Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 10 Januari 2016 20:28

Ufeministi, itikadi na misingi yake (14)

Ufeministi, itikadi na misingi yake (14)

 Karibuni kuwa nasi tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachojadili na kukosoa itikadi za ufeministi. Katika kipindi cha wiki iliyopita tulizungumzia fikra ya mafeministi inayodai kuwa watoto wanazuia maendeleo ya shughuli za kijamii na kazi za wanawake na kwa msingi huo wameamua kuziachia chekechea kazi ya kulea na kutunza watoto. Tuliashiria pia madhara yanayosababishwa na itikadi hiyo. Leo tutazungumzia itikadi nyingine ya ufeministi ambayo ni ya uhuru wa maingiliano ya kingono.        >>

Ulimwengu wa leo umekumbwa na mporomoko wa kimaadili kutokana na kuwa mbali na dini na mafundisho ya Mwenyezi Mungu. Mwenendo wa sasa wa kueneza ufisadi na ufuska umesababisha matatizo mengi katika nchi za Magharibi. Kwa mfano tu mafeministi wenye misimamo mikali wanasisitiza kuwa, mipaka ya mahusiano ya kingono na kujamiiana kati ya mwanamke na mwanaume ni miongoni mwa minyororo inayomfunga mwanamke na wanawahamasisha wanawake kujikomboa na kujitoa kwenye minyororo hiyo. Mwanafikra Shahid Murtadha Mutahhari anasema: Mjadala mkuu unaotawala Magharibi katika zama hizi ni kutukuza na kuheshimu matakwa ya maingiliano ya kingono na udharura wa maingiliano hayo kuwa huru na kuondolewa mipaka yote katika uwanja huo. Anasema, ustaarabu wa sasa katika nchi za Magharibi hususan Marekani ni kujielekeza zaidi kwenye masuala ya ngono na kutupilia mbali kigezo cha maadili.

Jarida la Newsweek mwaka 1967 liliandika yafuatayo kuhusu mabadiliko yaliyokuwa yakitokea katika nchi za Magharibi katika uwanja huo: Miiko ya kale imo katika hali ya kufa na kunajitokeza jamii mpya zinazohalalisha ufuska na maingiliano huru ya kingono…

Mwandishi wa kitabu “Magharibi Inaumwa” anasema katika sehemu moja ya kitabu hicho kwamba: Jarida moja la Marekani limeeleza sababu tatu za kishetani zinazochochea moto baina ya wananchi ambazo ni kwanza: Fasihi mbaya na chafu iliyotokea baada ya vita na kuenea kwa kasi baina ya watu. Pili ni filamu zinazochochea hisi za ngono na matamanio ya nafsi, na tatu ni kuporomoka kwa maadili baina ya wanawake ambako kunadhihiri katika mavazi yao na hata katika kutembea uchi na kuingiliana ovyo na bila mpaka na wanaume”, mwisho wa kunukuu.

Kuna takwimu zinazotia wasiwasi mkubwa kuhusu suala hili la uhuru wa maingiliano ya kingono na mgogoro wa kijamii katika nchi za Magharibi vinavyotokana na mitazamo ya kifeministi. Hata hivyo inatupasa kusema kuwa, kwa ujumla zinaa na maingiliano haramu baina ya wanawake na wanaume na mwenendo wa kuanzisha familia bila ya kufunga ndoa na kuenea kwa mambo hayo vina mfungamano wa moja kwa moja na itikadi za kifeministi. Hata hivyo kadhia hii haiishii hapo, kwani wataalamu wa masuala ya jamii wanasema, matokeo ya mitazamo hiyo ya kifeministi ni pamoja na kukithiri zinaa, kutoa na kuavya mimba, kukithiri familia zenye mzazi mmoja, yaani mama na mtoto tu, magonjwa ya kuambukiza, ngono baina ya watu wenye jinsia moja, ukahaba, kuporomoka kwa taasisi ya familia, kuporomoka maadili na kadhalika.    >

Tumesema kuwa kuporomoka kwa maadili kumeifanya taasisi ya familia ikabiliwe na mgogoro mkubwa katika nchi za Magharibi. La kushangaza zaidi ni kuwa, roho ya ufuska na kukiuka maadili sasa inatawala mikataba na maazimio mengi ya jumuiya za kimataifa ikiweno ile ya kupambana na ubaguzi dhidi ya wanawake. Kwa kuwa msingi wa kifikra unaotawala maazimio mengi ya taasisi hiyo unatokana na itikadi za asili ya ladha na anasa za dunia, hivyo basi maadili na akhlaki vimetupiliwa mbali, na kunafanyika jitihada za kuanzisha jamii isiyotilia maanani maadili na misingi ya tabia na mwenendo mwema. Maazimio hayo yanajali na kuzipa umuhimu tu ladha na matamanio ya kinafsi ya wanawake.

Kwa mfano tu ukahaba na kazi ya wanawake kuuza miili yao kumetajwa katika kifungu cha sita cha makubaliano ya kufuta ubaguzi dhidi ya wanawake. Kamati ya makubaliano hayo inafasiri kipengee hicho ikisema, kina maana ya kuruhusu rasmi kazi ya ukahaba na wanawake kuuza miili yao. Mwaka 2000 kamati hiyo ilizishinikiza nchi kama Russia, Mexico, Romania, Ufilipino na Peru kuidhinisha rasmi kazi ya ukahaba na kuwalinda makahaba.

Suala la kwanza linalopewa mazingatio na mafeministi ni kadhia ya uhuru na maingiliano huru ya kingono. Kwa maneno mengine ni kuwa, mafeministi wanaeneza uhuru wa maingiliano ya ngono kwa kisingizio cha uhuru wa mwanamke na mwanaume.

Dini tukufu ya Uislamu imepinga vikali uhuru usio na mpaka na inasisitiza kuwa, uhuru wa aina hiyo unatoa pigo kubwa kwa taasisi ya familia na kutishia maslahi ya jamii. Ni wazi kuwa familia husambaratika pale mwanamke na mwanaume wanapokosa kutekeleza majukumu na ahadi zao kwa kila mmoja wao. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amasema: Iwapo wanadamu wangeachwa hivi hivi kushibisha matamanio yao ya ngono bila ya kuwekewa mipaka, basi familia zisingeundwa au zingekuwa zikisambaratika kwa sababu ndogo. Kwa msingi huo kila mahala panaposhuhudiwa uhuru wa mahusiano ya kujamiiana, hushuhudiwa pia kudhoofika kwa misingi ya taasisi ya familia", mwisho wa kunukuu.

Makundi yanayohubiri maadili ya kisasa katika masuala ya ngono yanategemea msingi wa uhuru wa mtu binafsi yakisisitiza kuwa, unapaswa kulindwa na kuheshimiwa. Hata hivyo yamesahau au kujisahaulisha kwamba, mshale mkubwa zaidi uliolenga maadili ulitumwa kwa jina la uhuru. Akhlaki na maadili yana umuhimu mkubwa sana kiasi kwamba Mtume Muhammad (saw) amesema: "Nimetumwa kuja kutimiza maadili mema."

Miongoni mwa taathira za maadili ni kuratibu mahusiano ya kujamiiana baina ya wanadamu. Mwanahistoria wa Magharibi Will Durant anasema: Miongoni mwa kazi muhimu za maadili ni kuratibu mahusiano ya ngono kwa sababu matamanio hayo husababisha matatizo mengi si wakati wa ndoa tu bali kabla na baada yake na matokeo ya kushadidi na kuchupa kwake mipaka na kutoka katika njia ya kimaumbile ni utovu wa nidhamu na machafuko katika taasisi za kijamii.."

Uislamu mpenzi msikilizaji umeheshimu sana taasisi ya familia na unasisitiza kujiepusha na uhuru usio na mipaka katika uwanja huo kwa ajili ya kulinda misingi ya taasisi hiyo tukufu. Kwa msingi huo matatizo na migogoro inayohusiana na maingiliano ya kujamiiana inatokea kwa kiwango kidogo katika jamii za Kiislamu na pale inapotokea basi sababu yake huwa ni kutoheshimiwa na kutoshikamana na sheria na maadili ya Kiislamu. Uislamu unasisitiza sana kwamba, mazingira ya familia yanapaswa kuwahusu mke na mume pekee na jamii inapaswa kuwa mahala pa kazi na shughuli za kila siku za kimaisha na kuwekwa mbali na ufuska na uchupaji wa mipaka ya maadili ili vipawa vya watu vipate fursa ya kuchanua na jamii ipate uzima wa kimaadili na kiroho.                    >>

       

  

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)