Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 08 Disemba 2015 14:04

Ufeministi, Itikadi na misingi yake (10)

Ufeministi, Itikadi na misingi yake (10)

Ni wakati mwingine wa kuwaletea sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachojadili na kukosoa itikadi na misingi ya Ufeministi. Katika kipindi kilichopita tulijadili mitazamo ya mafemenisti wanaopinga suala la kuwa mama na kulea watoto kama wadhifa muhimu na wa asili wa mwanamke. Tulisema kuwa misimamo hiyo ilipelekea kudhoofishwa nguzo za familia katika nchi za Magharibi. Tulisisitiza kuwa katika mtazamo wa Uislamu kazi na wadhifa asili wa mwanamke ni kutunza nyumba na kulea watoto wema ambao ndio kizazi cha kesho cha mwanadamu na kwamba wanawake wanaweza sambamba na wadhifa huo wa asili- kujishughulisha na kazi nyingine za kijamii zisizopingana au kugongana na wadhifa wao wa asili. Kipindi chetu leo kitatupia jicho na kukosoa itikadi nyingine ya mafeministi ya kupinga ndoa.

Miongoni mwa masuala yanayojadiliwa na mafeministi ni upinzani wao dhidi ya ndoa na kujenga familia. Mafeministi wanaiona ndoa, kuzaa na kulea watoto kuwa ni udhalilishaji wa mwanamke kwa sababu – kwa mtazamo wao- mambo hayo ndiyo msingi na nguzo za dhulma na ukandamizaji wa mwanamke. Kwa msingi huo mafeministi wenye misimamo mikali wanatilia mkazo udharura wa kufanyika mapinduzi katika masuala hayo na matokeo ya fikra kama hiyo ni kukomeshwa kabisa ndoa na kutoweka maana ya mwanamke kuwa mama.

Mwandishi mfeministi wa Ufaransa, Simone De Beauvoir anasema kuhusu maudhui hii kwamba: “Mambo mawili yanambakisha mwanamke katika minyororo ya utumwa nayo ni taasisi ya ndoa na suala la kuwa mama.” Mwandishi huyu anashambulia vikali mfumo wa familia kama nguzo ya maisha ya kijamii na kulea watoto salama na kuitambua kuwa ndiyo sababu ya kile anachokiita masaibu ya wanawake. Vilevile anautaja upinzani dhidi ya masuala ya kuzaa na kuanzisha familia kwa kuolewa wanawake kama ilivyo hivi sasa kuwa ni miongoni mwa mambo muhimu sana ya harakati ya ufeministi.

Mafeministi wengi wana uhasama mkubwa dhidi ya familia inayojengwa kupitia ndoa na wanataka kufanyike mapinduzi ya kidemokrasia ya wanawake ndani ya familia. Wanaamini kwamba, wanawake hawapasi kupewa uhuru wa kushiriki katika kuanzisha au katika kudumisha taasisi ya familia kwa mtindo wa sasa. Baadhi ya vinara wa mafeministi kama ((Sherhight)) wanafurahishwa sana na suala na kuwepo idadi kubwa ya familia zisizo na baba na watoto wengi wanaharamu katika jamii ya Marekani wakisema kuwa, malezi kama hayo ya wavulana wasio na baba yaani wanaharamu, yatapelekea kubadilika mienendo yao kuhusu wanawake.

Kwa mtazamo wa mafeministi, familia si jambo tukufu wala mtindo bora wa maisha ya pamoja bali ni udhalilishaji kwa mwanamke. Kwa msingi huo sehemu kubwa ya mafeministi inaundwa na mashoga kwa maana ya watu wanaoingiliana kinyume na maumbile. Uhasama na uadui wa mafeministi dhidi ya familia ulikuwa sababu na kufutwa neno “familia” katika taarifa za mkutano wa Beijing na badala yake kulitumiwa neno household.

Hapana shaka kuwa matokeo ya vita vya mafeministi dhidi ya mwanaume ni kupambana na familia na ada na taratibu zake za miaka mingi. >

Miongoni mwa matokeo machungu ya kuenea fikra za mafeministi wenye misimamo mikali ni watu kukimbia na kukwepa suala la kujenga na kuanzisha familia katika dunia ya leo. Kwa sasa familia za kijadi ziko katika ncha ya kutoweka kabisa. Uchunguzi mwingi wa masuala ya kijamii unaonesha kuwa, mtazamo wa Wamagharibi kwa ndoa kama njia ya maisha ya pamoja baina ya mwanamke na mwanaume umepungua na kufifia na kumeanzishwa aina mpya za maisha ya jinsia hizo mbili, suala ambalo limeibua matatizo mengi ya kijamii. Hata hivyo ukweli ni kwamba, ndoa ni miongoni mwa vigezo muhimu sana vya familia au kusambaratika kwa familia katika kila jamii kutokana na sababu za kihistoria na udhibiti wa masuala ya jamii.      >

Uislamu kama dini kamili ya Mwenyezi Mungu imelipa umuhimu mkubwa suala la kufunga ndoa na kulitambua kuwa ni thamani (value) aali, kwa kadiri kwamba kwa mujibu wa mafundisho ya dini hiyo, mtu anayefunga ndoa na kuanzisha familia huwa amekamilisha nusu ya dini yake. Katika mtazamo wa Uislamu mwanadamu anapaswa kuoa au kuolewa ili aweze kuwa na maisha ya utulivu na kupiga hatua za kuelekea kwenye ukamilifu. Mwenyezi Mungu mtukufu anasema katika aya ya 21 ya Suratu Rum kwamba: “Na katika Ishara Zake ni kuwaumbia wake (wenzi wenu) kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao na akajaalia mapenzi na huruma baina yenu, hakika katika haya kuna ishara kwa watu wanaotafakari.” Haja kubwa zaidi inayodhaminiwa na kukidhiwa kutokana na kufunga ndoa ni haja ya utulivu na amani ya kinafsi. Hivyo basi, ili mwanadamu aweze kukidhi haja hii ya kuwa na usalama na utulivu wa kinafsi katika mtazamo wa Uislamu na vilevile kushibisha mahitaji yake ya kimaumbile hana budi kuoa na kuanzisha familia. La sivyo ghariza na hisi hiyo ya kimaumbile yenye nguvu kubwa itadhihiri na kujitokeza katika sura nyingine yenye hatari na madhara makubwa kama inavyoshuhudiwa sasa katika jamii zilizopuuza bali hata kupinga ndoa baina ya jinsia mbili tofauti.

Ni wazi kuwa ndoa ni njia ya kumkamilisha mwanamke na mwanaume. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, hakuna mwanadamu mkamilifu –isipokuwa mawalii na Mitume wa Mwenyezi Mungu-, na wanadamu daima huwa katika harakati za kufidia nakisi na mapungufu yao. Vijana hufanya juhudi za kupata uhuru na kujitegemea kifikra na kupunguza nakisi na kukidhi mahitaji yao mengi kwa kujielekeza kwenye ndoa; na hutayarisha mazingira mazuri zaidi ya kufikia ukamilifu kwa kuchagua mwenza na mwanandoa anayefaa.

Katika upande mwingine miongoni mwa matunda makubwa ya kufunga ndoa na kuanzisha familia ni kupata watoto na kubakisha hai kizazi cha mwanadamu. Suala hili la kuzaa na kudumisha kizazi cha mwanadamu halipaswi kupuuzwa hata kidogo. Kuzaa na kulea kizazi chema, safi na stahiki cha mwanadamu ni takwa la agizo la Mwenyezi Mungu Muumba. Mafundisho ya Uislamu yanasisitiza kwamba, kuwa na mtoto mwema ni amali na tendo jema kwa baba na mama na huwa na taathira kubwa katika saada na ufanisi wa dunia na Akhera wa wazazi wawili.

Kwa utaratibu huu mfuatiliaji wa kipindi, inabainika wazi kuwa, misimamo ya mafeministi ya kupinga ndoa na kuanzisha familia inawazuia wanadamu kukidhi mahitaji yao ya kimaumbile na kupata usalama na utulivu wa kinafsi na kijamii. Vilevile mitazamo hiyo inakwaza na kukwamisha harakati ya jamii ya kuwa na kizazi salama na chema.     >

Kipindi chetu kinaishia hapa kwa leo. Usikose kuwa nasi wiki ijayo katika sehemu nyingine panapo majaaliwa na Mwenyezi Mungu.      

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)