Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 27 Disemba 2014 06:53

Mauaji ya Kimbari (11)

Mauaji ya Kimbari (11)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Karibuni katika sehemu hii ya 11 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za zinazozungumzia mauaji ya kimbari katika zama zetu hizi. Katika sehemu iliyopita, pamoja na mambo mengine tulisema kuwa, mwaka 2004, mahakama ya kimataifa ya kufuatilia jinai za Yugoslavia ya zamani ilitangaza rasmi kwamba mauaji yaliyofanyika dhidi ya wakazi wa maeneo ya kaskazini mwa Bosnia hususan eneo la Srebrenica, yalikuwa ni mauaji ya kimbari. Waserbia waliwalazimika wanawake, watoto wadogo na vizee karibu elfu 25 hadi 30 kuhama makazi yao. Jinai hiyo nayo ilihesabiwa na mahakama hiyo kuwa ni ushahidi wa kuthibitisha kwamba jeshi la Serbia lilifanya kwa makusudi mauaji ya kimbari. Leo tunaendelea na tulipofikia.
KASIDA
Wapenzi wasikilizaji, mwezi Februari 2007, mahakama ya kimataifa ya jinai za Yugoslavia kwa kifupi ICJ ilisema: Mahakama (hiyo) imefikia uamuzi kwamba, vitendo vilivyotendeka huko Srebrenica ambavyo vinajumuishwa katika vipengee vya A na Be vya kifungu cha pili cha makubaliano (ya Geneva), vinahesabiwa kuwa ni mauaji ya kimbari ambayo yalifanywa na wanajeshi wa Serbia katika mji wa Srebrenica na vitongoji vyake kuanzia tarehe 13 Julai 1995. Idadi kubwa ya waliouliwa katika mauaji hayo ya kimbari walikuwa ni watu wa makamo, mabarobaro na vijana. Kati ya wahanga wa mauaji hayo ya kimbari walikuwemo pia vijana wadogo wa chini ya miaka 15, wanaume wa zaidi ya miaka 65, wanawake na hata watoto wachanga. Hadi kufikia mwezi Juni 2011, miili 6594 iliyofukuliwa kutoka katika makaburi ya umati ilikuwa imeshafanyiwa uchunguzi wa vinasaba DNA na kujulikana wasifu wao. Mauaji ya kimbari ya Srebrenica yaliutumbukiza kwenye lawama kubwa Umoja wa Mataifa na Katibu Mkuu wake wa wakati huo, Kofi Annan. Baadhi ya viongozi wa nchi za Magharibi nao walikiri kwamba viongozi wa baadhi ya nchi hizo hususan Uholanzi pamoja na Umoja wa Mataifa walizembea kazi zao na hivyo kuruhusu kutokea mauaji ya kimbari ya Srebrenica. Kwa mfano Jack Straw, waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Uingereza amesema dunia imefedheheka kwa kushindwa kuzuia mauaji yaliyofanywa na Waserbia huko Bosnia. Naye Kofi Annan, Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa mataifa amesema, matukio ya Srebrenica yataendelea kuuadhibu moyoni Umoja wa Mataifa. Marc Brown, mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa naye amesema maneno kama hayo kwamba jinai za Srebrenica zimeutia doa lisilofutika Umoja wa Mataifa.
Wahusika wakuu wa mauaji ya kimbari ya Bosnia walikuwa ni Radovan Karadžić, Rais wa wakati huo wa Serbia na Ratko Mladić, kamanda wa jeshi wa zamani wa Serbia. Karadžić alitiwa mbaroni tarehe 21 Julai 2008 huko Belgrade na Mladić alitiwa nguvuni siku ya Alkhamisi ya tarehe 26 Mei, 2011 huko Lazarevo. Mwezi Julai 2014 pia mahakama moja nchini Uholanzi ilitoa hukumu na kuibebesha lawama serikali ya Uholanzi kuhusu mauaji ya kimbari ya zaidi ya Waislamu 300 huko Srebrenica yaliyofanywa na Waserbia mwaka 1995. Waislamu hao 300 walikuwa ni kati ya Waislamu 5000 wa Bosnia walioomba hifadhi kwa askari wa kulinda amani wa Uholanzi mwezi Julai mwaka 1995. Mahakama hiyo ya mjini Hague Uholanzi ilisema kuwa, askari wa kulinda amani walishindwa kuwalinda Waislamu wa Bosnia wakati walikuwa wanajua kuwa kuna hatari ya kutokea mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu hao. Kwa kweli mauaji ya kimbari ya Bosnia Herzegovina yameonesha kuwa, hata katika dunia ya leo inayodaiwa kustaarabika, uko uwezekano wa kutokea mauaji ya kutisha ya kimbari huku mashirika ya kutetea haki za binadamu yakishindwa kutekeleza ipasavyo wajibu wao. Tab'an mauaji ya kimbari yanaendelea hivi sasa katika maeneo tofauti ya dunia na wahanga wake wakubwa ni Waislamu. Hata hivyo muda umeisha kwa leo. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)