Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 09 Novemba 2015 17:42

Ufeministi, itikadi na misingi yake (6)

Ufeministi, itikadi na misingi yake (6)

Karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi cha Ufeministi, Itikadi na Misingi yake. Katika kipindi cha wiki iliyopita tulizungumzia baadhi ya misingi ya kifikra ya ufeministi kama ubinafsi (Individualism) na kumtanguliza mwanadamu mbele ya kila kitu hata Mwenyezi Mungu na itikadi za kidini (humanism). Tulisema kuwa umuhimu wa mtu binafsi katika fikra za humanism umekwenda mbele zaidi kiasi kwamba kigezo na kipimo cha hata kanuni za kimaadili pia ni "mtu" mwenyewe na "matamanio" ya nafsi yake. Tulisema ubinafsi (individualism) na uasili wa ladha na anasa (hedonism) ni katika misingi ya fikra ya ufeministi. Tulisema maisha ya mtu kwa mujibu wa dhana hiyo yanafungama na kumhusu yeye peke yake na si kitu kingine chochote. Ana hiari ya kutenda chochote kwa mujibu wa idara ya matakwa yake. Wapenzi wasikilizaji kipindi chetu cha leo kitaendelea kujadili mada hii.

Itikadi za ubinafsi (individualism) na uasili wa anasa (hedonism) za ufeministi zimekuwa sababu ya wanawake kufuata matamanio yao ya kinafsi bila ya mpaka wowote. Kwa msingi huo kaulimbiu kama ile ya haki ya mwanamke ya kumiliki na kudhibiti mwili wake inayotawala fikra za ufeministi imeeneza sana masuala ya kuavya na kutoa mimba na vilevile uhuru wa maingiliano ya ngono kama haki za kimaumbile za wanawake. Mafeministi wanaoamini fikra za ubinafsi (Indivisualism) wanaamini kuwa, maadamu maslahi na manufaa ya mtu binafsi yanahalalisha kufanya lolote analopenda mtu, kwa nini mwanamke astahamili mashaka na mipaka inayotokana na kuwa mama na kuwa mwaminifu kwa mwanaume? Huu wapenzi wasikilizaji, ndio mwanzo wa kudhoofika misingi ya familia. Baada tu ya kuanza harakati ya ufeministi, watu wenye misimamo ya kupindukia katika harakati hiyo walisisitiza na kutilia mkazo umuhimu wa wanawake kupata nafasi yao kama watu binafsi bila ya kujali mahusiano ya kifamilia. Kwa msingi huo wimbi la pili la ufeministi lilitilia mkazo zaidi fikra kwamba, familia ndiyo kituo kikuu cha kumkandamiza mwanamke. Mabadiliko hayo kwa ujumla yalieneza misingi na mienendo ya ubinafsi ndani ya familia na matokeo yake familia kama taasisi muhimu ya mwanadamu inayoundwa na watu kadhaa, ilitoweka kabisa katika nchi za Magharibi. Hii leo pia maandiko na nyaraka za kimataifa zilizoathiriwa na fikra za kifeministi zinasisitiza sana haki ya mwanamke ya kuchagua aina ya uhusiano wa kingono, na kuchagua ama kufanya ngono na mwanamke mwenzake au jinsia tofauti. Mafeministi wanaamini kuwa ili kufidia yaliyopita na kufuta kabisa roho na tabia ya wanawake ya kusalimu amri na kutii waume zao, suala la uhuru wa mtu binafsi linapaswa kupewa kipaumbele na umuhimu mkubwa na kwamba kuna udharura wa kutiliwa mkazo zaidi uhuru wao wa mtu binafsi ili kwa njia hiyo tuweze kuimarisha moyo wa kukhitari na kujichagulia wakipendacho.

Matokeo ya itikadi za ubinafsi za ufeministi ni utawala wa matakwa na matamanio na kinafsi ya mwanadamu. Ni wazi kuwa, msingi huo unapingana na fikra na itikadi za Kiislamu. Sheria za Uislamu zimemwachia mtu binafsi uhuru wa kuridhisha matakwa yake ya kinafsi lakini wakati huo huo haumruhusu mwanadamu kuwa mtumwa na mateka wa matamanio hayo. Katika fikra za Kiislamu, Mwenyezi Mungu ndiye mhimili na msingi wa kila kitu, kwa sababu Yeye ndiye Muumbaji na Mmiliki wa kila kitu, na saada na ufanisi wa dunia na Akhera wa mtu haupatikani bila ya kufanya mambo yake kwa mujibu wa sheria na kanuni za Mwenyezi Mungu. Ubinafsi mutlaki ndani ya familia hauna maana yoyote katika fikra za Uislamu, na wanawake na wanaume wanawajibika mbele ya kila mmoja wao. Vilevile maendeleo na ufanisi wa mmoja wao ni maendeleo na ufanisi wa mwenzake.   >

Wafuatiliaji wa kipindi hiki mwanamke na mwanaume ni jinsia mbili tofauti ambazo zinatofautiana kutokana na sifa makhsusi za kimaumbile za kila mmoja wao. Hata hivyo linajitokeza swali kwamba, ni upi mpaka wa tofauti zilizopo baina ya mwanaume na mwanamke?

Baadhi ya mafeministi na wataalamu wa masuala ya kijamii wanaamini kuwa, hakuna tofauti yoyote baina ya jinsia hizo mbili isipokuwa tofauti za kibiolojia na kwamba tofauti nyingine kama zile za mawazo na tabia zinatokana na taathira za kimazingira na kiutamaduni na hazina msingi wowote wa kimaumbile. Mkabala wake, wataalamu wengi wa elimu nafsi wanasisitiza kuwa, kuna tofauti za kimaumbile baina ya mwanamke na mwanaume. Kwa mujibu wa mtazamo huo mwanamke na mwanaume ni sayari mbili zinazozunguka kuelekea pande mbili zinazohitilafiana. Mwanafalsafa wa Kijerumani, Immanuel Kant anasema, muundo wa kinafsi na kimwili wa mwanamke unatofautiana na wa mwanaume. Kant anaamini kuwa, ubunifu na nafasi ya kila mmoja wa wawili hao ndani ya familia inaainishwa kwa msingi wa tofauti hizo.

Katika mtazamo wa Uislamu mwanamke na mwanaume wanatofautiana si kimwili pekee, bali hata katika nyanja mbalimbali za kinafsi, kihisia, kimawazo na kimwenendo. Tofauti hizo zinaanzia zile za muundo wa mwili, wastani wa urefu na uzito na kiwango cha ubongo hadi tofauti katika tabia, ubunifu katika masuala ya sanaa, kiwango cha kustahamili, jinsi ya kuathiriwa na kuchochewa, uwezo wa kufikiria, upande wa kutambua uzuri na urembo na mambo mengine mengi. Katika mtazamo wa Uislamu, mwanaume na mwanamke wanakamilishana, na jambo hili linaonekana katika sifa za kimaumbile na katika haki na majukumu ya kila mmoja wao mkabala wa mwenzake. Hivyo kadiri wanadamu wanavyofanya jitihada za kukamilishana, ndivyo kadiri jinsia hizo mbili za wanadamu huelekea kwenye ukamilifu zaidi. Hata hivyo inatupasa kuelekwa kuwa, tofauti za kimaumbile si sababu ya jinsia moja kuwa bora kuliko nyingine, bali ni njia ya kutengeneza maisha bora kwa kiumbe mwandamu. Mwenyezi Mungu SW anasema katika aya ya 32 ya Suratu Zukhruf kwamba:  Sisi tumewagawanyia baina yao maisha yao katika uhai wa duniani, na tukawanyanyua baadhi yao juu ya wengine kwa daraja nyingi; kwa hivyo baadhi yao wanawafanya wengine wawatumikie. Na rehema za Mwenyezi Mungu ni bora kuliko hayo wanayoyakusanya."

Ni wazi kuwa, tofauti hizo ndiyo sababu ya kutokea mfumo wa kutumikiana kwa jinsia zote mbili, kukidhi mahitaji ya pande zote mbili, familia na jamii na sababu ya kumsukuma mwanaume kwa mwanamke na mwanamke kwa mwanaume na hatimaye sababu ya kukamilishana wawili hao, kuziba na kukidhi nakisi na mapungufu ya pande mbili na kujitokeza taasisi ya familia.

Kukamilishana kwa mwanaume na mwanamke kutatimia pale mwanadamu atakapotambua rasmi hisi ya kila jinsia kuihitaji jinsia tofauti. Uimara wa taasisi ya familia pia unafungamana na hisia hii ya kuihitajia jinsia tofauti. Kwani wakati mwanaume anapohisi kuwa, hana haja ya msaada wa mke katika familia, na kama mke hakumtambua mwanaume kuwa msaidizi wake ndani ya familia kwa kutegemea mali na utajiri wake, itawezekana vipi mwanaume na mwanamke kukamilishana na kujenga familia imara?

Katika fikra za Kiislamu mbali na kuthamini na kuenzi nafasi na majukumu ya kijamii ya mwanamke, vilevile kunatiliwa mkazo nafasi makhsusi ya mwanamke na mwanaume katika taasisi ya familia. Katika dini ya Uiislamu kila mmoja kati ya mwanamke na mwanaume ana mchango na nafasi mbili zinazokamilishana ndani ya familia na katika jamii, na majukumu hayo ya pamoja na makhsusi yanapaswa kulindwa katika kila hali kwa mujibu wa vigezo na mipaka ya kidini.

Tunakomea hapa kwa leo, tukutane tena wiki ijayo katika sehemu nyingine panapo majaaliwa ya Mwenyezi Mungu.

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)