Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 19 Januari 2016 11:40

Ufeministi, itikadi na misingi yake (15)

Ufeministi, itikadi na misingi yake (15)

Katika kipindi cha wiki iliyopita tulijadili moja kati ya itikadi za ufeministi yaani uhuru usio na mipaka wa maingiliano ya kingono. Tulisema kuwa kuenea kwa fikra hii ya ufeministi kulitayarisha mazingira ya Magharibi kubadili maadili ya masuala ya kujamiiana kwa daraja 180. Tulisema kuwa miongoni mwa matokeo ya kuenea fikra hii katika nchi za Magharibi ni kukithiri zinaa na mahusiano haramu ya ngono, matatizo mengi ya kimaadili kama kuavya na kutoa mimba, kuzaliwa idadi kubwa ya wanaharamu, kuongezeka familia zenye mzazi mmoja (mama na mtoto au watoto), kukithiti maradhi ya kuambukiza, kuzagaa vitendo vya kujamiiana watu wenye jinsia moja, uhakaba na kusambaratika misingi ya familia.

Kipindi chetu leo kitatupia jicho moja ya athari mbaya za fikra ya uhuru usio na mpaka wa maingiliano ya kingono ya fikra za ufeministi yaani suala ya kutoa mimba. 

Kuenea kwa fikra za ufeministi katika zama hizi imekuwa sababu ya kujitokeza matatizo mengi na utovu wa maadili kama suala la kuavya na kutoa mimba. Suala hili limesababisha matatizo mengi katika jamii za Magharibi na nchi zinazofuata fikra za kifeministi. Ili eti kumkomboa mwanamke na majukumu ya kulea mtoto na kupata uhuru wa mtu binafsi, mafeministi wenye misimamo mikali wamekuwa wakipendekeza na kuhubiri suala la kutoa mimba. Kwa maana kwamba kila mwanamke anaweza kutoa mimba wakati wowote anaopenda na kujivua eti na mzigo na minyororo ya kulea na majukumu ya kutunza watoto.

Suala la kutoa mimba kwa maana hii ya mafeministi si sawa na kutoa mimba kutokana na ushauri wa daktari ambako mama mwenye mimba hushauriwa kutoa mimba kwa sababu za kiafya, usalama na maisha ya mama na kadhalika ambapo mwanamke mwenye mimba hushauriwa kutoa mimba kwa ajili ya kulinda uhai wake. Kwa hakika kuua kiumbe aliye tumboni mwa mama bila ya sababu yoyote ya kimantiki na kitiba huumiza roho ya kila mwanadamu mwenye hisi ya utu na hukumbusha kipindi cha ujahilia cha kabla ya Uislamu ambapo Waarabu na watu wa kaumu nyingine walikuwa wakiwazika watoto wao wakiwa hai.

Katika zama hizi jamii ya Magharibi imepiga hatua kubwa za maendeleo katika baadhi ya mambo ya kimaada lakini kutokana na kutekwa na mitazamo ya kifeministi na kimaada imesahau kabisa au kutupilia mbali masuala ya kimaadili na kiroho. Mwandishi George Grant wa Marekani anaandika kwamba: Vyombo vya habari vya nchi za Magharibi vimeshindwa vibaya katika medani ya maadili na havichukui jukumu la kuwajulisha watu na umma kwamba mambo machafu na maovu tuliyokuwa tukiyanasibisha na kuyahusisha na madaktari wa Hitler hii leo yanafanywa kila siku na madaktari na watafiti wakubwa katika mahospitali ya Marekani dhidi ya watoto wachanga", mwisho wa kunukuu.

Suala la kuavya mimba na juhudi za baadhi ya jamii za Magharibi za kutetea jambo hilo linalojadiliwa chini ya anwani ya kuvutia na ya kuhadaa watu ya mafeministi ya eti 'haki miliki ya mwanamke juu ya mwili wake', lina mizizi katika utovu wa maadili katika jamii ya sasa yenye uhuru usio na mpaka katika maingiliano ya kingono kwenye nchi za Magharibi. Kutoa mimba ni jambo lisilo la kibinadamu na linalopingana na maumbile safi ya mwanadamu na mbinu zake mbalimbali zinaakisi kukanyagwa kwa misingi ya maadili. Vitendo hivyo viovu vinaongezeka sana katika nchi kama Marekani, Uingereza na Canada. Utafiti uliofanywa na wataalamu wawili wa Uingereza kwa majina ya Michael Litchfield na Susan Kentish unaonesha kuwa kila mwaka maelfu ya vijusi (mtoto aliyetumboni mwa mama) walioavya na wanawake huchomwa katika matanuri nchini Uingereza. Wataalamu hawa wawili ambao walitembelea hospitali na kliniki kadhaa nchini Uingereza kwa ajili ya kutoa mimba, wameandika kumbukumbu zao katika kitabu walichokipa jina la Babies for Burning (Watoto kwa Ajili ya Kuchomwa). Kitabu hicho ambacho kiliitumbukiza Uingereza katika kashfa kubwa kilikasirikiwa na kupigwa vita haraka na vyombo vya habari, suala ambalo si la kushangaza katika nchi za Magharibi zinazotawaliwa na fikra za ufeministi.

Mbinu zinazotumiwa katika kutoa mimba katika jamii za magharibi pia zinafungamana sana na biashara ya mabepari wa kisasa. Kwa sasa kuna watu huko magharibi ambao wako tayari wanaua vijusi na watoto walioko matumboni mwa mama zao kwa malengo ya kibiashara na kupata faida ili vijusi hivyo vitumiwe katika maabara na masuala mengine ya uhakiki.

Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba hii leo madaktari wa Ulaya wanatumia vijusi na mimba zilizoavywa kwa ajili ya kutengeneza vipodozi na kupata faida za kibiashara. Katika mojawapo ya matamshi ya kuchukiza na kutikisa nyoyo, Profesa Chris Bagley ambaye ni mhadhiri na daktari anayetetea suala la kutoa mimba anasema: Mafuta ya kijusi yanahitajiwa sana katika utengenezaji wa vipodozi. Daktari huyo asiye na utu anaendelea kusema kwamba amekuwa akitoa mimba pevu na kwamba maadamu vijusi hivyo vinaweza kutumiwa kwa ajili ya biashara ni aibu kuvitupa katika matanuri ya moto. Anasema amekuwa akitoa mimba za wanawake hata zile zilizokamilisha miezi saba….

Daktari huyu katili anakiri waziwazi kuwa amekuwa akiua wanadamu wasio na hatia ambao kosa lao pekee ni umbile lao dogo bila ya kuchukuliwa hatua yoyote.

Takwimu zinaonesha kuwa utoaji wa mimba unaongezeka sana katika nchi mbalimbali. Inaripotiwa kuwa nchini Marekani mimba milioni 1.6 hutolewa na wanawake kila mwaka. Ili kuthibisha kuavya mimba na kuua mwanadamu asiye na hatia, mtaalamu mmoja wa Marekani aliunganisha chombo cha kuchukua picha ndani ya mwili wa mama mmoja ambaye alikuwa akitoa mimba yenye umri wa wiki 12 kisha akatayarisha filamu aliyoipa jina la 'Kilio cha Kimyakimya. Filamu hiyo inasikitisha sana na inaonesha kijusi na kitoto hicho tumboni kikijaribu kukimbia huku na kule bila ya matumaini mbele ya chombo kilichokuwa kikivuta na kukatakata maungo yake kimoja baada ya kingine na kukitoa nje ya tumbo la mama.

Canada ni miongoni mwa nchi ambazo mabunge yao yamepasisha na kuruhusu uhuru wa kutoa mimba licha ya upinzani mkubwa wa wananchi wengi. Takwimu zinaonesha kwamba, kila siku zaidi ya mimba 270 hutolewa katika mahospitali na kliniki makhsusi nchini Canada na asilimia 25 ya mimba hizo hutolewa na wasichana vijana. Mwanahistoria Profesa Ian Gentles wa Canada anaandika kuhusu haki za watoto nchini humo akisema: Watoto ambao hawajazaliwa wana haki ya kurithi nchini humo na wanaweza kumshtaki mtu mwingine wakiwa tumboni mwa mama zake. Lakini haki pekee ambayo watoto hao hawapewi ni haki ya kuishi na kutouliwa. Hii ni kwa sababu serikali inampa mama haki ya kuua mtoto wake. Msomi huyo anaendelea kuandika kuwa: Katika hospitali za Canada vijusi na watoto waliotolewa hupelekwa katika maabara ya patholojia na kisha hutumwa kwenye matanuri ya moto kwa ajili ya kuchomwa. Mimba hizo nyingi huwa zinatolewa na kuavya kwa mbinu na njia za kuhuzunisha sana. Mwandishi Gadner anasema kuhusu mbinu za kuavya mimba nchini Canada kwamba: Suala la kutoa mimba linaonesha taswira ndogo ya vita vikubwa zaidi vya ndani dhidi ya maadili na thamani za kibinadamu katika nchi za Magharibi.

Makala yetu kwa leo inaishia hapa, tukutane tena wiki ijayo katika sehemu nyingine ya kipindi hiki.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)