Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 19 Januari 2016 12:13

Ufeministi, itikadi na misingi yake (16)

Ufeministi, itikadi na misingi yake (16)

Ni wakati mwingine umewadia wa kuwaleta sehemu nyingine ya makala ya Ufeministi Itikadi ya Misingi Yake. Katika kipindi cha wiki iliyopita tulizungumzia moja kati ya itikadi za mafeministi yaani kutoa na kuavya mimba na kusema kuwa, mafeministi wenye misimamo mikali wanasisitiza suala hilo kwa ajili eti ya kumkomboa mwanamke na kumuondolea majukumu ya kulea mtoto na kupata uhuru wa kibinafsi. Kwa maana kwamba kina mwanamke anaweza kutoa mimba yake wakati wowote ule anaopenda na kujiondoa katika minyororo ya mimba na kulea mtoto, huku wakighafilika kwamba jambo hilo ovu lina taathira nyingi mbaya hata kwa wanawake wenyewe. Kipindi hiki cha leo kitatupia jicho baadhi ya taathira mbaya za kutoa mimba na mtazamo wa Uislamu katika uwanja huo.

Kutoa mimba ni maradhi ya kimwili. Takwimu za taifa kuhusu kuavya mimba nchini Marekani zinaonesha kuwa, asilimia 10 ya wanawake wanaotoa mimba kwa matashi yao wenyewe wanasumbuliwa na matatizo mengi na kwamba asilimia 20 ya matatizo hayo ni makubwa zaidi kuliko mengine. Tamwimu hizo zinasema yumkini baadhi ya matatizo ya kuavya mimba yanaweza kutibiwa lakini kuna matatizo makuu yanayobakia kwa muda mrefu na yanayosababisha hatari ya kupatwa na ugumba. Uchunguzi uliofanyika katika uwanja huo pia umeonesha kuwa asilimia 3 hadi 5 ya wanawake wanaotoa mimba hupatwa na ugumba.

Wakati huo huo uchunguzi mwingi wa kisayansi umeonesha kuwa wanawake walioavya mimba wanakabiliwa zaidi na hali ya kupatwa na saratani ya matiti. Uchunguzi wa Taasisi ya Taifa ya Saratani nchini Marekani tarehe Pili Novemba mwaka `1994 ilitangaza kuwa asilimia 50 ya wanawake waliotoa mimba wanakabiliwa zaidi na hatari ya kupatwa na saratani ya matiti kuliko wanawake wengine. Wakati huo huo kutoa mimba huambatana na magonjwa ya akili. Matokeo ya uchunguzi uliofanyika kwa wanawake wiki kadhaa baada ya kutoa mimba unaonesha kuwa, asilimia 40 hadi 60 miongoni mwao walikuwa na mtazamo hasi na mbaya kuhusu utoaji mimba. Wanawake hao waliandamwa na hisi na nafsi inayowasuta kutenda dhambi kubwa, matatizo ya kinafsi, matatizo ya kupata usingizi na matatizo katika kuchukua maamuzi na kadhalika.

Vilevile uchunguzi uliofanywa na wataalamu unaonesha kuwa, migogoro ya kipindi cha baada ya kutoa mimba hushadidi zaidi kila inapowadia tarehe na siku ya kumbukumbu ya kitendo hicho au mapema zaidi. Uchunguzi wa washauri wa wanawake waliotoa mimba unaonesha kuwa, baadhi ya matatizo yanayowapata wanawake waliojihusisha na utoaji wa mimba ni pamoja na huzuni na msongo wa mawazo, kutojiamini, mienendo isiyo sahahi na ya uharibifu, matatizo ya usingizi, kupoteza kumbukumbu, majuto ya kudumu na kuandamwa na hisi ya kutenda dhambi, kuandamwa na hisi ya kufanya ukatili, kulia mara kwa mara, kukosa umakini na kuchukia watu na kazi za kabla ya kutoa mimba..

Katika mfumo wa dini tukufu ya Uislamu, kutoa mimba kunahesabiwa kuwa ni uhalifu na kosa kubwa na mwanadamu yeyote hana haki na kutoa mimba bila ya sababu za kitiba. Uislamu umeupa umuhimu mkubwa uhai wa kiumbe mwanadamu na unatambua uhai kuwa ni miongoni mwa haki za dhati za kiumbe huyo. Vilevile tunapaswa kutambua kuwa, hakuna mfumo wowote wa kifikra unaopinga haki hiyo ya uhai isipokuwa mfumo wa ufashisti unaosisitiza kuwa ukamilifu wa mwanadamu umo katika migongano, vita, unyonyaji na kuwatwisha watu wengine matakwa yako na kadhalika. Hata hivyo inatupasa kusisitiza hapa kuwa, baadhi ya Wamagharibi wenye fikra za kimaada wanatambua uhai wa kimaada tu kuwa ndio wenye umuhimu na kupuuza uhai wa kimaanawi na kiroho wa mwanadamu. Kwa msingi huo tunaona kuwa wasomi na wanafalsafa wakubwa wa zama hizi wanasisitiza kuwa, hatari kubwa zaidi inayotishia jamii na utamaduni wa ustaarabu wa Magharibi ni kutenganishwa uhai na maisha ya mwanadamu na masuala ya kimaanawi na kiroho.   

Ilani ya Haki za Binadamu ya Kiislamu iliyopasishwa na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) hapo mwaka 1990 inasisitiza katika kifungu nambari 17 kinachohusiana na kijusi na mimba kwamba: Kila mwanadamu ana haki ya kuishi katika mazingira safi yasiyokuwa na ufuska na maradhi ya kimaadili na kujijenga kiroho, na jamii na serikali zinawajibika kutayarisha mazingira mazuri ya kutumia haki hiyo."   >

Maudhui ya uhai yana umuhimu mkubwa sana katika mtazamo wa dini na mafundisho ya Uislamu yanasisitiza kuwa mwanadamu hana haki ya kumaliza uhai wa mwanadamu mwenzake bali pia hana hata haki na kudhuru na kumaliza uhai wake mwenyewe. Kwa msingi huo pale linapoulizwa swali kwamba je, katika mtazamo wa Uislamu mwanadamu anaweza kufumbia macho haki yake ya uhai?, tunakumbana na majibu ya aina mbili tofauti, moja ni lile la sheria za binadamu, na jingine la sheria za mbinguni na za Mwenyezi Mungu. Sheria za Magharibi, kwa kutegemea kwamba nafsi na uhai wa mwanadamu ni haki yake yeye mwenyewe, zinamruhusu mwanadamu kujiua na kujitoa uhai. Kwa msingi huu mafeministi na sheria za kimaada za Magharibi zinaruhusu wanawake kutoa mimba kwa kisingizio kwamba wana haki juu ya miili na uhai wao wenyewe. Kinyume chake, dini ya Uislamu inaharamisha na kukataza katakata suala la kuua na kutoa uhai hata na mwanadamu mwenyewe na inakitambua kitendo cha mwanadamu kujiua yeye mwenyewe kuwa ni kuua nafsi isiyo na hatia. Mafundisho ya Uislamu yanasisitiza kuwa uhai ni amana ya Mwenyezi Mungu kwa mwanadamu na kiumbe huyo anapaswa kulinda na kuchunga amana hiyo yenye thamani kubwa. Hivyo mwanadamu hana haki si ya kuua nafsi yake na wenzake tu bali pia anawajibika kulinda uhai wa kimwili na kiroho na pia uhai wa kiumbe kilichoko tumboni mwake ambacho pia ni amana ya Mwenyezi Mungu. Sehemu ya aya ya 195 ya Suratul Baqara katika Qur'ani Tukufu inasema: "Wala msijitie katika maangamizo kwa mikono yenu…" Si hayo tu bali hata pindi mwanadamu anapokuwa katika hali ngumu kupita kiasi na kupatwa na matatizo makubwa ya kinafsi na kimwili, Uislamu haumruhusu kujiua na kukomesha uhai wake au uhai wa kiumbe mwingine. Hii ni kutokana na ukweli kwamba katika dini hiyo mwanadamu -ikiwemo mimba iliyoko tumboni- ana utukufu wa aina yake kwa kadiri kwamba aya ya 32 ya Suratul Maida ya Qur'ani tukufu inasisitiza kuwa mtu anayetoa uhai wa mwanadamu mmoja huwa sawa na mtu aliyeua wanadamu wote, na mwenye kumuokoa mtu na (mauti) ni kama amewaokoa watu wote. Katika mtazamo wa dini huyo tukufu, kijusi na mtoto aliyeko tumboni mwa mama yake anapopewa roho huwa ni kiumbe na mwanadamu kama wengine na huwa na haki ya kuwa na uhai na kuishi. Kwa msingi huo wazazi na madaktari wanaoavya na kutoa mimba bila ya sababu ya kisheria hutambuliwa kuwa ni wahalifu na huchukuliwa hatua za kisheria.

Pamoja na hayo inatupasa kuelewa kuwa, katika mtazamo wa Uislamu mwanamke anaruhusiwa kutoa mimba wakati mimba hiyo inapokuwa hatari na tishio kwa uhai wake mwenyewe.    >>>>

Muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki umemalizika. Tukutane tena wiki ijayo katika sehemu nyingine panapo majaaliwa na Mwenyezi Mungu.          

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)