Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 07 Februari 2016 14:30

Ufeministi, itikadi na misingi yake (19)

Ufeministi, itikadi na misingi yake (19)

Ni wasaa mwingine wa kuwa nanyi tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa fikra na mitazamo ya mafeministi. Katika kipindi cha wiki iliyopita tulizungumzia mitazamo ya mafeministi ya kudhoofisha majukumu ya wanaume katika familia. Leo tutazungumzia majukumu muhimu ya baba hususan katika mtazamo wa Uislamu.

Mfumo wa mafeministi umepuuza sana moja ya majukumu muhimu zaidi ya wanaume ambayo ni pamoja na nafasi yake kama baba ndani ya familia na majukumu ya kulea watoto. Ni wazi kuwa, nafasi ya baba ndani ya familia ni muhimu sana na mafanikio yake yanahitaji uelewa, kujitolea, maadili na mwenendo mwema na itikadi sahihi. Baba ana nafasi na mchango mkubwa katika kuimarisha hali ya kujiamini ndani ya familia. Anawajibika kuchunga na kufuatilia malezi ya watoto na kuwatayarishia uwanja mzuri wa kustawi na kufikia ukamilifu wa kibinadamu. Kwa kutekeleza vyema majukumu yake, baba huwa dhihirisho la sheria, uadilifu na insafu mbele ya watoto na kimbilio salama kwa familia yake. Mwenendo wa baba unapaswa kuwa wa upendo na insafu, na uwezo wa baba huwa na taathira kubwa katika mustakbali wa watoto wake.

Kwa kawaida mtoto anapozaliwa huwa na uhusiano mkubwa na wa karibu zaidi na mama yake, lakini kadiri umri wake unavyokuwa hujenga na kuwa na uhusiano mkubwa zaidi na baba. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa, baba huingia zaidi katika maisha ya mtoto, akili na fikra zake. Hapa mtoto huanza kudiriki kuwa, baba ndiye kimbilio lake, dhihirisho la tadbiri, kiongozi na mtungaji sheria. Mtoto humuona baba kuwa shakhsia na nembo ya familia na hufanya jitihada za kutaka kujifananisha naye. Wataalamu wa elimu nafsi wanaamini kuwa, watoto hususan wale wa kiume katika kipindi cha umri wa miaka 3 hadi 6 humfanya baba kuwa kigezo cha kuiga. Baba huwa nembo ya nguvu, uwezo na dhamana ya familia kwa mtoto, na matarajio yote ya mtoto ni kutaka kuwa mithili ya baba.

Sambamba na hayo baba katika mtazamo wa mtoto, huwa dhamana ya mahitaji yake ya kimaisha. Baba ndiye mdhamini wa mahitaji ya familia na kadiri umri wa mtoto unavyokua hususan katika kipindi cha ujana, humuona mama kama dhihirisho la upendo na huruma, na baba kuwa ni dhamana ya maisha ya familia.

Wakati huo huo wataalamu wa elimu nafsi wanasema, baba hudhamini usalama wa mtoto na familia. Wakati hatari inapomkabili mtoto hukimbilia usalama kwa mama wakati wa utotoni, lakini kuanzia karibu kipindi cha miaka minne mtoto anayekabiliwa au kuhisi hatari hukimbilia usalama kwa baba yake. Baba pia huwa kituo cha elimu, fikra na maarifa kwa watoto wake. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, watoto hudhani kuwa baba zao hujua kila kitu. Si hayo tu hata wale watoto wenye mtazamo mbaya kuhusu baba zao huwatetea mbele ya wenzao na kusifia fikra, akili na uhodari wao.

Baba mwema wasikilizaji wapenzi, ana majukumu na nyadhifa muhimu. Miongoni mwa nyadhifa muhimu sana za baba akiwa pamoja na mama katika familia, ni kulea watoto. Mazingira ya familia ndiyo mazingira bora zaidi ya kulea na kustawisha watoto kwa sharti kwamba, baba na mama watekeleze ipasavyo majukumu yao. Malezi mema ya mtoto ndiyo haki kubwa zaidi ya watoto kwa wazazi wao. Baba katika uwanja huu ana nafasi ya moja kwa moja na anawajibika kumpa mtoto malezi na mafundisho ya maadili, adabu za kibinadamu na Kiislamu na mwenendo mzuri ili aweze kuwa na faida kwa familia na jamii yake katika siku za usoni.

Wazazi vilevile wanapaswa kufanya jitihada kubwa za kulea na kustawisha mwili, fikra, akili na uzima wa kiroho wa watoto wao. Wanalazimika kutumia mbinu sahihi na uwezo wao wote kuhakikisha wanastawisha uwezo wao wa kifikra, kiakili na kiroho sambamba na kudhamini mahitaji yao ya kimwili na kimaada. Wazazi wanawajibika kukuza vipawa vya sifa njema na maadili ya kibinadamu katika nafsi za watoto wao na kuwafunza thamani aali za kibinadamu na Kiislamu kama kujitolea, uungwana, uadilifu, insafu na kadhalika.             >>>>

Katika mtazamo wa Uislamu zahma na usumbufu wote anaostahamili baba mkabala wa familia yake hutambuliwa kuwa ni miongoni mwa majukumu yake ya kidini na kimaadili, sawa kabisa na mashaka na usumbufu anaopata mama katika kulea watoto na kutunza familia. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa, watoto huwa mithili ya wageni walioalikwa na baba na mama zao katika kitanga na meza ya familia; kwa msingi huo baba huwa na wadhifa na majukumu makubwa zaidi ya kuwashughulikia na kuwakirimu ipasavyo wageni hao. Mtume Muhammad (saw) amesema: “Mtu anayefanya jitihada kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya familia yake huwa sawa na mtu anayepigana vita vya jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu.”

Katika mtazamo wa dini, watoto wana haki kwa baba zao ambazo zimetiliwa mkazo sana. Miongoni mwa haki hizo ni kwamba mbali na ulazima wa kuwapa mafunzo ya maadili na mwenendo mzuri, baba pia wanawajibika kutafuta rizki ya familia kupitia njia za halali. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, rizki ya halali huwa na taathira kubwa katika hatima na mustakbali wa watoto. Imam Ali bin Abi Twalib (as) ambaye ni wasii wa Mtume wetu Muhammad (saw) amesema kwamba: “Msipeleke tonge la rizki ya haramu majumbani mwenu”. 

Miongoni mwa majukumu muhimu ya baba ni kuchunga dini na imani ya watoto wake. Mtume Muhammad (saw) amesema: Ninyi nyote ni wachungaji na nyote mutaulizwa kuhusu mlichochungisha. Mwanaume ni mchungaji wa familia yake na ataulizwa kuhusu alichokichunga. Mwanamke pia ni mchungaji wa familia, mume na watoto wake na ataulizwa kuhusu alichokichunga”, mwisho wa Hadithi. Uislamu wapenzi wasikilizaji umewapa thamani na hadhi maalumu wazazi wanaotekeleza majukumu yao ipasavyo kiasi kwamba aya za Qur’ani Tukufu zinazungumzia ulazima wa kuwaheshimu wazazi wawili yaani baba na mama, baada ya kutilia mkazo na kuzungumzia wajibu wa kumwabudu Mwenyezi Mungu Mmoja na kutii amri zake.

Malezi ya kidini ya watoto ni miongoni mwa mambo yenye umuhimu mkubwa katika saada na ufanisi wao na njia ya kumkinga mtoto na utovu wa maadili, uhalifu na ufuska. Wazazi wanaoshikamana na utekelezaji wa sheria za Mwenyezi Mungu, suala hilo huwa na taathira kubwa katika nafsi za watoto wao. Imam Mussa al Kadhim (as) ambaye ni miongoni mwa wajukuu watukufu wa Mtume wetu Muhammad (saw) anasema: Mwenendo wa watoto ni athari ya mwenendo wa wazazi wao.” Ni wazi kuwa baba ana nafasi na mchango mkubwa zaidi katika uwanja huu wa mwenendo wa watoto na mghafala wa aina yoyote wa baba katika suala hili yumkini ukawa na taathira mbaya katika mustakbali wa watoto. Iwapo wazazi wawili hususan baba wanashikamana barabara na mafundisho ya dini, watoto wao pia hufuata mwenendo huo; kwa sababu kwa kawaida watoto huiga na kufuata nyayo za wazazi wao.

Katika kipindi cha utotoni hakuna kitu bora zaidi kama mafunzo ya kivitendo. Baba anawajibika kuwafunza kivitendo watoto wake na kuwaonesha jinsi wanavyopasa kuwa. Kwa mfano tu baba analazimika kumfunza mtoto jinsi ya kutoa sadaka na kusabilia alicho nacho tangu kipindi cha utotoni mwake. Mafundisho ya Uislamu yanasisitiza kuwa, kama baba ana nia ya kutoa chochote kama fedha katika njia ya Mwenyezi Mungu basi bora ampe fedha au kitu hicho mtoto wake, na mtoto akabidhi fedha hizo kwa maskini au muhitaji. Hatua hii wapenzi wasikilizaji, humfunza mtoto na kumhimiza kuwasaidia wasiojiweza, kujitolea, kuwaonea huruma maskini, kushiriki katika masuala ya kijamii na kadhalika.

Ukweli ni kuwa utafiti uliofanywa na wataalamu umebaini kuwa, wazazi wawili wana taathira kubwa na za kubakia daima katika malezi ya watoto na kwamba sambamba na mama, watoto pia wana haja ya kuwa na kuishi na baba. Hivyo jitihada zozote za kutaka kufifiza nafasi na mchango wa baba katika malezi ya watoto, kama inavyoonekana leo katika harakati za mafeministi, zitakuwa na uharibifu mkubwa si kwa familia pekee bali jamii nzima ya mwanadamu.    >>>

          

                   

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)