Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 02 Februari 2016 12:15

Ufeministi, itikadi na misingi yake (18)

Ufeministi, itikadi na misingi yake (18)

Karibuni kuwa nasi tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki ambacho kinatupia jicho na kukosoa kwa muhtasari itikadi na misingi ya fikra za ufeministi.

Katika kipindi cha wiki iliyopita tulizungumzia juhudi za mafeministi za kudunisha nafasi na hadhi ya mama ya mwanamke. Tulisema kuwa mafeministi wanasisitiza kwamba, kuwa mama kwa mwanamke ni miongoni mwa sababu za dhulma na ukandamizaji wa wanawake na wanawataka wanaume pia wawe na nafasi kama ya mama ndani ya familia na jamii. Wito huu wa mafeministi umedhoofisha nafasi ya baba ndani ya familia. Leo tutajadili zaidi suala hili. <<<<< >>>>>>

Juhudi za mafemenisti zinajikita zaidi katika kupambanisha baina ya thamani za mwanamke na mwanaume. Tatizo la mafeministi ni kwamba, linapozungumziwa suala la haki za wanawake humchukulia mwanaume kuwa ndiyo kigezo na mizani ya ubinadamu na kwa msingi huo hupima utukufu na haki za mwanamke kwa mizani na vigezo vya kuwa mwanaume; na pale mwanamke anapokosa kuwa na vigezo hivyo vya kuwa mwanaume hutambuliwa kuwa ni kiumbe nakisi; hivyo wanasisitiza sana juu ya kupigania vigezo hivyo vya jinsi ya kiume. Suala hili, mpenzi msikilizaji, limechochea sana mpambano na ushindani baina ya mwanamke na mwanaume ndani ya familia na katika jamii. Kwa maneno mengine ni kuwa, limechochea mashindano makali baina ya jinsia hizo mbili juu ya nani ni mwanaume zaidi ya mwingine! Fikra za kifeministi kwa hakika zinataka kubaini zaidi kwamba ni yupi kati ya jinsia hizo mbili- mwanaume na mwanamke- mwenye thamani za kiume kuliko mwenzake, ni yupi anayeweza kufanya kazi na kuzalisha utajiri na mali zaidi na mwingine, yupi baina yao mwenye uwezo mkubwa zaidi wa kiuchumi na nani baina ya mwanaume na mwanamke mwenye nguvu kubwa zaidi ya mwingine katika medani ya vita na mapambano na nani baina yao mwenye hisia nyepesi za upole na huruma kuliko mwingine na kadhalika. Kwa mtazamo wa mafeministi, kila mmoja kati ya mwanaume na mwanamke anayekuwa na vigezo vingi zaidi kati ya hivyo vilivyotajwa hutambuliwa kuwa mwanadamu kamili zaidi. Kwa maneno mengine ni kuwa, kadiri mwanamke anapokuwa na sifa zaidi za kiume na kujishughulisha zaidi na masuala ya kiume ndivyo anavyokaribia ubinadamu zaidi, na pale anapokuwa na sifa zaidi za kike kama upendo hisia nyepesi, upole na huruma hutambuliwa kuwa mwanadamu nakisi na asiye kamili. Kwa msingi huo mwanamke katika fikra za kifeministi anahimizwa kujivua na hisi za kike na kufanya jitihada za kuwa na vigezo vya kiume.

Suala hili kama wanavyosisitiza wataalamu, limemuondoa mwanamke chini ya mwavuli wa himaya ya mwanaume na kumfanya mwanaume akose upendo, mahaba na huruma ya mwanamke. Matokeo ya hali hii ni kukosekana ile hali ya kukamilishana baina ya mwanamke na mwanaume na kuchochea zaidi ushindani baina ya wawili hawa. Jambo hili pia limemfanya mwanamke achukie uanauke wake wake na kukumbwa na hali ya mparaganyiko na matatizo ya kinafsi na kiroho inayosababisha mtikisiko katika familia na jamii. ........

Mpambano na ushindani huu umedhoofisha nafasi ya baba katika familia za Magharibi na kudunisha vigezo vya kijamii vya uanaume. Kwa msingi huo wataalamu wanasema miongoni mwa sababu za kudhoofishwa nafasi ya vijana wa kiume huko Magharibi na nafasi na mchango wa wanaume katika jamii ya Marekani ni kukosekana vigezo hivyo. Dakta Leonard Sax ambaye kitaaluma ni tabibu wa masuala ya familia nchini Marekani anasema: Baba wa sasa wa Kimarekani amebadilika na wala hatekelezi majukumu yake ipasavyo. Baba huyu hana taathira nzuri kwa watoto wake wa kiume na ni kwa msingi huo ndiyo maana vijana wa kiume wa Magharibi hawana taswira nzuri kuhusu jinsia ya kiume. Daktari Sax anaendelea kusema: Vijana wa kiume kawaida hutaka kupata vigezo vya kuiga lakini inasikitisha kuwa, wamekosa vigezo hivyo vya baba na mwanaume bora katika jamii za Magharibi."

Tabibu huyu ambaye pia ni mtaalamu wa elimu nafsi anasema: Aghlabu ya tamaduni zilizobakia hai kwa karne nyingi hujaza kipindi cha kuhama kutoka utotoni na kwenda utu uzima kwa mafunzo, adabu na desturi za kidini, lakini sisi Wamarekani wa karne ya 21 tunazicheka na kuzikebehi kwa kiburi ada na desturi hizo. Daktari huyo anasisitiza kuwa, kughafilika na kupuuzwa ada na desturi hizi za kipindi cha kuhama kutoka utotoni na kwenda kwenye utu uzima kimekuwa sababu ya kukosekana wanaume wenye ghera, huruma na wapole, kuwepo wanaume wavivu na wasiowajibika. <<<<< >>>>>

Ukweli ni kuwa mafeministi wanaghafilika kwamba miongoni mwa majukumu ya kimsingi ya wanaume ni kusimamia familia na wanawake. Ni wazi kuwa pale nafasi hiyo inapodhoofishwa, mhasirika mkuu huwa ni wanawake wenyewe ambao hulazimika kufanya kazi za sulubu na ngumu na kustahamili mashaka makubwa na hatimaye kukumbwa na matatizo ya kiroho na kimwili. Jambo hili la usimamizi wa wanaume kwa wanawake linasisitizwa katika aya ya 34 ya Suratul Nisaa ambayo inafungamanisha usimamizi huo wa wanaume kwa wanawake na majukumu yao ya kudhamini mahitaji ya kimaisha na kiuchumi ya wanawake.

Yumkini hapa likajitokeza swali kwamba, ni kwa nini wanaume wanapaswa kuwa wasimamizi wa wanawake? Ili kupata jibu sahihi la swali hili inatupasa kwanza kuchunguza kuwa je, usimamizi na umudiri na uendeshaji wa mwanaume masuala ya familia unaoana na kunasibiana na maumbile ya mwanaume na mwanamke au la?

Ni wazi kuwa, familia kama zilivyo taasisi nyingine zote katika jamii, inahitaji mudiri na msimamizi anayepaswa kuchukua maamuzi ya mwisho ya taasisi husika. Kuhusu taasisi ya familia kuna aina tatu za uendeshaji na usimamizi zinazoweza kutasawarika. Kwanza ni kuwa mwanaume na mwanamke wote wawili wawe mudiri na wasimamizi kwa kiwango sawa, pili mwanamke awe mudiri na msimamizi na tatu mwanaume awe msimamizi na mudiri wa familia. Kuhusu aina ya kwanza hapana shaka kuwa, ni vigumu au haiyumkini kuwapo wasimamizi wawili wenye mamlaka sawa, na kuwapo kwa mudiri na wasimamizi wa aina hii kwenye taasisi moja maana yake ni kutokuwapo usimamizi kabisa, tukiachia mbali mashaka na matatizo yanayoweza kujitokeza katika taasisi kama hiyo wakati wa kuchukua maamuzi, suala ambalo yumkini likapelekea kusambaratika familia.

Kuhusu dhana ya pili yaani mwanamke kuwa msimamizi na mudiri wa taasisi ya familia uchunguzi wote wa wataalamu umethibitisha kuwa, jambo hili halioani na maumbile na fitra ya mwanamke. Mtaalamu wa elimu nafsi wa Magharibi Bibi Marabel Morgan anasema: Japokuwa mwanaume na mwanamke wana hali sawa katika upande mmoja lakini wanatofautiana katika majukumu na nyadhifa zao. Mwenyezi Mungu amejaalia mwanaume awe rais na mwanamke awe naibu na makamu wake. Kila taasisi ina rais, mwenyekiti na mkurugenzi wake, vivyo hivyo taasisi ya familia katika jamii na hakuna njia ya kuweza kubadili utaratibu huu. Mtaalamu huyu wa elimu nafsi anasisitiza kuwa utaratibu wowote unaokwenda kinyume na huu hupelekea kusambaratika familia.

Mafeministi wanaeneza propaganda chafu kwamba, mwanamke kukubali usimamizi na umudiri wa mwanaume ni sawa na kuwa mtumwa wa mwanaume na wanawahimiza wanawake kupigania eti haki zao dhidi ya waume zao, jambo ambalo mara nyingi limekuwa sababu ya kuvunjika muungano mtakatifu wa ndoa. Ili kuondoa dhana hiyo potofu, Daktari Morgan anasisitiza kuwa: Maisha ya ndoa ni mithili ya utawala wa kifalme ambako mume huwa mfalme na mke huwa ni malkia. Katika ndoa za kifalme uamuzi wa mwisho huwa wa mfalme katika masuala ya malkia na taifa zima. Hata hivyo katika mfumo huu wa utawala malkia si mjakazi wa mfalme kwa sababu anajua vyema nafasi na mchango wake. Yeye huwa malkia wa mfalme na malkia wa taifa, kama ambavyo mke huwa malkiia wa mume wake na malkia wa familia nzima. Anaweza kuketi kwenye kiti cha mfalme na kueleza hisia zake zote. Anaendelea kusema kuwa: Japokuwa mfalme huwa anapata ilhamu na mashauri ya malkia lakini pale kunapotokea hitilafu za kimawazo, basi maamuzi ya mwisho huwa ya mfalme."

Katika mafundisho ya Uislamu tunakutana na hadithi ya Mtume Muhammad (saw) anayesema: Mwanaume ni sayidi na bwana wa familia yake, na mwanamke ni sayida na mkuu wa nyumba yake." Katika kugawa majukumu ndani ya familia, Mtume (saw) anasisitiza kuwa mwanaume huwa msimamizi na mudiri wa masuala ya familia, na mwanamke ni mudiri na msimamizi wa masuala ya nyumbani kwake kutokana na maumbile na hisia laini na nyepesi za kianakike, upendo, roho maridadi na moyo wa huruma ambavyo vyote vina mchango mkubwa katika furaha na saada ya familia nzima. Hata hivyo ieleweke kwamba, usimamizi na umudiri wa mwanaume katika familia hauna maana kwamba, mke hana haki ya kutoa maoni na mapendekezo yake, bali mudiri wa familia nzima pia, kama ilivyo katika taasisi nyingine, analazimika kutumia mitazamo na maoni ya watu wa chini yake na kushauriana nao kabla ya kuchukua maamuzi muhimu. Mwishowe mudiri na msimamizi huchukua maamuzi ya mwisho kwa kutilia maanani maslahi ya familia nzima na kwa kuchunga haki za wanachama wake wote. <<<<< >>>>.

Kipindi chetu juma hili kinaishia hapa. Tukutane wiki ijayo katika sehemu nyingine ya kipindi hiki panapo majaaliwa ya MwenyezI Mungu.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)