Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 14 Februari 2015 12:14

Mauaji ya Kimbari (17)

Mauaji ya Kimbari (17)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Karibuni katika sehemu hii ya 18 ya mfululizo wa makala hizi za mauaji ya kimbari katika zama zetu hizi. Leo tutaendelea kutupia jicho mauaji ya kimbari yaliyofanywa na makundi ya kitakfiri yaani yanayokufurisha Waislamu wengine katika nchi za Iraq na Syria. Katika sehemu iliyopita tulijaribu kuonesha namna propaganda za kwamba kundi la Daesh ni la Waislamu wa Kisuni, au linawawakilisha Waislamu wote kutokana na kujiita Dola la Kiislamu, zilivyokuwa hazina mashiko wala msingi wowote kutokana na vitendo viovu na jinai za kundi hilo lililoundwa na linaloendelea na jinai zake kwa msaada wa madola ya Magharibi na vibaraka wao. Karibuni.


*******

Katika toleo lake la Oktoba 10, 2014, Mtandao wa habari wa International Business Times ulimnukuu mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, Staffan de Mistura akifananisha mzingiro uliokuwa umeukumba mji wa Kikurdi wa Waislamu wa Kisuni wa Kobani huko Syria na mzingiro uliofanywa na Waserbia huko Srebrenica, Bosnia Herzegovina mwaka 1995 ambako zaidi ya Waislamu 8,000, wanaume, watoto wadogo na wanawake wauliuwa kwa umati. Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa alifanya hivyo kama juhudi za kuwashawishi viongozi wa Uturuki wazuie kutokea mauaji zaidi ya kimbari huko Syria. Mtandao huo uliendelea kuandika: Kundi la Daesh limeanzisha mashambulizi makubwa dhidi ya mji huo wa Kisuni huko Syria kwa kutuma mamia ya wapiganaji wake. Umoja wa Mataifa uliwataka viongozi wa Uturuki waruhusu wapiganaji wa Kikurdi wa Peshmerga waelekee huko Kobani Syria kwenda kuulinda mji huo. Hata hivyo, viongozi wa Uturuki ambao wanashutumiwa kuyasaidia makundi ya kigaidi yanayofanya mauaji katika nchi za Iraq na Syria, walitoa masharti ya kutengwa eneo lililo marufuku kupaa ndege ndani ya ardhi ya Syria na vile vile walikataa kushiriki katika jitihada za kuwaokoa Waislamu hao wa mji wa Aynul Arab huko Syria hadi pale Rais Bashar al Assad wa Syria atakapoondoka madarakani. Tab'an ni vyema tukiashiria hapa kwamba, kwa mujibu wa baadhi ya ripoti, tayari mji wa Kobani wa Syria umeshakombolewa baada ya kufurushwa wanamgambo wa Daesh kwenye mji huo. Amma jambo la kusikitisha ni kuona kuwa, kundi la kigaidi la Daesh linahusishwa kwa makusudi na Waislamu wa Kisuni na baadhi ya wakati vyombo vya habari vya Magharibi vinafanya njama za makusudi za kueneza propaganda kwamba eti kundi la Daesh linawawakilisha Waislamu wote duniani. Hata hivyo kundi hilo haliwawakilishi Waislamu wa Kisuni, wala Waislamu wote duniani, bali ni kundi la kitakfiri na kibaath ambalo halikubaliani na fikra za kundi lolote jingine hata yale ambayo yana mitazamo ya kitakfiri kama yake. Katika moja ya matamshi yake, Fadhil al Gharrawi, mjumbe wa Kamati ya Haki za Binadamu ya Iraq alisema kwenye makao makuu ya Bunge la nchi hiyo mjini Baghdad kwamba, watoto wadogo wa Iraq wako katika hatari ya kukumbwa na maafa makubwa baada ya kundi la kigaidi la Daesh kuteka mikoa ya Nainawa na Salahuddin na kufanya operesheni za kinyama za kigaidi. Hadi wakati anatoa matamshi hayo, zaidi ya watoto elfu moja walikuwa wameshauliwa kwa umati na kundi la Daesh na zaidi ya watoto 400 walishakuwa wakimbizi kwenye mkoa huo wa Iraq. Watoto wengi walipoteza maisha wakati wa kuzaliwa kutokana na kukosekana suhula za maana za uzazi katika kambi walizokimbilia wazazi wao. Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Iraq iliutaka Umoja wa Mataifa na shirika la UNICEF kuchukua hatua za haraka wa kuwasaidia watoto wadogo waliotumbukia kwenye maafa makubwa kutokana na jinai za Daesh katika mikoa wa Salahuddin na Nainawa, huko Iraq. Muda umeisha, tutaendelea na makala hii katika sehemu ya 19 ya mfululizo huu.


Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

 

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)