Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 07 Machi 2015 12:23

Mauaji ya Kimbari (20)

Mauaji ya Kimbari (20)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Karibuni katika sehemu hii ya 20 ya makala ya mauaji ya kimbari katika zama zetu hizi. Tunaendelea kuzungumzia mauaji ya kimbari na jinai zinazoendelea kufanywa kikatili na makundi ya kigaidi ambayo yamejipachika majina ya Kiislamu hususan kwa vile kundi la Daesh linaendelea kufanya jinai za kutisha katika maeneo mbalimbali kuanzia Syria na Iraq hadi Libya, barani Afrika. Ni matumaini yetu mtakuwa nasi hadi mwisho wa dakika hizi chache za kukuleteeni sehemu hii ya 20 ya mfululizo wa makala hii. Karibuni.

*******Wapenzi wasikilizaji, siku ya Jumamosi ya tarehe 21 mwezi uliopita wa Februari, televisheni ya al Iraqiya ya nchini Iraq ilitangaza kuwa, kundi la kigaidi la Daesh, limewaua kwa kuwachoma moto hadi kufa Wairaq 50 mjini Hīt, kaskazini magharibi mwa mji wa ar Ramadi nchini Iraq. Televisheni hiyo iliongeza kuwa, kundi hilo lilifanya jinai hiyo kwa kutegemea maandishi ya vitabu vya Ibnu Taymiya ambayo hayakubaliani kabisa na mafundisho sahihi ya Uislamu. Jambo la kusikitisha zaidi ni kuendelea propaganda za kuvionesha vitendo viovu vya kundi hilo kuwa eti vinatokana na mafundisho ya Uislamu, wakati Wamagharibi wenyewe wanakiri kuwa, ni wao ndio walioliunda kundi hilo la kigaidi na kuliunga mkono hadi leo hii. Hivi karibuni, televisheni ya lugha ya Kiarabu ya CNN ya Marekani ilimnukuu Jenerali mstaafu wa nchi hiyo, Wesley Clark, akikiri kwamba Washington na waungaji wake mkono ndio walioanzisha kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh na kwamba lengo kuu lilikuwa ni kukabiliana na harakati ya Hizbullah ya Lebanon. Jenerali Clark ambaye aliwahi kuwa kamanda wa Jumuiya ya Kijeshi ya Nchi za Magharibi (NATO) kuanzia mwaka 1997 hadi 2000, alisema katika televisheni hiyo ya CNN ya Marekani kwamba lengo la kuundwa kundi la Daesh, ni kuiangamiza harakati ya Hizbullah ambayo ni tishio kwa Israel. Jenerali huyo mstaaafu wa Marekani alisema: "Kundi la Daesh lilianzishwa kwa msaada mkubwa wa fedha kutoka kwa waitifaki na rafiki zetu ambao walilizatiti kwa silaha dhidi ya Hizbullah." Pia alisema, serikali ya Washington imekuwa ikitoa mamilioni ya dola kwa ajili ya kuchafua sura ya Hizbullah. Aidha alisema, Marekani inasaidia sana katika kusambaza picha za jinai za kutisha zinazofanywa na kundi hilo la kitakfiri duniani kupitia vyombo vyake vya habari. Kabla ya hapo pia Webster Griffin, mwanahistoria, mwandishi, mhadhiri na mtaalamu maarufu wa masuala ya kisiasa wa Marekani alifichua uhusiano wa karibu mno uliopo baina ya Abubakar al Baghdadi, kiongozi wa kundi la Daesh na Seneta John McKean wa jimbo la Arizona la Marekani aliyewahi kugombea urais wa nchi hiyo na kusema kuwa, kundi hilo la kigaidi ni jeshi la siri la Marekani katika nchi za Kiislamu na za Kiarabu. Kuunda na kuunga mkono madola ya Magharibi, makundi ya kigaidi yanayotenda jinai kubwa kama lile la Daesh, hakuna madhara tu kwa Waislamu, bali kunawasababishia matatizo makubwa pia Wakristo na watu wa dini nyinginezo wanaoishi kwenye maeneo zinakofanyika jinai za makundi hayo. Ni hivi majuzi tu ambapo kundi la Daesh liliwachinja kama wanyama na kuwaua kwa umati, Wakristo 21 raia wa Misri katika mji wa bandari wa Derna nchini Libya. Wakristo wa nchini Iraq nao hawakusalimika na jinai hizo za Daesh. Hata Wakristo wa nchini Syria nao wamekumbwa na jinai za makundi ya kigaidi kama vile Jabhatun Nusra. Hata hivyo muda umeisha kwa leo tutaendelea na mada hii katika sehemu ijayo ya mfululizo huu. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)