Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 13 Disemba 2014 08:52

Mauaji ya Kimbari (9)

Mauaji ya Kimbari (9)

Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Karibuni wapenzi wasikilizaji katika sehemu hii ya tisa ya Mauaji ya Kimbari. Katika sehemu iliyopita yaani sehemu ya nane ya mfululizo huu tulianza kutupia jicho mauaji makubwa ya kimbari yaliyotokea katika zama hizi barani Ulaya yaani mauji ya Waislamu wa Bosnia Herzegovina. Tulisema kuwa, mauaji hayo ya kimbari yaliyoanza mwaka 1992 dhidi ya Waislamu wa Bosnia Herzegovina katika Yugoslavia ya zamani, yalifanyika kwa baraka zote za madola ya Magharibi yanayodai kulinda na kutetea haki za binadamu ulimwenguni. Leo tutaendelea tulipofikia. Karibuni.

Wapenzi wasikilizaji, jumuiya ya kupigania haki za wanawake waliopata madhara katika vita vya Bosnia imesema katika ripoti yake kuwa, hadi hivi sasa Umoja wa Mataifa umeshapelekewa mafaili 2500 ya wanawake waliopata madhara katika vita vya Bosnia. "Hajic" ni mmoja wa wanawake mwanachama waandamizi wa "Jumuiya ya Wanawake Waliopata Madhara katika Vita vya Bosnia" amesema katika moja ya mahojiano aliyofanyiwa kama ninavyomnukuu: Wakati Bosnia ilipojitangazia uhuru wake mwaka 1992, mimi wakati huo nilikuwa ninaishi na mume wangu na mabinti zetu wawili katika mji wa Višegrad. Wakati vita vilipoanza mimi nilikuwa mfanyakazi katika Manispaa ya mji huo. Wakati huo nilikuwa ninaona kwa mastaajabu makubwa namna Waserbia walivyoanza kuondoka kwa wingi mjini humo licha ya kwamba kwa miaka mingi tulikuwa tunaishi pamoja kwa usalama, mapenzi na amani. Baada ya Waserbia kutoka mjini humo, mji wa Višegrad ukazingirwa na Waserbia mwaka 1992. Kuanzia wakati huo, Waserbia wakawa wanaingia katika nyumba moja baada ya nyingine na kumuua kila waliyemkuta katika nyumba hiyo. Waliua kikatili na kwa umati, Waislamu wengi sana. Walikuwa wanawachukua wanaume na wanawake na kuwapeleka juu ya daraja la mto Drina na kuwapiga risasi. Jina la daraja hilo lilikuwa ni la mwandishi maarufu wa riwaya aliyejulikana kwa jina la Ivo Andrić ambaye alipata tunzo ya Nobel kutokana na uandishi wake. Hata hivyo, ukatili wa Waserbia dhidi ya wakazi wa mji wa Višegrad uliyageuza rangi ya damu maji ya mto huo.
Bi "Hajic" anaendelea kuhadithia kisa chake cha kusikitisha akisema: Waserbia waliingia pia katika nyumba yake na wakamnajisi binti yake mdogo mbele ya macho yake na wakampiga na kumjeruhi vibaya kichwani binti huyo. Siku iliyofuata walikwenda wakamchukua nyumbani na kumpeleka kwenye kituo chao cha polisi. Huko anasema walimnajisi mara kadhaa. Anasema kwa huzuni kubwa kwamba jambo hilo lilikuwa chungu mno maishani mwake. Katika kituo hicho cha polisi, alimuona jirani yake Mserbia akishiriki katika uhalifu licha ya kwamba kabla ya kuanza uhalifu huo mwaka 1992 familia zao zilikuwa na mahusiano mazuri na walikuwa wakitembeleana. Anasema, kuwanajisi wanawake ilikuwa ni miongoni mwa stratijia na mikakati maalumu waliyokuwa nayo Waserbia katika vita hivyo vya kidhulma na vya umwagaji mkubwa wa damu walivyotwishwa Waislamu wa Bosnia Herzegovina. Kunajisi wanawake kulikuwa kunafanyika kwa mipangilio na stratijia maalumu. Watu walioanzisha vita hivyo vya kikatili walikuwa wanaujua vizuri mno muundo wa kifamilia wa Waislamu na walikuwa wanajua ni kitu gani wakiwafanyia Waislamu watakuwa wamewaumiza kupindukia kiroho. Walikuwa wanafanya vitendo hivyo wakijua kwamba watakuwa wamewadhalilisha kupita kiasi Waislamu hao. Tutaendelea na makala yetu hii katika sehemu ijayo Inshaallah. Ishini salama.

 

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)