Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 18 Januari 2015 15:52

Mauaji ya Kimbari (14)

Mauaji ya Kimbari (14)

Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Karibuni wasikilizaji wapenzi katika sehemu hii ya 14 ya mfululizo wa makala hizi fupi fupi za Mauaji ya Kimbari katika zama zetu hizi. Tunaendelea na kuzungumzia mauaji ya kimbari yaliyofanywa na Wazayuni huko Ghaza katika miezi ya hivi karibuni. Kwenye sehemu ya 13 ya mfululizo huu pamoja na mambo mengine tulisema kuwa: Utawala wa Kizayuni wa Israel ulifanya mauaji ya kimbari katika mashambulizi yake ya siku 50 huko Ghaza kwa kifua kipana na kwa kutangaza kuwa ni haki yake kufanya hivyo. Tulilinukuu gazeti la Kizayuni la Times of Israel ambalo liliandika makala maalumu chini ya kichwa cha maneno: Wakati mauaji ya kimbari yalipokuwa yanajuzu ambapo mwandishi Mzayuni, Yochanan Gordon alisema kuwa kuuliwa kwa umati Wapalestina wote ni jambo linalojuzu jambo ambalo lilitekelezwa kivitendo na wanajeshi makatili wa Kizayuni katika mashambulizi yao huko Ghaza. Leo tutaendelea mbele na mada hiyo. Karibuni.

                                                                                             *******

Wasikilizaji wapenzi, wanadamu wangali wanaikumbuka vizuri Ujerumani ya Kinazi ya utawala wa Hitler ya miaka ya 1939 hadi 1945. Msimamo wa Wazayuni wa kuhalalisha mauaji ya watu kwa madai ya kufikia lengo ndio mMsimamo huo huo aliokuwa nao Hitler ikiwa ni pamoja na kupenda kutanua mipaka yake ya utawala kwa kuzivamia na kuzikalia kwa mabavu nchi nyingine za Ulaya. Kama ambavyo Hitler hakuheshimu sheria zozote za kimataifa, ni vivyo hivyo walivyo Wazayuni, wanakaidi kila kitu kinachoitwa sheria ya kimataifa mbele ya Wapalestina. Leo hii Wazayuni wanalikuza kupindukia suala la vitendo vya utawala wa Hitler huko Ujerumaini kwa kujionesha kuwa walidhulumiwa sana na utawala huo, na matokeo yake wameaumua kuteka ardhi za Wapalestina na kuwafanya mamilioni ya Wapalestina kuwa wakimbizi katika kona hii na ile duniani. Kama inadaiwa kuwa Hitler alikuwa dhidi ya Mayahudi, leo hii utawala wa Kizayuni wa Israel nao ni dhidi ya Wapalestina na unafanya kila njia kuliangamiza kikamilifu taifa la Wapalestina na kila anayesimama kupinga jinai zao huko Palestina.
Uhakika kwamba Wazayuni wanafanya mauaji ya kimbari huko Palestina si jambo lililofichikana tena mbele ya walimwengu na mbele ya wanasiasa wengi duniani. Hayo yameshuhudiwa katika hotuba mbalimbali za viongozi tofauti wa kisiasa duniani.
Miongoni mwa viongozi hao ni Fidel Casro, kiongozi maarufu wa Cuba. Aliandika makala ya kuwaunga mkono Wapalestina chini ya kichwa cha maneno: "Mauaji ya Kimbari ya Wapalestina wa Ghaza" na ndani yake alilaani jinai na mauaji ya kimbari yanayofanywa na Wazayuni dhidi ya wakazi wa Ghaza na kuelezea kusikitishwa mno na namna nchi nyingine duniani na jamii za kimataifa zinavyonyamazia kimya jinai hizo. Aidha aliandika kwamba, zaidi ya watoto 400 walikuwa wameshauawa shahidi huko Ghaza hadi wakati anaandika makala hiyo.
Jinai za Wazayuni huko Ghaza zilipelekea pia kuzuka upinzani wa Mayahudi duniani. Zaidi ya Mayahudi 300 walionusurika kwenye mauaji ya Mayahudi wakati wa utawala wa Hitler huko Ujerumani au wana na wajukuu wa wahanga hao waliandika barua ya wazi kulaani mauaji yaliyokuwa yanafanywa na Israel dhidi ya wananchi wa Palestina na kusema kuwa hayo ni mauaji ya wazi ya kimbari. Barua hiyo ilichapishwa kwenye gazeti la New York Times toleo la Jumamosi, Agosti 23, 2014 na waliotia saini barua hiyo ya wazi waliitaka Israel iache kuuzingira Ukanda wa Ghaza. Waliilaumu Marekani kwa kuiunga mkono kijeshi Israel. Barua hiyo ilibeba kichwa kisemacho: Mauaji ya Kimbari mbele ya kimya cha walimwengu. Tutaendelea na mada hii katika sehemu ya 15 ya mfululizo huu Inshaallah. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)