Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Alkhamisi, 31 Disemba 2015 15:33

Ufeministi, itikadi na misingi yake (13)

Ufeministi, itikadi na misingi yake (13)

Ni wakati mwingine wa kuwaletea  sehemu nyingine ya kipindi cha Ufeministi, Itikadi na Misingi Yake. Katika kipindi kilichopita tulizungumzia taathira za ufeministi kwa familia. Tulisema miongoni mwa taathira za ufeministi ni kuongezeka familia zenye mzazi mmoja. Vilevile miongoni mwa taathira za fikra za ufeministi ni wanawake kujizuia kuzaa, suala ambalo linaongezeka sana katika nchi za Magharibi. Sababu za swala hilo ni pamoja na eti kupata elimu ya juu, kufanya kazi na kufikia malengo ya kiajira, ubinafsi, kupenda anasa na kadhalika. Katika upande mwingine mafeministi wanawatambua watoto kuwa ni kizuizi cha maendeleo na shughuli za kijamii na kufanya kazi wanawake, kwa msingi huo wanawake wengi wanazitupia chechechea baadhi ya majukumu yao ya kulea watoto. Kipindi chetu leo kitatupia jicho taathira za ongezeko la chekechea zinazochukua nafasi ya mama katika jamii. >

Mchango wa wazazi wawili hususan mama katika maisha na malezi ya watoto ni muhimu na mkubwa sana. Mazingira ya familia yanafananishwa na ardhi yenye rutuba ya kijani kibichi, na watoto wa familia ni mithili ya maua yenye rangi za kuvutia na kupendeza. Baadhi ya wanafikra wanasema, saada na ufanisi wa watoto au upotofu na kukosa mafanikio kwa watoto kunafungamana zaidi na familia na mbinu za malezi. Ni wazi kuwa, mama ana mchango mkubwa zaidi katika suala hili.

Mama ana nafasi muhimu sana katika malezi ya watoto katika pande mbili. Kwanza ni kwamba, mtoto hupitisha miaka muhimu zaidi ya kujenga shakhsia yake katika mikono yenye upendo na mahaba ya mama. Kipindi na miaka hii ndiyo msingi wa malezi ya awali ya mtoto ambaye huiga na kufuata ada na sifa za kimwenendo za mama. Pili ni kwamba, mama kutokana na hisi zake na upendo na ikhasi huwa kimbilio salama kwa mtoto na wakati wowote mtoto anapohisi ukosefu wa amani hutafuta upendo na mahaba ya mama mzazi. Mtaalamu wa elimu nafsi wa Uingereza, Balby John anasema: Mtoto huhitaji kuwepo mama pamoja naye sawa kabisa na anavyohitajia chakula."

Katika harakati zao za kuwa na nafasi sawa na ya wanaume, hii leo mafeministi wanafanya mikakati ya kuzidhihirisha chekechea na vituo vya kutunza watoto kuwa ni mbadala wa nafasi ya mama katika familia na jamii. Mafeministi wengi wanaamini kwamba, ni kazi isiyokuwa ya kiungwana mwanamke kutumia wakati wake akiwa pamoja na watoto na kwamba njia ya ufumbuzi ni kuwapeleka kwenye chekechea na vituo vya kulea watoto. Kwa msingi huo kumeanzishwa chekechea na vituo vya kulea watoto bure katika nchi za Magharibi suala linaloonesha kuwepo ratiba na mpango maalumu wa kubadili nafasi ya mama na familia. Mwandishi William Gardner ameandika katika kitabu cha Vita dhidi ya Familia kwamba: "Suala la chekechea ni miongoni mwa nyenzo za mafeministi wenye misimamo mikali katika vita vyao dhidi ya familia."

Wataalamu wengi wa masuala ya malezi wanaamini kuwa, chekechea na vutuo vya kulea waototo vita taathira nyingi mbaya katika fikra na nafasi ya mtoto. Miongoni mwa taathira hizo ni kuvuruga hisi ya kujiamini na kuzidisha ukatili. Mwandishi Belsky Barglow anasema, watoto wanaopelekwa chekechea, hususan wanapokuwa katika maeneo hayo kwa zaidi ya masaa 20 kwa wiki, hulitambua suala hilo kuwa ni sawa na kufukuzwa na wazazi wao. Mhadhiri Jay Belsky wa Cho Kikuu cha Pennsylvania huko Marekani anaamini kuwa: Chekechea zinazowatunza watoto kwa kipindi kirefu kama masaa 20 kwa wiki ni hatari kubwa kwa watoto, familia na jamii. Anasema uchunguzi umebaini kwamba, nafasi za juu za vitendo vya ukatili, kukatiza masomo, watu waliotiwa nguvuni na kuswekwa jela, watu wasio na ajira, walevi, wasio na makazi aghlabu zinashikwa na watu ambao utotoni mwao hawakupata upendo na mahaba ya wazazi wawili.   >

Suala la kutozingatiwa nafasi na mchango wa mama katika malezi ya watoto limezitumbukiza jamii za Magharibi katika mgogoro mkubwa. Mtaalamu wa masuala ya jamii wa Marekani, Davis Kingsley anasema: Inaonekana kwamba miongoni mwa ajenda kuu za mfumo wa elimu katika nchi za Magharibi ni kuwafanya watoto wawaone wazazi wao kuwa ni watu ajnabi. Mama katika nchi za Magharibi, anaendelea kusema Kingsley, hutumia wakati wake mwingi akiwa nje ya nyumba na kazini na kumwacha mtoto wake kwenye vituo vya kutunza watoto na chekechea. Baada ya kurudi nyumbani, mama hushindwa kutekeleza ipasavyo majukumu yake ya kimama kutokana na uchovu.

Dakta Elliot Baker wa matatizo ya kinafsi ambaye amekuwa akishughulikia watu wenye matatizo ya ukatili na wauaji kwa kipindi cha zaidi ya miongo miwili anasema watu wengi wanaowaona wazazi wanaokwenda kuwatembelea watoto wao waliohusika na ukatili na mauaji huuliza: Wazazi hawa walikuwa wapi wakati watoto wao walipokuwa wakiwahitajia? Daktari huyo anasema, wagonjwa wake wengi walikumbwa na hali hiyo kutokana na kuachwa au kutengana na mama zao muda mfupi baada ya kuzaliwa na kuwa chini ya usimamizi na malezi na watu wengine.."

Matokeo ya kudhamini hali bora katika nchi za Magharibi ni kutayarisha nafasi sawa kupitia njia ya kupokea ushuru wa kulazimisha kutoka kwa wananchi. Ushuru na kodi hizo huwa nzito na kubwa kiasi kwamba familia za kawaida yaani mke na mume, hulazimika kufanya kazi na kuwapeleka watoto wao katika chekechea za umma ili kuzimudu. Hii ni pamoja na kuwa, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Wizara ya Afya na Masuala ya Jamii ya Canada, thuluthi mbili ya Wacanada wanaamini kuwa, nyumbani na kandokando ya wazazi ndiyo mahali bora zaidi kwa ajili ya watoto kabla ya kuanza shule za misingi.

Pamoja na hayo yote na licha ya mafemenisti kutilia mkazo suala la kupelekwa watoto kwenye chekechea na vituo vya kulea watoto, wanawake wengi wameonesha kuwa wanapendelea kubakia nyumbani wakiwa pamoja na watoto ndani ya familia. Hali hii imedhihiri katika uchunguzi uliofanyika huko Marekani. Uchunguzi uliofanywa na Los Angeles Times na kuwashangaza mafemenisti umeonesha kuwa, asilimia 79 ya wanawake wa Marekani wanaofanya kazi wakiwa na watoto wanasema iwapo wangeweza kumudu matatizo ya kifedha basi wangekhitari kubakia nyumbani na kushughulikia watoto wao. Uchunguzi kama huo pia ulifanyika nchini Canada na asilimia 69 ya wanawake ilikhitari kubakia nyumbani na kulea watoto badala ya kwenda kazini kama hali ingeruhusu.

Suala la malezi sahihi ya watoto limepewa umuhimu mkubwa sana katika dini ya Uislamu na wazazi wawili hususan mama wamepewa nafasi kubwa katika suala hilo. Mikono yenye upendo, hisi zilizojaa mahaba na moyo wenye huruma wa wazazi wawili hususan mama huwa kinga kubwa ya matatizo mengi ya kinafsi na kiroho. Hadithi zilizopokewa kutoka kwa Mtume (saw) na Ahlubaiti zake watoharifu zinasisitiza kuwa miongoni mwa haki za mtoto kwa wazazi wawili ni kumpa malezi mema, jina zuri na kumfundisha Qur'ani na Swala. Kiongozi Muadhamu wa mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Khamenei pia anasisitiza kuwa: Familia ndiyo eneo ambako hisi za upendo na mahaba zinapopaswa kustawishwa na watoto kuona na kuhisi hali hiyo….     >

Msikose kufuatilia mfululizo wa kipindi hiki wiki ijayo.         

       

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)