Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 22 Novemba 2014 11:45

Mauaji ya Kimbari (5)

Mauaji ya Kimbari (5)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Hii ni sehemu ya tano ya makala hizi fupi fupi zinazotupia jicho istilahi ya mauaji ya kimbari, historia na madhara yake. Leo tutaendelea kuzungumzia kiundani kidogo kuhusu mauaji ya kimbari ya nchini Rwanda ya mwaka 1994 na wasababishaji wake wakuu. Karibuni.

******

Wapenzi wasikilizaji, tunaendelea moja kwa moja na tulipofikia katika makala iliyopita. Makala hizi zinapatikana pia kwenye mtandao wetu wa Intaneti wa Kiswahili.irib.ir. Tarehe Mosi Julai mwaka 1962, Rwanda ilipata uhuru wake kutoka kwa mkoloni Mbelgiji na mwaka 1973, Juvenal Habyarimana kutoka kabila la Kihutu, akawa Rais wa Rwanda. Siasa za Habyarimana zilishadidisha chuki baina ya Wahutu na Watutsi huku Watutsi walio wachache wakikandamizwa vibaya katika utawala huo. Utawala wa Habyarimana ulilipa nguvu suala la ukabila kiasi kwamba ulianzisha kundi la mauaji la Interahamwe ambalo lilikuja kufanya jinai mbaya nchini Rwanda. Tarehe 6 Aprili 1994, ndege iliyokuwa imembeba Rais Juvenal Habyarimana wa Rwanda ilitunguliwa wakati ilipokuwa inarejea nyumbani kutoka katika nchi jirani ya Tanzania kwenye mazungumzo ya amani kati ya Wahutu na Watutsi. Masaa machache tu baada ya kuangushwa ndege ya Habyarimana, genge la Interahamwe kwa kushirikiana na vikosi vya serikali lilianzisha mauaji mabaya ya kimbari huko Rwanda dhidi ya kabila ya Kitutsi ambalo lilidaiwa kuhusika na utunguaji wa ndege ya Rais huyo wa Rwanda. Mauaji hayo ya kimbari yaliendelea kwa miezi kadhaa, ambapo katika kipindi cha chini ya miezi mitatu, karibu watu milioni moja, Watutsi na Wahutu wenye misimamo ya wastani waliuliwa kwa umati na Wahutu wenye misimamo mikali. Amma cha kusikitisha ni kuwa mauaji hayo makubwa ya kimbari yalifanyika mbele ya kimya na kutojali jamii ya kimataifa. Karibu moja ya 10 ya Wanyarwanda waliuawa katika kipindi hicho mbele ya macho ya Umoja wa Mataifa. Wahutu wenye misimamo mikali hawakuwaonea huruma hata vitoto vichanga vinavyonyonya, na waliua watu kwa ukatili mkubwa. Waliwachoma moto wazima wazima Watutsi ndani ya nyumba zao. Hata Wahutu wenye misimamo ya wastani nao hawakusalimika na ukatili huo. Si hayo tu, lakini pia katika ukatili huo, mamia ya wanawake na wasichana wa Kitutsi walinajisiwa. Wanawake wengi wahanga wa jinai hiyo wameambukizwa virusi vya ukimwi. Licha ya kupita miaka 20 tangu kutokea jinai hiyo, lakini bado akinamama hao wanakumbuka machungu ya mateso na ukatili wa kuchupa mipaka waliofanyiwa na magaidi wa Interahamwe. Akinamama wameshindwa kuwaangalia kwa jicho zuri watoto waliowazaa kutokana na ukatili na kunajisiwa wakati wa jinai hiyo. Bi Mary, mmoja wa wahanga wa jinai hiyo anasema, katika siku za awali za mauaji hayo ya kimbari na baada ya wanamgambo wa Interahamwe kumvamia na kumnajisi, hakuwa na njia nyingine ila kukimbilia nyumbani kwa ami yake. Hata hivyo huko nako alishuhudia ukatili wa kupindukia. Siku chache baadaye, jeshi la Kihutu lilivamia nyumba hiyo. Bi Mary anasema, walipofika katika nyumba hiyo walimuua kila aliyekuwemo ndani. Ami yake, shangazi yake na kila mtu aliyekuwemo katika nyumba hiyo aliuawa. Anasema, yeye alijificha chini ya kitanda. Anasema aliona namna magaidi hayo walivyomuua shangazi yake na kukichukua kitoto chake kichanga na kukiweka juu ya kifua chake. Damu ilitapakaa kila mahala. Kila mtu alikuwa maiti katika nyumba hiyo isipokuwa kitoto hicho kichanga ambacho kiliendelea kunyonya maziwa ya mama yake aliyekufa. Tutaendelea mbele na kuzungumzia jinai hiyo katika sehemu inayofuata ya mfululizo huu. Kwaherini.

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)