Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 22 Novemba 2014 11:47

Mauaji ya Kimbari (6)

Mauaji ya Kimbari (6)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya sita ya mfululizo wa makala hizi zinazoangalia kwa muhtasari istilahi ya mauaji ya kimbari, historia na madhara yake. Katika sehemu ya tano ya mfululizo huu tuliendelea kutoa maelezo kuhusu mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda na tulimalizia kwa kisa cha mmoja wa wahanga wa mauaji hayo ya kutisha Bi Mary, ambaye katika kisa chake cha kusikitisha alisema kuwa, katika siku za awali za mauaji hayo ya kimbari na baada ya wanamgambo wa Interahamwe kumvamia na kumnajisi, alikimbilia nyumbani kwa ami yake. Huko nako lakini aliona unyama wa kutisha kwani siku chache tu baadaye jeshi la Kihutu lilivamia nyumba hiyo. Bi Mary anasema, walipofika katika nyumba hiyo walimuua kila aliyekuwemo ndani. Anasema, yeye alijificha chini ya kitanda na aliona namna magaidi hao walivyomuua shangazi yake na kukichukua kitoto chake kichanga na kukiweka juu ya kifua chake. Damu ilitapakaa kila mahala. Kila mtu alikuwa maiti katika nyumba hiyo isipokuwa kitoto hicho kichanga ambacho kiliendelea kunyonya maziwa ya mama yake aliyekufa. Leo tutaendelea kutokea hapo katika mfululizo huu.

*******

Jambo la kusikitisha ni kuona kuwa jinai na mauaji ya kimbari nchini Rwanda yalifanyika mbele ya macho ya jamii ya kimataifa na jamii hiyo iliandalia kwa macho tu kwa madai kuwa eti haiwezi kuingilia masuala ya ndani ya Rwanda. Kitabu maarufu cha Shake Hands with the Devil (Kupeana Mikono na Shetani) cha Romeo Dallaire, jenerali mstaafu wa jeshi la Canada, kuna nyaraka na ushahidi muhimu unaohusiana na mauaji ya kimbari ya nchini Rwanda. Tarehe 7 Aprili 1994, jenerali huyo mstaafu alikuwa kamanda wa kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini Rwanda. Anasema alipewa amri ya kuondoka nchini Rwanda kama ilivyotolewa kwa askari wote wa kigeni waliokuweko nchini humo. Lakini yeye aliamua kupinga amri hiyo, na alibakia nchini Rwanda. Anasema, jamii ya kimataifa ambayo inataka demokrasia itawale katika kona zote za dunia, ilikaa kimya mbele ya jinai hizo kana kwamba hakuna chochote kilichokuwa kinatokea huko Rwanda. Katika siku za awali kabisa za mauaji hayo ya kimbari, askari 1000 wa Ulaya waliotumwa nchini Rwanda kuondoa raia wa kigeni, waliondoka haraka nchini humo. Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Ubelgiji ambao walikuwa wanalinda mashule yaliyokuwa yamewahifadhi Watutsi elfu mbili, waliwatelekeza Watutsi hao na kuondoa nchini Rwanda baada ya kutolewa amri hiyo, jambo ambalo lilifungua uwanja wa kufanyika mauaji makubwa ya kimbari dhidi Watutsi hao. Bi Linda Melvern, mwandishi na mtafiti kutoka Uingereza anasema kuwa, nchi nyingi duniani zilikuwa na taarifa kuhusu mauaji ya kimbari ya Rwanda na zilifanya makusudi kutowasaidia wananchi wa Rwanda. Anatoa mfano akisema: Kwa mfano serikali ya Ubelgiji ilikuwa na taarifa kamili kuhusu jinai hiyo. Wiki chache kabla ya kutokea mauaji hayo, serikali ya Ubelgiji iliwataka wanadiplomasia wa Uingereza na Marekani katika Umoja wa Mataifa wafanye mpango wa kuongezwa idadi ya askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa huko Rwanda. Hata hivyo Uingereza na Marekani zilikataa ombi hilo la Ubelgiji kwa madai ya kutokuwa na fedha. Upinzani huo wa Marekani na Uingereza ulipelekea kupasishwa amri ya kuondolewa askari wa kigeni nchini Rwanda na hivyo kufungua njia kwa makundi ya mauaji kufanya ukatili mkubwa nchini Rwanda.
Miezi miwili kabla ya kutokea mauaji ya kimbari nchini Rwanda, Jacques Roger Bobo, alitumwa nchini humo kuwa mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa. Kutokana na ripoti ambazo Umoja wa Mataifa ulikuwa unazipokea kutoka nchini Rwanda, umoja huo ulikuwa unajua kuwa kuna mauaji mkubwa yamekaribia kutokea nchini humo. Haikuwa sadfa kwa umoja huo kutuma askari wa kofia buluu wa kulinda amani nchini Rwanda mwishoni mwa mwaka 1993. Muda umeisha. Kwaherini....

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)