Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 08 Disemba 2015 13:59

Ufeministi, itikadi na misingi yake (9)

Ufeministi, itikadi na misingi yake (9)

Karibuni kuwa nasi tena katika sehemu nyingine ya makala ya Ufeministi, Itikadi na Misingi Yake. Katika kipindi kilichopita tulizungumzia baadhi ya misingi ya Ufenimisti kama usekulari na kujitenga na mafundisho ya dini na kusema kuwa hii leo mfumo wa familia umekumbwa na mgogoro mkubwa wa masuala ya kiroho na maadili katika nchi za Magharibi kutokana  na kuwa mbali na dini na masuala ya kiroho. Kipindi chetu leo kitakosoa mtazamo wa mafeministi wa kulipa kipaumbele cha kwanza na uasili suala la kufanya kazi mwanamke nje ya nyumba na kupinga wadhifa wa mwanamke kama mama na mama wa nyumbani na taathira zake. 

Miongoni mwa misingi ya kifikra ya ufeministi ni kuwahamasisha na kuwalazimisha wanawake na wasichana kufanyakazi nje ya nyumba. Mafeministi wanaamini kuwa kubakia mwanamke nyumbani na kutofanya kazi nje ya maskani na makazi na nyumbani kwake ndiyo sababu kuu ya dhulma za kisiasa, kijamii na kuchumi zinazowapata wanawake. Kwa msingi hiyo dhulma hiyo itakomeshwa tu pale kwanza wasichana kupitia njia ya malezi ya ndani ya familia na kisha malezi rasmi mashuleni watakapohamasishwa na kutayarishwa kufanya kazi nje ya nyumba kama wenzao wanaume. Wanasema iwapo wasichana watatayarishiwa uwanja mzuri wa kushiriki katika masuala ya kisiasa, kijamii na kiuchumi wataweza. Sawa kabisa na wenzao wanaume, kujishughulisha na masuala hayo. Kwa hakika tunaweza kusema kuwa, dhana ya kwanza ya kuwakomboa wanawake katika itikadi za mafeministi ni kuwaingiza watu wa jinsia hiyo katika soko la kazi na viwanda na katika awamu ya pili kuyafanya masuala ya kufanya kazi na malezi ya watoto nje ya nyumba kuwa suala la kijamii.

Fikra ya kupinga suala la mama kufanya kazi za nyumbani na wadhifa wake kama mama ni miongoni mwa misingi na nguzo kuu za ufeministi. Mafeministi wanafanya jitihada za kupunguza nafasi ya mama ya wanawake na kudhihirisha suala la mama kufanya kazi ndani ya familia yake kuwa ni kudunishwa. Katika uwanja huo mafeministi wanasisitiza katika kampeni zao kwamba kuwa mama au kujishughulisha na kazi za mama na kulea mtoto si chaguo zuri kwa wasichana. Wanasema maadamu mwanamke anajihusisha na masuala hayo mawili itakuwa muhali kumkomboa kutoka kwenye udhibiti wa mwanaume. Kwa msingi huo baadhi ya watafiti wanasisitiza kuwa lengo la mafeministi ni kuanzisha vita dhidi ya familia.

Mafeministi wanaamini kuwa, kazi za mama nyumbani hazina thamani yoyote maadamu hazina kipato cha fedha licha ya kwamba zinatayarisha mazingira salama na ya utulivu kwa familia yake. Mwandishi Ann Oukly wa Magharibi anakumbusha maneno ya Lenin aliyesema: Madamu nusu ya jamii ya mwanadamu inashikiliwa mateka jikoni, hakuna taifa linaloweza kuwa huru, kisha anapendekeza misingi mitatu kwamba nafasi ya mama wa nyumbani inapaswa kufutwa, familia inapaswa kufutwa na hatimaye nafasi zinazohusiana na jinsia pia zinapaswa kutupiliwa mbali na kufutwa. Kwa fikra kama hizo mafeministi wanapendekeza kuundwa jumuiya na taasisi za kijamii ambazo zitachukua nafasi ya familia na mama. Uhasama na uadui wa mafeministi dhidi ya familia umefikia kiwango cha baadhi yao kutaja kazi ya mwanamke kuwa mama kuwa ni adhabu kwa jinsia hiyo!

Tulisema kuwa mafeministi wote wanakutambua kuolewa, kuwa mama na kuwa mke kuwa vinatokana na mfumo dume na kwamba ni nyenzo za kuendelea kumshikilia mateka na kumfunga mwanamke. Kwa msingi huo katika mtazamo wa mafeministi, wanawake wote wanapaswa kuondoka majumbani na kuingia katika soko la kazi. Mwandishi wa kitabu cha ‘Jinsia ya Pili’ (The Second Sex) mwenye misimamo mikali ya kifeministi wa Magharibi, Simone de Beauvoir anasema: Mwanamke yeyote hapasi kuruhusiwa kubakia nyumbani na kujishughulisha na malezi ya watoto wake. Jamii inapaswa kubadilika kabisa na isiwaruhusu wanawake kulea watoto tu."

Betty Friedan ambaye ni feministi mashuhuri wa kiliberali wa Marekani katika kitabu cha The Feminine Mystique anaeleza chuki yake kubwa dhidi ya nafasi yamwanamke nyumbani na kusema katika maneno ya upotoshaji mkubwa kwamba, kina mama wa nyumbani ni mithili ya wahanga wa kambi za mateka, bali hali yao ni mbaya zaidi. Friedan anawahamasisha wanawake kujikomboa kutoka kwenye tundu ya nyumba zao za familia na kusisitiza kuwa nyumbani si mahala mwafaka kwa wanawake. Inasikitisha kuona kwamba mafeministi wanawalazimisha wanawake kuondoka mahala ambako kwa itikadi za watu wengi ni fursa kubwa zaidi na isiyo na kifani kwa ajili ya kulea na kumstawisha mwanadamu.

Pamoja na hayo mpenzi msikilizaji sisi sote tunajua kwamba, mwanadamu hawezi kuficha ukweli wa kupambana na fitra na maumbile yake asili katika kipindi kirefu. Ukweli huu pia ulisadiki na kutimia kwa mafeministi na wanawake wengi; na hata wanaharakai wa ufeministi hawakuweza kukabiliana na kupigana na hakika ya ndani ya nafsi zao kwa kuwa wao wenyewe pia walikuwa wake na mama watoto. Kwa msingi huo mafeministi wengi katika kipindi cha muda mrefu walifanya jitihada za kutubu na kurekebisha matamshi na mitazamo yao isiyo sahihi. Kwa mfano tu, Betty Friedan miaka kadhaa baada ya kitabu chake cha kwanza cha The Feminine Mystique alilegeza misimamo yake ya awali na kuandika kitabu cha The Second Stage kwamba wanawake wanaweza kuambatanisha kazi za nje na zile za nyumbani na zile za nje na kuziweza zote. Katika kitabu hicho Friedan anaeleza wasiwasi wake kuhusu mustakbali wa wanawake waliotanguliza mbele mafanikio ya kikazi kuliko kuunda na kuanzisha familia na sasa wamechanganyikiwa na kukosa matumaini. Wanawake watalakiwa wasiokuwa na nafasi nzuri kikazi na wanasumbuliwa na ufukara, kina mama wasio na waume wanaokabiliwa na mustakbali mgumu, wanawake ambao kufanya kazi nje ya nyumba limekuwa jambo la dharura na lazima kwao na wakati huo huo wanalazimika kutekeleza majukumu yake ya mke na mama, yote haya yamewatia wasiwasi magwiji wa fikra za kifeministi.

Ukweli ni kuwa kuwachochea wanawake kufanya kazi nzito na ngumu nje ya nyumba na kupuuza nafasi yao asili vimekuwa na matokeo mabaya kwa wanawake wenyewe, familia na jamii kwa ujumla. Mwandishi Nancy Lee demos wa huko huko Magharibi anasema: Kuwachochea wanawake wachukie kazi za nyumbani na kuwaburuta katika kazi za nje kwa ajili ya kuridhisha matakwa na nafsi zao hakukuwa na natija isipokuwa kuwazidishia mashunikizo na msongo wa mawazo na wengi miongoni mwao hawawezi tena kuishi bila ya msaada wa wataalamu na kutumia dawa. Wanawake hao ambao wamekuwa wakihama kutoka huku na kwenda kule kufanya kazi za aina mbalimbali zaidi wametumbukia katika mahusiano haramu ya ngono na kadhalika.

Daktari mtaalamu wa wanawake Jessica Anderson anasema: Kazi ni sehemu ya maisha na wadhifa mkuu na wa asili wa mwanamke ni kulea mtoto, lakini utamaduni wa kimaada wa Magharibi umelifanya suala la kufanya kazi nje ya nyumba kuwa ndiyo asili na msingi, na kazi ya mama ya kulea watoto na familia kuwa ni jambo la pembeni na lisilo la msingi. Daktari huyo anasema: Kuendelea kwa mwenendo huo kunazidisha mashinikizo ya kiroho na kinafsi kwa wanawake na akina mama katika jamii za Magharibi."

Uislamu umetambua rasmi haki ya wanawake ya kufanya kazi sambamba na kutilia maanani maumbile na shakhsia yao. Aya ya 32 ya Suratu Nisaa inasema: Wanaume wana fungu katika waliyoyachuma na wanawake wana fungu katika waliyoyachuma,.." Wafasiri na wanazuoni wa Kiislamu wanasema ayah ii inajuzisha kufanya kazi kwa wanawake. Vilevile suna na sira ya Mtume (saw) na Ahlubaiti zake watoharifu inaonesha kuwa wanawake wanaweza kujishughulisha na baadhi ya kazi ambazo zinaendana na roho zao nyepesi. Hata hivyo sheria za dini ya Uislamu zinasisitiza kuwa, kazi za wanawake zinapaswa pia kutilia maanani malashi na msingi wa familia. Pamoja na hayo katika mtazamo wa Uislamu nafasi kuu na ya asili ya mwanamke ni kulea mtoto na anaweza kufanya kazi nyingine za kijamii kando ya kazi na wadhifa wake wa asili. Katika uwanja huo Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei anasema: Uislamu umeafiki mwanamke kufanya kazi na si tu kwamba umeafiki suala hilo bali pia unaiona kazi kuwa ni jambo muhimu na la dharura maadamu haogongani na kazi na wadhifa wake mkuu yaani kulea mtoto na kulinda familia. Anasisitiza kuwa hakuna nchi isiyohitaji nguvu kazi ya wanawake katika nyanja mbalimbali lakini kazi hizo zinapaswa kuoana na utukufu na thamani za kiroho na kibinadamu za mwanamke..".

Tukutane tena wiki ijayo panapo majaaliwa yake Mwenyezi Mungu.

 

          

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)