Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Ijumaa, 19 Disemba 2014 11:07

Mauaji ya Kimbari (10)

Mauaji ya Kimbari (10)

Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Hii wapenzi wasikilizaji ni sehemu ya kumi ya mfululizo wa makala hizi za Mauaji ya Kimbari katika zama zetu hizi. Tumesema huko nyuma kuwa, Waserbia kwa baraka kamili za madola ya Magharibi walifanya jinai kubwa dhidi ya Waislamu wa Bosnia Herzegovina. Walianzisha vita hivyo vya kikatili wakijua vizuri mno muundo wa kifamilia wa Waislamu na walikuwa wanajua ni kitu gani wakiwafanyia Waislamu watakuwa wamewaumiza kupindukia kiroho na kuwadhalilisha kupita kiasi Waislamu hao. Ndio maana waliwanajisi wanawake na wasichana mbele ya familia zao, waliwatenganisha watoto na wazee wao sambamba na kufanya mauaji ya kutisha kama vile kuwachukua juu ya daraja la mto Drina na kuwapiga risasi na kuacha viwiliwili vyao visivyo na roho vianguke kwenye mto huo ambapo mauaji yalikuwa makubwa kiasi kwamba maji ya mto yaligeuka rangi ya damu. Leo tutaendelea na tulipofikia.

*******

Madhara ya jinai za kinyama za Waserbia dhidi ya Waislamu wa Bosnia zilianza kuonekana zaidi mwaka 1993. Akiendelea kutoa kisa chake cha kusikitisha, Bi "Hajic" Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wanawake Waliopata Madhara katika vita vya Bosnia anasema: Hivi sasa na licha ya kwamba watuhumiwa wengi wa jinai hizo wametiwa nguvuni, lakini bado kuna watu wengi waliofanya jinai kubwa katika miji ya Višegrad, Brčko, Foča na miji mingine ya Bosnia hawajatiwa mbaroni na ni wafanyakazi katika idara za polisi, au viwandani au katika wizara ya elimu. Bibi "Hajic" anasema, hawawezi kutulia mpaka wahakikishe kuwa watenda jinai wote wametiwa mbaroni na kufikishwa mbele ya sheria. Anasema jumuiya yao haipiganii haki za wanawake Waislamu tu, bali inapigania pia haki za wanawake wa Serbia na Croatia. Anasema, Waserbia waliotenda jinai huko Bosnia Herzegovina hawakuwahurumia bali waliwanajisi pia hata wanawake wa Kiserbia na Kicroatia ambao walikuwa wameolewa na Waislamu.
Pamoja na kwamba jinai hizo zilizofanyika katika maeneo hayo ya kaskazini mashariki mwa Bosnia Herzegovina zilikuwa ni kubwa sana, lakini jinai kubwa zaidi za mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu huko kaskazini mashariki mwa Bosnia Herzegovina zilifanyika katika mji wa Srebrenica. Watu karibu 8000 waliuliwa kwa umati katika mji huo wa Waislamu. Mwezi Aprili 1993, Umoja wa Mataifa ulitangaza kuwa, eneo lililozingirwa la Srebrenica lililoko katika bonde la Drina huko kaskazini mashariki mwa Bosnia Herzegovina, ni eneo salama na linalindwa na askari wa Umoja wa Mataifa. Hata hivyo mwezi Julai 1995, kikosi cha Umoja wa Mataifa kilichojulikana kwa jina la UNPROFOR kilichoundwa na askari wa Uholanzi kwa ajili ya kulinda usalama wa eneo hilo, kiliruhusu kwa makusudi kuvamiwa na kutekwa eneo hilo la Srebrenica na askari wa Serbia na huo ndio ukawa mwanzo wa kufanyika jinai kubwa sana dhidi ya Waislamu wa eneo hilo. Mwaka 2004, mahakama ya rufaa ya kimataifa iliyokuwa inashughulikia masuala ya Yugoslavia ya zamani ilitangaza rasmi kwamba mauaji yaliyofanyika dhidi ya wakazi wa eneo hilo, yalikuwa ni mauaji ya kimbari. Waserbia waliwalazimika wanawake, watoto wadogo na vizee karibu elfu 25 hadi 30 kuhama makazi yao. Kitendo hicho kilihesabiwa na mahakama hiyo kuwa ni ushahidi wa kuthibitisha kwamba jeshi la Serbia liliazimia kufanya mauaji ya kimbari. Na hivyo ndivyo ilivyotendeka. Muda umeisha, tutaendelea na makala hii katika sehemu ijayo tukijaaliwa. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)