Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 22 Novemba 2015 17:07

Ufeministi, itikadi na misingi yake (7)

Ufeministi, itikadi na misingi yake (7)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi tena katika sehemu nyingine ya kipindi cha Ufeministi, Itikadi na Misingi yake. Katika kipindi cha wiki iliyopita tulisema kuwa tofauti na mtazamo wa fikra za kifeministi, katika mtazamo wa Uislamu mwanamke na mwanaume wanatofautiana si kimwili pekee, bali hata katika nyanja mbalimbali za kinafsi, kihisia, kimawazo na kimwenendo. Tulisema  tofauti hizo ndiyo sababu ya kutokea mfumo wa kutumikiana kwa jinsia zote mbili, kukidhi mahitaji ya pande zote mbili, familia na jamii na sababu ya kumsukuma mwanaume kwa mwanamke na mwanamke kwa mwanaume na hatimaye sababu ya kukamilishana wawili hao, kuziba na kukidhi nakisi na mapungufu ya pande mbili na kujitokeza taasisi ya familia. Tulisema kuwa katika fikra za Kiislamu, mbali na kuthamini na kuenzi nafasi na majukumu ya kijamii ya mwanamke, vilevile kunatiliwa mkazo nafasi makhsusi ya mwanamke na mwanaume katika taasisi ya familia. Katika dini hiyo kila mmoja kati ya mwanamke na mwanaume ana mchango na nafasi mbili zinazokamilishana ndani ya familia na katika jamii, na majukumu hayo ya pamoja na makhsusi yanapaswa kulindwa katika kila hali kwa mujibu wa vigezo na mipaka ya kidini. Kipindi chetu cha leo kinaendelea kujadili na kukosoa misingi ya ufeministi na itikadi zake. >>

Hii leo katika nchi za Magharibi kunaenezwa sana fikra ya usawa na mfanano kamili baina ya mwanamke na mwanaume kutokana na kuenea fikra za ufeministi, na suala hilo limesababisha mgogoro mkubwa wa kijamii. Kwa sababu kabla ya jambo lolote, nara na kaulimbiu hiyo imekuwa na madhara makubwa kwa wanawake wenyewe. Hii ni kwa sababu kwa kutumia kisingizio hicho cha usawa na mfanano wa mwanamke na mwanaume, kumetolewa fikra ya kugawana sawa majukumu ya kifamilia baina ya mwanamke na mwanaume, na mahari, matumizi anayolazimika kutoa mwanaume kwa mkewe vimetoweka na kufutwa kabisa kwa kisingizio kwamba vinadunisha shakhsia huru na inayojitegemea ya mwanamke na kumfanya kiumbe tegemezi kwa mwanaume. Hivyo wanawake wanalazimika kuvamia masoko ya kazi na ajira kwa ajili ya kudhamini na kukidhi mahitaji yao ya kifedha na kwa shabaha ya kulinda shakhsia zao za kijamii.

Katika upande mwingine wanawake, kutokana na dukuduku za masuala ya kifamilia na tofauti za kimaumbile na kivipawa, hawawezi kushindana na wenzao wanaume hususan katika upande wa masuala ya uongozi. Kidhahiri chekechea na mabweni vimeweza kwa kiasi fulani kupunguza dukuduku za wanawake, na vyakula vya kununua mikawahawani vinaweza kwa kiasi fulani kuziba pengo la kutokuwepo kina mama majumbani mwao; lakini katika maeneo ya kazi, wanawake wamechakaa na kutaaabika zaidi kimwili na kiroho kuliko wanaume na wanalazimika kustahamili mashinikizo ya kazi za nyumbani sambamba na sulubu za kazi za nje ya nyumba. Baya zaidi ni kuwa wanawake wanaofanya kazi nje ya nyumba kivitendo wamepoteza uwezo wa ubunifu ndani ya taasisi ya familia kama mke na mama. Kwa msingi huo, wanawake wamebakia kuwa wanadamu wenye maisha yasio na roho, ari, vuguvugu la upendo, na kuishi katika mazingira yasiyofaa ya kazi na hatimaye katika ukosefu wa maelewano na mume na watoto.  >>

Miongoni mwa misingi ya kifikra ya ufeministi ni moyo wa kupiga vita wanaume na kupinga kabisa majukumu ya mwanamke. Baadhi ya mafeministi ambao wanakana suala la kuwepo tofauti za kimaumbile kati ya mwanaume na mwanamke kimsingi wanaitambua jinsia ya mwanaume kuwa ni adui nambari moja wa mwanamke na wanasisitiza sana juu ya udharura wa kupambana naye. Baadhi ya maandishi ya kundi hilo wanaweka mipaka ya kisiasa baina ya mwanamke na mwanaume badala ya kuainisha msingi na chanzo cha upotofu wa jamii mbalimbali ambacho ni ujinga na ubinafsi wa jinsia hizo mbili. Katika upande mwingine kwa kuzingatia kwamba utamaduni mpya wa Magharibi umejengeka kwa msingi wa maslahi ya mtu binafsi na unafanya jitihada za kuimarisha mfumo wa ubepari wa Magharibi, matokeo ya ubinafsi na maslahi ya mtu binafsi ni mgongano baina ya maslahi ya watu binafsi na makundi mbalimbali ya kijamii na matunda yake ni kutanguliza mbele haki kuliko maadili.

Matokeo mengine ya ubinafsi huko Magharibi ni kwamba kila mmoja kati ya mwanamke na mwanaume ni kiumbe anayejitosheleza na asiyemhitajia mwenzake na kila mmoja wao huangaliwa peke yake katika ratiba na mipango yote ya masuala ya kiutaumaduni na kisheria. Fikra ya mgongano na mpambano baina ya mwanaume na mwanamke ni matokeo ya mtazamo huu. Hata hivyo katika mtazamo wa Uislamu, ni kwa kukubali hakika ya tofauti za kimaumbile zilizopo baina ya jinsia hizo mbili na kutilia maanani mwongozo wa Mwenyezi Mungu pamoja na kutayarishwa mazingira ya maelewano na ushirikiano ndipo inawezekana kupatikana maslahi na manufaa ya jinsia hizo mbili na si kinyume chake.

Wakati fikra ya mgongano na vita baina ya mwanamke na mwanaume inapoenezwa na kupigiwa debe katika jamii, kila mmoja kati ya jinsia hizo mbili humuona mwenzake kuwa ni adui na hufanya jitihada za kukabiliana naye zaidi. Matokeo ya mtazamo huo ni kutowajibika na kukimbia majukumu ya ndoa. Kwa sasa katika nchi za Magharibi kunajitokeza aina nyingine ya jinsia ya kiume ambayo ni adui mkubwa na hatari zaidi kwa wanawake. Kundi hili la wanaume mashoga, halitaki kabisa kuwa na uhusiano wa aina yoyote na wanawake.

Dakta  Henry Makow ameandika katika kitabu cha "Ufeministi, Kushindwa kwa Ngano ya Ukombozi wa Wanawake" kwamba: Hatimaye utambulisho halisi wa ufeministi utadhihirika wazi. Mafemenisti wamemvua mwanaume shakshia yake ya kiume na kuwafanya wanawake kuwa wanaume, na katika njia hiyo jinsia zote mbili zimepoteza utambulisho wake…", Vilevile Dokta Tony Grant wa hukohuko Magharibi anasema: Mwanamke wa sasa ni mwanaume bandia. Wameanzisha vita dhidi ya wanaume wa kweli na kwa msingi huo wameparaganyikiwa na kukosa utulivu..".   >

Kwa sasa harakati ya ufeministi imeitumbukiza taasisi ya familia katika mgogoro mkubwa kwenye nchi za Magharibi kutokana na kueneza na kupigia debe fikra ya kupiga vita na kukana familia, kudhoofisha hisi za kuwajibika, moyo wa kutunza familia, maadili na kukata uhusiano baina ya mwanaume na mwanamke na kutotilia maanani fitra na maumbile ya jinsia hizo mbili. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei anasema katika uwanja huo kwamba: Harakati ya kumtetea na kumkomboa mwanamke katika nchi za Magharibi kwa hakika ni harakati kipofu, isiyo na mantiki, iliyojengeka kwa msingi wa ujahili, isiyotegemea misingi ya suna na kanuni za Mwenyezi Mungu wala maumbile asili na safi ya mwanadamu na hatimaye imekuwa na madhara kwa jinsia zote mbili japokuwa madhara yake ni makubwa zaidi kwa mwanamke.."   >

Msikose kujiunga nasi tena wiki ijayo katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachozungumzia na kukosoa fikra za ufeministi, itikadi na misingi yake. Hadi wakati huo tunakutakieni kila la kheri...

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)