Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 07 Februari 2015 11:14

Mauaji ya Kimbari (16)

Mauaji ya Kimbari (16)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Karibuni katika sehemu hii ya 16 ya mfululizo wa makala hizi fupi fupi zinazozungumzia mauaji ya kimbari katika zama zetu hizi. Baada ya kuzungumzia mauaji ya kimbari yaliyofanywa katika nchi za Rwanda, Bosnia Herzegovina na Palestina, leo hii tutaanza kutupia jicho mauaji ya kimbari yaliyofanyika katika nchi za Iraq na Syria na nafasi ya jamii ya kimataifa katika mauaji hayo. Karibuni.


*******


Daesh ni jina la kundi la kigaidi ambalo lina misimamo mikali ya kuona kuwa kila linachoamini kundi hilo ndicho sahihi na kila kinachoaminiwa na makundi mingine ni batili. Kundi hilo linaundwa na watu wenye fikra za Kisalafi na watu wenye fikra za kibaath wa utawala wa Saddam uliopinduliwa nchini humo. Kundi hilo linadai kuunda utawala wa Khilafa na umezisababishia matatizo mengi mno nchi za Iraq na Syria. Kundi hilo limefanya mauaji makubwa sana katika nchi hizo, bila ya kujali aina ya watu linaowaua. Kundi la kigaidi na kibaath la Daesh liliundwa tarehe 15 Oktoba 2006 baada ya kufanyika vikao kadhaa baina ya makundi yenye silaha nchini Iraq. Tangu lilipoundwa; kundi hilo limeshatangaza kuhusika katika operesheni na mashambulio mengi ya kigaidi nchini Iraq. Baada ya kufichuka nafasi ya Abubakar al Baghdadi akiwa kiongozi kundi hilo, vitendo vya kigaidi vya kundi hilo viliongezeka sana. Mwishoni mwa mwezi Septemba 2013 na mwanzoni mwa mwezi Aprili 2014 wakati jeshi la Iraq lilipoanzisha operesheni za kuusafisha mkoa wa al Anbar, wanamgambo wa Daesh waliuvamia mji wa Fallujah mkoani humo, na kufanya vitendo vingi vya kigaidi. Ripoti zinasema kuwa, katika nusu ya pili ya ya mwaka 2013, kundi la Daesh liliripua nyumba 1400 za watu nchini Iraq. Watu wasiopungua elfu mbili waliuawa na zaidi ya elfu tatu wengine wakajeruhiwa. Mwezi Mei 2014, wanamgambo wa Daesh waliyavamia makao makuu ya mkoa wa Nainawa, yaani Mosul na kuuteka mji huo. Silaha zilizopatikana kwa kundi la kigaidi la Daesh zinaonesha ni kiasi gani madola ya kigeni yanalisaidia kupindukia kundi hilo. Watu wa jinsia na mataifa tofauti ambao imma imepatikana miili yao au kutiwa mbaroni katika mapambano na kundi hilo la Daesh, wanazidi kuthibitisha kuwa kundi la kigaidi la Daesh linaundwa na watu kutoka kona mbalimbali za dunia. Ushahidi unaonesha kuwa mabaki ya utawala uliopinduliwa wa Saddam nchini Iraq, yana nafasi kubwa katika kuundika na katika vitendo vya kigaidi vya Daesh. Kuna na madola ambayo hayakufurahishwa na kuingia madarakani viongozi waliochaguliwa na wananchi nchini Iraq, nayo yanahesabiwa kuwa na mkono wa moja kwa moja katika kuundika kundi hilo. Madola hayo ni madola jirani na hata ya Ulaya ambayo viongozi wa Iraq, mara kwa mara wamekuwa wakilalamika kuwa yanachochea ugaidi nchini humo. Tangu kuasisiwa kwake, kundi la Daesh lilitangaza wazi nia yake ya kuliangamiza kundi lolote ambalo halikubaliani na fikra zake. Kundi hilo lilitekeleza kivitendo jambo hilo kwa kuafanya mauaji ya kutisha dhidi ya raia wa Iraq. Maelfu ya Waislamu wa Kishia na Kisuni, Wakristo na watu wa kabila la Yazidi huko kaskazini mwa Iraq ni katika wahanga wakuu wa vitendo hivyo vya kigaidi na mauaji ya kimbari ya kundi la Daesh. Tutaendelea na mada hii katika sehemu ya 17 ya mfululizo huo.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)