Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 19 Disemba 2015 21:16

Ufeministi, itikadi na misingi yake (11)

Ufeministi, itikadi na misingi yake (11)

Katika kipindi cha wiki iliyopita tulisema kuwa, itikadi za ufeministi zina madhara na uharibifu mkubwa na miongoni mwa matokeo yake ni kupinga suala la kuanzisha familia na kudhoofisha taasisi hiyo. Tulisema kinyume na itikadi za ufeministi, Uislamu unaitambua ndoa na kujenga familia kuwa ni jibu la mahitaji ya kimaumbile na kwamba miongoni mwa matunda na matokeo ya kuunda familia ni utulivu, usalama wa kinafsi na kuzidisha na kulinda kizazi cha mwanadamu. Leo katika kipindi hiki, tutajadili moja kati ya matokeo ya itikadi za mafeministi yaani kueneza hisi za uhasama na mgongano wa kudumu baina ya wanawake na wanaume.

Miongoni mwa misingi mikuu ya fikra za kifeministi ni upinzani wa daima wa mafeministi dhidi ya wanaume. Hii ni kwa sababu, mafeministi wanawaona wanaume na wanawake kuwa ni viumbe kinzani na wasio sawa na wenye maslahi yanayopingana. Mafeministi wanawatambua wanaume kuwa ni maadui wakubwa na wahusika asili wa kudunishwa wanawake na kwamba, wamepeta hadhi na nafasi yao ya kijamii kupitia njia ya kuwanyonya wanawake ndani ya taasisi ya familia. Hivyo wanasema ili kujiondoa katika udhibiti wa wanaume kuna udharura wa kuwa mbali na kujiepusha nao. Mafeministi wenye misimamo mikali wamefikia kiwango cha kupendekeza suala la wanawake kwenda kuishi mbali na katika kisiwa kisicho na mwanaume hata mmoja!

Stratijia hii ya mafeministi haikukubaliwa na wafuasi wengi wa pote hilo kutokana na kutokuwa na uwezo wa kutatua matatizo ya wanawake na kugongana na kupingana kwake na malengo mengine ya kundi hilo.

Itikadi hii inayosisitiza kuwa wanawake na wanaume ni viumbe wawili wanaopingana na daima wanapaswa kupambana na kupigana, imeyafanya maisha kuwa baridi, yenye mivutano ya mara kwa mara na yasiyokuwa na utulivu kwa mwanamke na mwamaume katika jamii za Magharibi. Mitazamo hii imekuwa na taathira mbaya zaidi kwa wanawake wenyewe. Mwandishi Dakta Toni Grant wa Magharibi anasema katika kitabu alichokipa jina la “Being a Woman” kwamba: Mwanamke wa zama hizi ni mwanaume bandia anayepigana vita na wanaume halisi, na kwa sababu hiyo amechanganyikiwa na kukosa utulivu.. “

Katika upande mwingine itikadi ya kuwepo mpambano na vita vya kudumu baina ya jinsia mbili za kike na kiume imekuwa na taathira na matokeo mabaya kwa wanaume. Toni Grant anasema katika kitabu tulichoashiria hapo awali cha Being a Woman kwamba: Kufuatia harakati hii ya ufeministi, wanaume wengi wamepoteza moyo wa kujiamini na kuhisi kwamba ili kuweza kulinda maisha yao wanapaswa kupambana na kukabiliana na wanawake. Katika hali ya kujihami, wanaume hao wameamua kulipiza kisasi na kukabiliana na wanawake aghlabu kwa kiburi na ujuba, kana kwamba wanataka kusema: Sisi ndio wanaume halisi na kama nyinyi ni wanaume kweli basi thibitisheni uanaume wenu”, mwisho wa kunukuu.

Misimamo hiyo mikali ya mafeministi ya kuwapambanisha wanaume na wanawake imewafanya watu wengi waelewe kuwa, jinsia hizo mbili haziwezi kuishi katika hali ya kupambana, kupingana na kupigana vita. Allen R. Klein ambaye ni mhadhiri wa masuala ya utafiti wa wanawake nchini Marekani ameandika katika kitabu alichokipa jina la “Uchi wa Ufeministi” akisema: Madai yaliyotiwa chumvi kuhusu dhulma ya mwanaume na mwenendo usio wa kiadilifu wa mafeministi dhidi ya wanaume yote yamesaidia kuzidisha chuki na kuondoa imani ya mwanamke kijana kuhusu ufeministi. Vilevile mwandishi Christina Hoff Sommers wa Marekani anasema katika kitabu alichokipa jina la “How Women Have Betrayed Women” kwamba: Mimi ninaamini kwamba ipo siku aidiolojia ya mafeministi itapoteza soko na mafeministi wengi watavua miwani ya jinsia na kutazama ukweli wa mambo ya kijamii kama ulivyo. Sidai kuwa hayo yatatokea hivi karibuni, lakini nina uhakika kwamba hapana shaka yatatokea”, mwisho wa kunukuu.  <

Mafeministi wametokomeza na kuangamiza kabisa sifa za mwanamke kwa kutaka kuwapachika wanawake sifa za wanaume. Ni wazi kuwa, katika mivutano ya kugombea nguvu na mamlaka makubwa zaidi uhusiano wa mwanamke na mwanaume hupatwa na madhara na suala hili lina maana na kifo cha penzi na mahaba kati ya jinsia hizo mbili. Wataalamu wa elimu nafsi wanasisitiza kuwa wanawake wanatofautiana na wanaume na kwamba sifa za kila jinsia kati ya makundi hayo mawili yaani sifa ya kuwa mwanaume ya mwanaume na ya kuwa mwanamke ya wanawake, zinapaswa kulindwa. Hii ni kwa sababu si mwanamke anayeweza kuficha sifa zake za kike na wala wanaume hawawezi kulinda uwezo wao kama wanaume baada ya kupoteza shakhsia zao za kiume. Si hayo tu, bali wanasaikolojia wanasema, hata wanawake wenyewe hawaridhishwi na suala la kutoa changamoto kwa wanaume. Kimsingi kumtazama mwanamke kama mwanaume kuna maana ya kushusha chini hadhi ya wanawake na kuwaondoa katika nafasi yao ya juu ya kibinadamu. Vilevile tunapaswa kutambua kwamba, kutaka kumfananisha mwanamke na mwanaume ni kukiri kwa njia moja au nyingine kwamba, mwanaume ni bora zaidi, na suala hili halioani na mtazamo wa mafeministi wa kuwadhalilisha na kuwadunisha wanaume wala halioani na nafasi na hadhi ya mwanamke. Mitazamo hii ya mafeministi ya kutaka kuwatambua na kuwafananisha wanawake na wanaume huwafanya wanawake wajione kuwa ni wageni na watu wanaoishi katika nafsi zisizokuwa zao, na hali hii ya kuwa katika barzakhi ya kuishi kama mwanamke-mwanaume inamtumbukiza mwanamke katika mgogoro wa mpasuko wa shakhsia yake.

Katika mtazamo wa Uislamu, kila mmoja kati ya mwanamke na mwanaume ameainishiwa taklifu na majukumu kulingana na sifa zake za kimaumbile. Katika mtazamo wa Uislamu mwanaume na mwanamke wanahitajiana kwa ajili ya kuunda familia na kuondoa nakisi na mapungufu ya kila upande kwa ajili ya kuelekea kwenye ukamilifu. Kwa mfano tu, miongoni mwa athari na matokeo ya kuoana mwanamke na mwanaume ni kushibisha ghariza na matamanio ya aina mbalimbali kama haja ya kupenda na kupendwa, matamanio ya kujamiiana, kudhamini usalama na utulivu wa kiroho na kinafsi na kadhalika. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 21 ya Suratur Rum kwamba: Miongoni mwa ishara zake ni kuwaumbia wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao na akajaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya zimo ishara kwa wenye kutafakari.

Hivyo basi katika Uislamu kila mmoja kati ya mwanamke na mwanaume ana nafasi yake maalumu, na tofauti na sifa makhsusi za kila mmoja wao hazipasi kuwa sababu ya kukabiliana na kuhitilafiana. Vilevile mafundisho ya dini hiyo yamewausia wanandoa, yaani mke na mume kushirikiana, na kusaidiana na kuwa na mwenendo wa upendo na mahaba baina yao. Mtume Muhammad (amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Aali zake amesema: Wakati mwanaume anapomtazama mkewe kwa mahaba, na mke akamuangalia mumewe kwa jicho na upendo, Mwenyezi Mungu huwaangalia wote wawili kwa jicho la rehma yake.

  

 

 

   

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)