Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 26 Disemba 2015 17:54

Ufeministi, itikadi na misingi yake (12)

Ufeministi, itikadi na misingi yake (12)

Ni wakati mwingine wa kuwa nanyi wafuatiliaji wa  kipindi hiki kinachojadili na kukosoa misingi ya ufeministi. Kipindi chetu leo kitazungumzia taathira za mitazamo ya ufeministi katika taasisi ya familia. Ni matarajio yangu kuwa mtaendelea kuwa kando ya redio zenu kusikiliza tuliyokuandalieni…..

Katika kipindi cha wiki iliyopita tulisema kuwa, miongoni mwa matokeo ya itikadi za kifeministi ni kupungua kwa ndoa na kuunda familia na vilevile kueneza hisi na uadui na makabiliano ya kudumu baina ya wanawake na wanaume. Katika upande mwingine kuenezwa kwa itikadi hizo za kifeministi kumekuwa sababu ya kufanyika mabadiliko katika taasisi ya familia, jambo ambalo limesababisha migogoro chungu nzima na matatizo mengi katika jamii za kisasa. Ushahidi unaonesha kuwa, kujitokeza kwa aina mbalimbali za familia hususan ongezeko la familia zenye mzazi mmoja na familia zisizo na mtoto kumeifanya taasisi ya familia ikumbwe na matatizo mengi.

Familia, ni taasisi ndogo lakini muhimu sana ya kijamii. Katika karne za kabla ya kuanza zama za viwanda, familia ilikuwa taasisi ya kijamii na kiuchumi inayojitosheleza ambayo kwa kawaida iliundwa na vizazi kadhaa. Katika majmui hiyo babu na bibi walikuwa wakiishi pamoja na watoto na wajukuu zao na kufanya jitihada za kulinda na kubakisha kizazi na familia nzima. Mwanzoni mwa karne 19 waume walianza kutambuliwa kuwa wakimu familia. Hata hivyo hatua kwa hatua na katika kipindi chote cha karne ya 19 ada za kijamii zinazohusiana na familia zilikumbwa na mabadiliko. Mabadiliko hayo yalisababisha mageuzi makubwa na ya kimsingi katika muundo wa familia huko Magharibi hususan Marekani katika miongo ya 60 na 70. Harakati kama zile za ufeministi ambazo zilikuwa zikifanya mikakati eti ya kuwakomboa wanawake, zilianza kuwahamasisha kufanya kazi nje ya nyumba na tangu wakati huo chekechea zilichukua nafasi ya mama na baba katika kulea watoto. Mtaalamu wa masuala ya familia wa Marekani, David H. Olson, anasema kuhusu kadhia hiyo kwamba: Kiwango kikubwa zaidi cha talaka kilitokea baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Katika mazingira hayo mapya ya baada ya vita, wanawake wengi waliingia katika soko la kazi. Baada ya masaa ya kazi na kurejea nyumbani waume zao, uhusiano wa kindoa baina ya wawili hao ulianza kukumbwa na mtetemeko. Katika mazingira hayo wanawake wengi waliomba talaka zao kwa shabaha ya kwenda kutafuta eti mwanaume bora zaidi", mwisho wa kunukuu.

Katika mchakato huo kulifanyika harakati nyingi na kubwa dhidi ya ada na kiutamaduni wa kijadi. Kwa mfano tu fikra ya uhuru wa maingiliano ya kingono ilizusha aina nyingine ya uhusiano wa maingiliano hayo, na moja ya matokeo yake ilikuwa kuishi pamoja mwanamke na mwanaume bila ya kufunga ndoa.

Tangu zama za kale, familia imekuwa ikiundwa na mwanamke na mwanaume ambao baada ya kuoana rasmi hupata watoto na kizazi. Hata hivyo baada ya mapinduzi ya viwanda katika nchi za Magharibi na baada ya kuanza harakati ya mafeministi na kudunishwa kwa ndoa na taasisi ya familia, kulijitokeza wapinzani wapya wa ndoa ambao hawakufanana hata kidogo na ndoa ya kiasili na kijadi. Wakati huo kulijitokeza familia za ajabu mithili ya familia zenye mzazi mmoja na maisha ya kindoa baina ya watu wawili wenye jinsia moja.   >

Familia zenye mzazi mmoja zilianza kuenea zaidi katika nchi za Magharibi kwenye muongo wa 1960. Katika familia hizo mtoto au watoto huishi na mmoja wa wazazi wawili na aghalabu ya wakati huwa wanaishi na mama.

Takwimu za nchi za Ulaya zinaonesha kuwa, zaidi ya asilimia 50 ya jamii ya nchi hizo katika kipindi cha miongo ya mwishoni mwa karne ya 20 ilikuwa ikiishi katika familia zenye mzazi mmoja. Wahakiki wa masuala ya kijamii wamesema katika ujumbe wa UNESCO kwamba sababu ya kujitokeza na kushamiri familia zenye mzazi mmoja ni kupungua ndoa rasmi, maisha ya mwanamke na mwanaume bila ya kuoana, ubinafsi uliopindukia, kupenda anasa, kukithiri kwa talaka na kadhalika. Inatupasa pia kusema kwamba, familia nyingi zenye mzazi mmoja zinaundwa na mama na mtoto aliyezaliwa kutokana na mahusiano na maingiliano haramu. Gazeti la Newsweek limeripoti kuwa, asilimia 57 ya wanaharamu wazungu nchini Marekani wanaishi na mama zao katika familia ya mzazi mmoja. Linaendelea kuandika kuwa, kwa sasa wasichana wengi katika jamii za nchi za Magharibi wamejiunga na familia za mzazi mmoja kutokana na kupata uja uzito kupitia zinaa na mahusinao haramu.

Wataalamu wa masuala ya jamii wanasema kuwa, sababu ya wimbi kubwa la watu wa Magharibi kujielekeza kwenye aina hii ya maisha ya pamoja baina ya mwanamke na mwanaume bila ya kufunga ndoa rasmi ni ufuska ulioenea katika mahusiano ya wanawake na wanaume. Jarida la Reader's Digest la Marekani limeandika kuwa: Masikitiko na majuto, kukosa makazi, jinai na usaliti, kusambaratika kwa familia na kushindwa kuwa na tathmini sahihi kuhusu mustakbali ni miongoni mwa matokeo ya mahusiano huru ya kingono katika jamii ya Marekani."

Kwa utaratibu huo tunaona kuwa, aghlabu ya familia zenye mzazi mmoja katika nchi za Magharibi ni matokeo ya uhusiano haramu na ufuska. Wakati huo huo wataalamu wa masuala ya jamii wanasema mwenendo huu umekuwa na taathira nyingi mbaya za kimalezi, kiuchumi, kiafya na kadhalika kwa familia na watoto wanaozaliwa katika familia hizo bali hata kwa jamii nzima kwa ujumla. Ili kuweza kuondoa au kwa uchache kupunguza athari hizo mbaya wataalamu wa masuala ya malezi na jamii kama Adam Bursua wa jimbo la Illinois nchini Marekani wanasema kuna udharura wa kuimarishwa familia za kijadi zinazoendelea kuwepo wakati wote wa uhai wa mtoto. Mtaalamu huyo anasema: Baba au mama hapaswi kubeba majukumu ya kulea mtoto peke yake na ili kuweza kutatua mgogoro wa familia ya mzazi mmoja kuna ulazima wa kupiga marufuku mwenendo wa kujifungua wanawake nje ya sheria na ndoa rasmi.

Katika mtazamo wa Uislamu familia imepewa umuhimu mkubwa na taasisi hiyo imetambuliwa kuwa ni mahala salama zaidi pa kukidhi mahitaji ya kiroho na kinafsi ya mwanaume na mwanamke, kudumisha kizazi cha mwanadamu, kulea watoto na kadhalika mambo ambayo hayapatikani katika familia zingine. Himaya ya kinafsi ya mume kwa mkewe na mke kwa mumewe  inayotokana na kujenga mahusiano salama na yenye utulivu huwa dhamana ya kuimarisha familia na kulinda uzima wa kifikra na kinafsi wa mtu binafsi na jamii. Malezi ya kijamii ya watoto pia ambayo hupatikana chini ya kivuli cha mahusiano yenye upendo, mahaba na utulivu wa kiroho wa wazazi wawili ni njia muhimu zaidi ya kupatikana dhamana hiyo. Hivyo basi ili kuzuia ongezeko la familia za mzazi mmoja kuna udharura wa kudumishwa familia za kijadi, nafasi ya wazazi wawili katika taasisi ya familia na vilevile kuimarishwa itikadi za kidini vitu ambavyo kwa pamoja vina taathira kubwa katika kulinda na kuimarisha taasisi ya familia. >

             

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)