Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 21 Februari 2015 12:59

Mauaji ya Kimbari (18)

Mauaji ya Kimbari (18)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Hii wapenzi wasikilizaji ni sehemu ya 18 ya mfululizo wa makala hizi za mauaji ya kimbari katika zama zetu hizi. Tunaendelea kutupia jicho mauaji ya kimbari yanayofanywa na makundi ya kitakfiri yaani yanayokufurisha Waislamu wengine hususan kundi la kibaath la Daesh. Kundi hilo hadi leo hii linaendelea kufanya mauaji ya kutisha dhidi ya kila anayepinga fikra zake za kumkufurisha kila asiyekubaliana nalo. Si hayo tu lakini pia linatenda jinai za kutisha dhidi ya watu hao kama ilivyotokea hivi karibuni kuwateka nyara na kuwaua kikakatili Wakristo 35 wa Misri katika mji wa bandari wa Derna huko Libya. Karibuni.

*******

Mtandao wa Intaneti wa The Gulf Today wa Umoja wa Falme za Kiarabu yaani Imarati uliripoti siku ya Jumatano ya Februari 18, kwamba kundi la Daesh limewachoma moto hadi kufa Wairaki 45 katika mji wa al Baghdadi. Mtandao huo ulimnukuu Kanali Qasim al Obeidi, afisa wa polisi wa mji huo akithibitisha habari hiyo. Mtandao huo ukaongeza kuwa, mauaji hayo ya kuwachoma moto watu hadi kufa yamefanywa na Daesh baada ya kundi hilo kusambaza video inayoonyesha namna walivyomchoma hai hadi kufa rubani wa Jordan Luteni Maaz al Kassasbeh wakiwa wamemfungia ndani ya kirimba na tundu la chuma ili asiweze kutoka. Hayo ni kwa mujibu wa mtandao huo wa The Gulf Today wa nchini Imarati. Amma Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Iraq amenukuliwa akisema kuwa, kundi la kigaidi la Daesh linawatumia watoto wa chini ya miaka 15 ili kufanya opereseheni za kigaidi na kuwatumia kama ngao ya binadamu. Hadi hivi sasa pia maelfu ya wananchi wa Iraq wametoweka na hawajulikani walipo. Jambo hilo limewatia wasiwasi mkubwa viongozi wa Iraq. Wengi wa watu hao wasiojulikana waliko ni wanawake na mabarobaro ambao ni wahanga wa jinai za kundi la Daesh. Jinai nyingine zinazofanywa na kundi hilo la kibaath ni kuwalazimisha kuolewa kwa nguvu wasichana na wanawake, kuanzisha bidaa ya ajabu waliyoipa jina la Jihadun Nikah, kuteka nyara watu, kuwafunga watu, kuwapiga mnada na kuwauza kama bidhaa wanawake na watoto wadogo na jinai nyinginezo nyingi ambazo zinaendelea kulalamikiwa kimataifa hadi leo hii. Katika moja ya ripoti zake, Umoja wa Mataifa ulilalamikia vikali mauaji yanayofanywa na kundi la Daesh dhidi ya Waislamu. Kwa mujibu wa moja ya ripoti hizo, baada ya kuiteka jela ya mji wa Mosul wakati ambapo nusu ya wafungwa waliokuwepo kwenye jela hilo walikimbia, kundi la Daesh liliwafanyia usaili wafungwa waliobakia na kuwatenga wafungwa 1500 kutokana na itikadi zao za Kishia. Baada ya hapo ikawachukua wafungwa hao na kuwatia kwenye malori hadi kwenye umbali wa kilomita tatu kutoka katika jela hiyo. Walipofika nao jangwani wakawapanga katika safu nne na kuua kwa umati wafungwa 670. Tab'an baadhi ya wafungwa hao walikuwa ni Masuni ambao walikataa kuwakufurishwa Waislamu wenzao wa Kishia. Nao waliingizwa kwenye mkumbo huo.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)