Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 03 Januari 2015 09:56

Mauaji ya Kimbari (12)

Mauaji ya Kimbari (12)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Katika sehemu 11 zilizopita za mfululizo huu mbali na kuzungumzia maana na sifa maalumu za istilahi ya mauaji ya kimbari kimataifa, tumetoa pia mifano kadhaa na kujadili kwa kina kiasi, mauaji ya kimbari yaliyotokea katika nchi za Rwanda na Bosnia Herzegovina na namna jamii ya kimataifa pamoja na nchi za Magharibi na Umoja wa Mataifa na mashirika yanayodai kutetea haki za binadamu duniani yalivyoruhusu kutokea kwa makusudi mauaji hayo dhidi ya watu wasio na hatia. Hii ni sehemu ya 12 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za mauaji ya kimbari katika zama zetu hizi. Karibuni.

******

Leo wapenzi wasikilizaji tutaanza kutupia jicho mauaji ya kimbari yaliyotokea miezi ya hivi karibuni dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Ghaza. Utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa siku zote unatekeleza njama zake za kuwagombanisha na kuwazozanisha Wapalestina. Hata hivyo makundi ya Kipalestina yaliona hakuna njia nyingine ila kuimarisha umoja baina yao na baada ya muda mrefu wa mazungumzo yenye misuguano mingi, Wapalestina walifikia makubaliano ya kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa na kuunganisha nguvu zao kwa ajili ya kupigania haki zao. Hatua hiyo iliwakasirisha mno Wazayuni na hivyo ikawa wanatafuta kisingizio cha kumalizia hamaki zao kwa Wapalestina. Haukuwa umepita hata muda mrefu tangu makundi ya Palestina yafikie mwafaka wa kuunganisha nguvu zao, ambapo Wazayuni walizuka na madai ya kutoweka walowezi watatu wa Kizayuni na baadaye Wazayuni hao hao wakatangaza kuwa miili ya vijana hao wa kilowezi imepatikana na hapo hapo wakadai kuwa Hamas ndiyo iliyohusika na mauaji ya walowezi hao bila ya kutoa ushahidi wowote na licha ya kwamba Hamas ilikanusha vikali madai hayo. Katika wiki ya pili ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, Wazayuni wakatumia kisingizio hicho kuanzisha mashambulizi ya kikatili na kinyama dhidi ya wakazi wa Ghaza. Waislamu wenye saumu wa Ghaza ambao wamezingirwa kila upande wakaanza kushambuliwa kikatili kwa kila aina ya silaha hata zilizopigwa marufuku, na kuufanya mwezi huo wa Ramadhani kuwa mwezi wa damu kwao. Katikati ya mashambulizi hayo, Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni akatoa amri ya kuingia ardhini wanajeshi wa Israel kwenye Ukanda wa Ghaza. Mashambulizi hayo ya siku 50 yalipelekea karibu Wapalestina 2,200 kuuawa shahidi na zaidi ya elfu kumi wengine kujeruhiwa. Mashirika ya haki za binadamu nayo yametoa ripoti mbalimbali yakisema kuwa, watoto wadogo wanaunda zaidi ya nusu ya wahanga wa ukatili huo wa Wazayuni. Mads Gilbert, ni daktari raia wa Norway anayefanya kazi katika hospitali ya Shifa mjini Ghaza. Hivi karibuni alizungumza na mwaandishi wa habari mjini Brussels na kuonesha picha za vitoto vichanga vya Kipalestina vilivyouliwa shahidi au kujeruhiwa katika mashambulizi hayo ya Israel. Na hapo hapo akahoji kwa kusema, je vitoto hivi vichanga navyo ni magaidi? Madaktari wa kigeni mjini Ghaza wametangaza kuwa, asilimia 80 hadi 90 ya wahanga wa mashambulizi ya kinyama ya Wazayuni huko Ghaza ni raia wa kawaida na moja ya nne ya wahanga hao ni watoto wadogo. Wanajeshi wa Kizayuni hawakumuhurumia yeyote katika mashambulizi yao ya kikatili huko Ghaza. Inaonekana walikuwa na chuki za muda mrefu dhidi ya binadamu, dhidi ya hospitali na vituo vya matibabu, dhidi ya magari ya wagonjwa na ya misaada, dhidi ya misikiti na mashule, dhidi ya raia, dhidi ya miti, dhidi ya wanyama na dhidi ya kila kitu kilichoonekana kwenye Ukanda wa Ghaza. Walikuwa wanashambulia kwa hamaki na chuki, kila kilichokuwa mbele yao. Lengo la Wazayuni katika ukatili huo usio na kifani lilikuwa ni kung'oa mizizi ya fikra ya muqawama na kusimama kidete taifa la Palestina katika kupigania haki zao. Wazayuni wanaamini kuwa watoto hao wachanga wa Kipalestina, kuna siku watakuwa wakubwa na watasimama kulinda heshima ya taifa lao na kupigania haki zao. Hivyo kwa Wazayuni, kila kitu kinachohusiana na Palestina kimo kwenye orodha yao ya magaidi.Muda umeisha, tutaendelea na maudhui hii katika kipindi kijacho Inshaallah. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)