Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 29 Novemba 2014 10:38

Mauaji ya Kimbari (7)

Mauaji ya Kimbari (7)

Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji. Hii ni sehemu ya saba ya mfululizo wa makala hizi za Mauaji ya Kimbari. Katika sehemu ya sita ya mfululizo huu tulisema kuwa, jamii ya kimataifa na nchi za Magharibi zilikuwa na taarifa ya kutokea mauaji makubwa ya kimbari nchini Rwanda hata kabla ya kutokea kwake mwaka 1994. Tulisema, haikuwa sadfa kwa Umoja wa Mataifa kutuma askari wa kofia buluu wa kulinda amani nchini Rwanda mwishoni mwa mwaka 1993. Hata hivyo jamii ya kimataifa iliacha mauaji hayo ya kimbari yatokee kwa madai ya eti haiwezi kuingilia masuala ya ndani ya Rwanda. Tulitoa ushahidi mbalimbali wa kuthibitisha jambo hilo. Leo tutaendelea na tulipofikia.

Wapenzi wasikilizaji, itakumbukwa kuwa miezi miwili kabla ya kutokea mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994, Jacques Roger Bobo, alitumwa nchini Rwanda kuwa mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kwani umoja huo ulikuwa unapokea taarifa za kukaribia kutokea mauaji makubwa ya kimbari huko Rwanda. Ni kwa sababu hiyo ndio maana mara tu baada kuanza kuharibika hali ya usalama huko Rwanda na kabla ya kupamba moto mauaji hayo, vikosi vya Umoja wa Mataifa vilianza kuondoa raia wa kigeni nchini humo. Hata hivyo Baraza la Usalama la umoja huo halikutoa idhini kwa vikosi hivyo kuzuia mauaji hayo. Umoja wa Mataifa ulishindwa hata kutumia neno mauaji ya kimbari katika taarifa zake. Rais wa wakati huo wa Marekani alikuwa ni Bill Clinton. Katika moja ya hotuba zake alionesha kutoshughulishwa na mauaji hayo ya Rwanda kwa kudai kuwa ni vita vya kikabila tu ndivyo vilivyokuwa vinaendelea nchini Rwanda, wakati mamia kwa maelfu ya Watutsi na Wahutu wenye misimamo ya wastani walikuwa wanauliwa kwa umati nchini humo. Ni mara moja tu ambapo Kofi Annan, Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa alisema, hatuwezi kusahau kwamba jamii ya kimataifa ilishindwa kuzuia mauaji ya watu laki nane, wanawake na watoto wadogo wasio na hatia nchini Rwanda. Alisema, tunapaswa tukiri kwamba hatukutekeleza wajibu wetu wakati wa mauaji hayo na tulishindwa kuzuia mauaji hayo ya kimbari. Dola la kikoloni la Ufaransa ambalo lilikuwa rafiki mkubwa wa utawala wa Wahutu huko Rwanda, lilituma kikosi chake nchini humo lakini askari hao wa Ufaransa hawakuchukua hatua zozote za kuzuia mauaji hayo. Mwaka 2008, tume moja ya uchunguzi nchini Rwanda ilitoa ripoti na kusema kuwa, Ufaransa ilikuwa na taarifa kamili kuhusiana na njama za Wahutu za kufanya mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi na ni dola hilo la kikoloni la Ufaransa ndilo lililowapa mafunzo wanamgambo wa Interahamwe waliofanya mauaji ya kimbari nchini Rwanda. Hadi hivi sasa wanaharakati wa haki za binadamu wanaulaumu Umoja wa Mataifa na baadhi ya madola makubwa ya Magharibi kwa kushindwa kuzuia mauaji ya kimbari nchini Rwanda. Hadi leo hii, serikali ya kikoloni ya Ufaransa inakana kuhusika katika mauaji ya kimbari ya nchini Rwanda. Ni mara moja tu na tena kutokana na kwamba alikuwa anatembelea Rwanda ndipo Nicolas Sarkozy, Rais wa zamani wa Ufaransa alisema kuwa, wanapaswa kukiri kwamba Paris walifanya baadhi ya makosa wakati wa mauaji ya kimbari ya Rwanda. Hata hivyo Rais Paul Kagame wa Rwanda alisema kuwa, kuna wakati Ufaransa ilishirikiana na wanamgambo wa Kihutu waliofanya mauaji hayo na kuna wakati kulifanyika mauaji kwa uungaji mkono wa wanajeshi wa Ufaransa huko Rwanda. Baada ya mauaji hayo ya kutisha huko Rwanda, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliunda mahakama ya kimataifa ya kuwafuatilia watenda jinai hizo. Wahalifu wengi wamekamatwa na kuhukumiwa mahakamani, lakini hilo haliwezi kufuta makovu ya mateso waliyopata wahanga wa mauaji hayo. Wanachotaka wahanga hao ni kuhakikisha chuki za kikabila zinazimwa na kila upande unatekeleza vizuri majukumu yake, ili kuzuia kutokea tena jinai kama hizo za mwaka 1994.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)