Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 06 Disemba 2014 08:59

Mauaji ya Kimbari (8)

Mauaji ya Kimbari (8)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Karibuni wapenzi wasikilizaji katika sehemu hii ya nane ya mfululizo wa makala hizi fupi fupi zinazozungumzia Mauaji ya Kimbari kwenye zama zetu hizi. Katika sehemu kadhaa zilizopita tulitupia jicho mauaji ya kimbari ya nchini Rwanda na jinsi jamii ya kimataifa na madola makubwa kama vile Marekani, Ufaransa na Uingereza yalivyodharau jambo hilo na kuruhusu kutokea mauaji mabaya zaidi ya Watutsi na Wahutu wenye misimamo ya wastani karibu milioni moja nchini Rwanda. Tuliyoyasema katika vipindi hivyo ni machache mno ikilinganishwa na ukubwa wa jinai hiyo ya mwaka 1994 iliyofanywa na Wahutu wenye misimamo mikali nchini Rwanda. Muda ukituruhusu katika siku za usoni tutazungumzia vipengee vingine vya mauaji ya kimbari ya nchini Rwanda. Amma leo tutaanza kutupia jicho mauaji makubwa ya kimbari yaliyotokea katika zama hizi barani Ulaya. Karibuni.

*******

Baada ya kusambaratika Yugoslavia, kufuatia kura ya maoni ambapo asilimia 67 ya wananchi walishiriki, asilimia 98 ya walioshiriki kwenye kura hiyo walipiga kura ya kujitenga Bosnia Herzegovina na hivyo kuanzia mwaka 1992, kukatangazwa uwepo wa nchi inayoitwa Bosnia Herzegovina katika uso wa dunia. Huo ndio uliokuwa mwanzo wa vita vya Bosnia. Waserbia wa Bosnia Herzegovina walisusia kura hiyo ya maoni. Waserbia hao waliokuwa wanaungwa mkono na Serbia na Montenegro, waliamua kuunda jamhuri ya Waserbia wa Bosnia kwa lengo la kuisambaratisha na kuikata vipande vipande nchi changa ya Bosnia Herzegovina na kuiunganisha jamhuri hiyo na ardhi ya Serbia Kuu. Kwa hakika vita vilivyoanzishwa na Waserbia dhidi ya Bosnia Herzegovina havikuwa vita vya kitaifa na wala vya kugombania ardhi, bali lengo lake hasa lilikuwa ni kuangamiza kizazi kizima cha Waislamu katika eneo hilo. Ni kwa sababu hiyo ndio maana, madola ya Magharibi yalinyamazia kimya jinai zilizofanywa na Waserbia karibu miaka 22 iliyopita katika eneo hilo lililoko kwenye kitovu ya bara la Ulaya linalojigamba kuwa limestaarabika. Kuna jinai kubwa sana zilifanyika katika vita hivyo vya kinyama na kwamba kovu chafu la ukatili huo litaendelea kuwepo milele katika paji la uso la wale wanaodai kutetea haki za binadamu duniani. Jinai hizo zilianzia kwenye kuwaua kwa umati Waislamu hadi kuwanajisi wanawake na wasichana kwa shabaha ya kuangamiza kikamilifu mbari ya Waislamu. Tunapotupia jicho matukio ya kusambaratika Yugoslavia ya zamani ambayo kusambaratika kwake kumezaa jamhuri sita tofauti tutaona kuwa, hakuna nchi yoyote mpya iliyojitangazia uhuru wake kutoka kwa Yugoslavia iliyopata madhara na kushuhudia jinai kama ilivyojiri kwa Bosnia Herzegovina ambayo asilimia kubwa ya watu wake ni Waislamu. Damu nyingi ya Waislamu ilimwagwa, wakati ambapo zile nchi zilizojitenga na Yugoslavia na ambazo wakazi wake wengi ni Wakristo, zilijitenga bila ya matatizo yoyote na hazikusakamwa kwa hali yoyote ile. Ni kwa sababu hiyo ndio maana Waislamu wa Bosnia Herzegovina hadi leo hii wanazilaumu tawala na serikali za nchi za Ulaya kwa kushiriki katika jinai za Waseribia ambao waliwaua kwa umati maelfu ya watu wasio na hatia huko Bosnia Herzegovina. Hii ni kusema kuwa, kwa mara ya kwanza kabisa, Waserbia walitumia kuwanajisi wanawake na wasichana wadogo pamoja na kuua watoto wadogo kama mbinu za kijeshi dhidi ya Waislamu wa Bosnia Herzegovina. Ripoti za kuaminika zilizowasilishwa kwa Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa, katika vita hivyo vilivyoanzishwa na Waserbia dhidi ya Wabosnia, zaidi ya raia laki tatu waliuawa na maelfu ya wanawake walinajisiwa. Tutaendelea na mada hii katika sehemu ijayo ya mfululizo huu tukijaaliwa.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)