Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 26 Januari 2016 14:53

Ufeministi, itikadi na misingi yake (17)

Ufeministi, itikadi na misingi yake (17)

Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao huu wa Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu. Karibuni kuwa nasi tena katika mfululizo wa kipindi cha Ufeministi, itikadi na misingi yake. Katika kipindi cha wiki iliyopita tulizungumzia athari mbaya za kuavya mimba kwa roho na nafsi ya wanawake na vilevile tulifanya ulinganisho baina ya mtazamo wa Uislamu na ule wa ufeministi katika suala hilo. Tulisema kuwa katika mtazamo wa Uislamu kijusi na mtoto anayekuwa tumboni mwa mama yake ni mwanadamu kama wanadamu wengine baada ya kupuliziwa roho na kwamba ana haki ya kuishi na kuwa hai. Kwa sababu hiyo tulisisitiza kuwa, wazazi na madaktari wanaotoa mimba bila ya sababu za kisheria hutambuliwa kuwa ni wahalifu. Tulisisitiza kuwa katika mtazamo wa Uislamu mama anaruhusiwa kutoa mimba pale mimba hiyo inapokuwa hatari kwa maisha na uhai wake mwenyewe au sababu nyingine zinazotajwa katika vitabu vya fiqhi na sheria. Endeleeni kuwa nasi katika kipindi hiki ambapo leo tutajadili itikadi nyingine ya mafeministi ambayo ni kupuuza suala la kuzaa na kudunisha nafasi mwanamke kama mama.

Familia wapenzi wasikilizaji ndiyo msingi mkuu wa kila jamii. Katika uwanja huu mwanamke kama mama, anaweza kuwa nguzo muhimu, imara na salama ya familia na jamii kwa ujumla. Hata hivyo inasikitisha kuwa dunia ya sasa ya Magharibi imekumbwa na mkwamo kutokana na kupuuza na kudharau thamani ya kimaumbile ya kifitra ya mwanamke na mchango wake kama mama. Ukweli  ni kuwa hali ya sasa ya ulimwengu wa Magharibi itapelekea kusambaratika kabisa msingi wa familia katika siku za usoni kutokana na kudunisha nafasi na mchango wa mama kama mlezi wa kizazi na jamii.

Mafeministi wenye misimamo mikali wanadunisha na kudharau sana nafasi ya mwanamke kama mama na kuona thamani ya mwanamke kuwa ni kujihusisha na kuhudhuria tu katika masuala ya kijamii nje ya nyumba. Hii ni licha ya kwamba, Uislamu hauzioni shughuli za kijamii za mwanamke kuwa zinakinzana au kupingana na nafasi na mchango wake mkubwa kama mama. Kwa mfano tu Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei anasema: Uislamu umemtukuza ipasavyo mwanamke. Dini hiyo imetilia mkazo sana nafasi na mchango wa mama, heshima ya mama na hadhi ya mama ndani ya familia; vilevile imetilia mkazo nafasi ya mwanamke, taathira yake kubwa, haki zake na majukumu yake ndani ya familia lakini suala hili halina maana kwamba dini hiyo inamzuia mwanamke kushiriki katika masuala mengine ya kijamii, kufanya harakati za mapambano au shughuli nyingine za umma. Baadhi wameelewa na kufahamu visivyo suala hilo", mwisho wa kunukuu.

Baadhi ya mafeministi wanadai kuwa, nafasi na majukumu yaliyoainishwa kwa ajili ya mama ndani ya familia zinawadhoofisha na kuwadunisha wanawake. Mary Wollstonecraft ambaye alikuwa kinara wa mafeministi barani Ulaya amedai kuwa kubakishwa wanawake majumbani na kunyimwa uhuru na fursa za kijamii ndiyo sababu ya kudunishwa kwao na alikuwa akiamini kuwa, iwapo mipaka hiyo itaondolewa wanawake pia wataweza kufikiri na kufanya kazi za kimantiki kama wanaume. Hata hivyo Wollstonecraft na wenzake wanapuuza kabisa uhakika wa mambo, mahitaji na fitra na maumbile ya mwanamke. Hii ni pamoja na kuwa, kutekeleza kazi za mama si kikwazo au myororo unaomfunga mwanamke kufanya kazi zake nyingine za kijamii bali kinyume chake historia imeshuhudia kuwa watu adhimu na wakubwa wamelelewa na kukulia katika mikono ya akina mama welewa na waliojua na kutekeleza vyema majukumu yao ya mama. Daktari Jessica Anderson wa Marekani ameandika kuwa: Jukumu kuu la mwanamke ni kulea mtoto lakini utamaduni wa kimaada wa Magharibi umebadili uhakika huo na kulifanya jukumu na wadhifa asli wa mwanamke kuwa ni kufanya kazi nje ya nyumba na familia huku suala la kuwa mama likipewa umuhimu mdogo na duni. Daktari huyo anasema kuendelea hali hiyo kumezidisha mashinikizo ya kiroho na kinafsi kwa akina mama na wanawake katika nchi za Magharibi.

Mafeministi wenye misimamo mikali wanapiga vita sana nafasi ya mwanamke kama mama katika familia na jamii na wanasisitiza kuwa ndiyo msingi wa dhulma na ukandamizaji wa mwanamke. Mfeministi Shulamith Firestone anasema: Wadhifa wa kuwa mama mwanamke unapaswa kufutiliwa mbali katika utamaduni wa mwanadamu. Anasema kuwapa watoto maziwa kwa kutumia chupa na shule na vituo vya chekechekea vimefuta haja ya mama katika familia na jamii. Upinzani wa mafeministi dhidi ya nafasi ya mama umefikia kiasi cha mtaalamu wa masuala ya jamii wa Uingereza, Ann Oakley kusema: Njia ya kuwakomboa wanawake ni kufuta kabisa nafasi ya mwanamke kuwa mama na kuangamizwa kabisa taasisi ya familia!

Nafasi ya mama ina nafasi kubwa sana katika mtazamo wa Uislamu. Uislamu unatilia mkazo upande wa kiroho wa nafasi ya mama na kufanya jitihada za kuimarisha uzima wa kinafsi na kiroho wa kina mama. Kwa msingi huo dini hiyo inatambua kwamba umadhubuti na saada na ufanisi wa kila jamii ni rehani ya malezi bora ya familia ambayo msingi na nguzo yake kuu ni mama. Hii leo tunaona kuwa katika dunia ya leo ambapo kina mama wamejitenga na kuwa mbali na watoto kutokana na mihangaiko mingi ya kazi za nje ya nyumba, watoto na maua haya mazuri ya binadamu yamekosa nafasi mbadala wa mikono na kifua chenye upendo na vuguvugu na huruma na mahaba ya mama. Kwa kweli hakuna chekechea au kituo chochote duniani hata vile vilivyotengenezwa kwa teknolojia ya hali ya juu zaidi kinachoweza kujaza nafasi ya mama na kumpa mtoto upendo, mahaba na huruma yake.

Daktari Henry Makow ambaye ni mtaalamu wa masuala ya akina mama nchini Marekani anasema yafuatayo akieleza tofauti ya mwanamke Mwislamu na asiye Mwislamu wa Kimarekani na taathira za ufeministi kwa akina mama. Anasema: Kitu muhimu zaidi mwa mwanamke Mwislamu ni familia yake; familia kwake ni mithili ya tungu la vifaranga wa ndege alilolitengeneza yeye mwenyewe kwa ajili ya watoto wake na kuwalea yeye mwenyewe. Hujali tungu hilo la kuwa nguzo muhimu ya familia yake. Mwanamke Mwislamu huwa mithili ya nesi anayelea na kuchunga familia yake na kuwa kimbilio salama kwa mume na watoto wake. Dakta Henry Makow anaendelea kusema: Nchini Marekani thamani ya mwanamke hupimwa kutokana na mvuto wake wa kingono na matokeo ya vigezo kama hivyo ni kuwepo wanawake waliochanganyikiwa, wenye fadhaa, wanaosumbuliwa na matatizo ya kinafsi na wasiofaa kuwa mke au mama ndani ya familia.

Miongoni mwa wadhifa na kazi za kimsingi za nafasi ya mama ni kulea mtoto. Katika mfumo wa Uislamu, kulea mtoto ni kuhuisha fitra na maumbile asili ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya harakati ya kuelekea kwenye ukamilifu. Wasii wa Mtume wetu Muhammad (saw), Imam Ali bin Abi Twalib (as) anasema katika barua ya 31 ya Nahjul Balagha kwamba: Roho ya mtoto mdogo ni mithili ya ardhi ambayo haijalimwa inayokubali kila mbegu inayopandwa humo.

Tatizo la dunia ya leo ya Magharibi ni kwamba, kina mama wamejitenga sana na watoto na kazi za nyumba na familia. Familia nyingi za Magharibi zimesahau au kughafilika na ukweli kwamba, mtoto anahitaji himaya, upendo na mahaba ya wazazi wake kuliko hata masuala ya kimaada na anasa na viburudisho vingine. Imam Ruhullah Khomeini amenukuliwa akisema kuhusu nafasi adhimu ya mama katika familia na jamii kwamba: Utukufu wa mwanamke katika Uislamu ni mkubwa zaidi kuliko utukufu wa mwanaume. Wanawake hulea wanaume mashujaa na watajika sawa kabisa na inavyofanya Qur'ani Tukufu inayotengeneza wanadamu kamili.".

   

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)