul Aaraf inasema: Enyi wana wa Adam! Tumewateremshia vazi lifichalo tupu zenu na vazi la pambo, lakini vazi la uchamungu ndilo bora zaidi..”

Ili kuweza kusalimika na athari mbaya za mitindo na fesheni mbaya, Uislamu umeweka mipaka maalumu kupitia sheria na mafundisho yake. Kwa mfano dini hiyo inatuamuru kujiepusha kuiga mitindo au kujifananisha na makundi au watu wasiofaa. Mtume Muhammad (saw) amesema: Msijifananishe na kaumu ya Mayahudi”.

Kwa muhtasari ni kuwa Uislamu umekubali na kuidhinisha hamu ya kutaka upya, mitindo ya nguo na mavazi kwa ujumla lakini kwa sharti kwamba vilinde utambulisho wa kidini, kihistoria na kiutamaduni wa visipingane na misingi na itikadi na sheria za Mwenyezi Mungu.  >>

Kipindi chetu kinaishia hapa kwa leo. Tukutane tena juma lijalo panapo majaaliwa ya Mwenyezi Mungu.  

      

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)