Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 10 Novemba 2014 15:29

Mauaji ya Kimbari (4)

Mauaji ya Kimbari (4)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Hii ni sehemu ya nne ya makala hizi fupi fupi zinazotupia jicho istilahi ya mauaji ya kimbari, historia na madhara yake. Katika sehemu tatu zilizopita za mfululizo huu tuliangalia kwa muhtasari namna istilahi hiyo ilivyoingia katika msamiati wa kisiasa dunia, vigezo vinavyotumiwa na Umoja wa Mataifa kubainisha maana ya mauaji ya kimbari namna jamii ya kimataifa inavyoamiliana na jinai hiyo, tofauti baina ya mauaji ya kimbari na jinai dhidi ya binadamu n.k. Tulitoa mifano kadhaa ya mauaji ya kimbari yakiwemo yale mauaji ya kutisha yaliyofanyika nchini Rwanda mwaka 1994. Hivi karibuni pia tulishuhudia mauaji mabaya ya kimbari huko Ghaza, Palestina kama ambavyo tunaendelea kushuhudia pia jinai zinazofanywa na kundi la kigaidi la Daesh katika nchi za Iraq na Syria, huku jamii ya kimataifa ikishindwa kuchukua hatua zozote za maana za kukomesha jinai hizo. Leo katika sehemu hii ya nne tutaanza kuchambua kiundani kidogo mauaji ya kimbari ya nchini Rwanda. Karibuni.

******

Wapenzi wasikilizaji, mauaji ya kimbari ya nchini Rwanda ni mgogoro ambao vyombo vya habari vya Magharibi vimekuwa vikiuzungumza kama kisa na riwaya ya mateso makubwa waliyoyapata watu lakini wakati huo huo vinakwepa kulipa nafasi suala la kuzungumzia wahusika halisi wa kutokea mauaji hayo ya kimbari. Leo tutaanza kwa kuangalia wasababishaji wa mauaji ya kimbari yaliyotokea katika nchi hiyo ya katikati mwa Afrika isiyo na bahari na ambayo imezungukwa kila upande nchi nyingine. Mwaka 1918, Ubelgiji iliivamia nchi hiyo na kuanza kuikoloni na kuikalia kwa mabavu. Kabla ya hapo ilijulikana kwa jina la Rwanda-Urundi wakati ilipokuwa ndani ya makoloni ya dola jingine la Ulaya, yaani Ujerumani. Mwaka 1933 Ubelgiji ilifanya sensa ya nguvu ya kuhesabu watu nchini humo na kumpa kitambulisho kila mkazi wa nchi hiyo. Ikiwa ni katika njama zake zenye malengo ya muda mrefu za kikoloni, wakoloni hao wa Ulaya waliwagawa Wanyarwanda kwenye vitambulisho hivyo katika makabila matatu, Wahutu, Watutsi na Watwa. Wakoloni wa Ubelgiji hawakuwa na nia njema katika mgao huo. Walitumia mgao huo kuchochea hisia za kikabila nchini Rwanda. Waliwapa nguvu watu wa kabila la Kitusti walio wachache na kuwaonesha kuwa ni bora kiheshima na kwa kila kitu mbele ya makabila mengine mawili yaliyobakia, ikiwa ni kuandaa mazingira ya kuzuka ugomvi na vita vya wenyewe kwa wenyewe miaka mingi itakayofuata.

Baada ya kupita miaka 20 tangu kufanyika njama hiyo mbaya, Watutsi wakawa wana nafasi nzuri zaidi katika upande wa eilimu, kazi na nafasi za juu katika utawala ikilinganishwa na ndugu zao Wahutu. Hivyo wakoloni wa Ubelgiji wakawa wametengeneza tabaka moja jipya la watu huko Rwanda na kuwapachika jina la watu weusi walio kamili. Mfumo wa masomo wa mkoloni Mbelgiji ulitilia mkazo suala la kuwasomesha watoto wa machifu na wakuu wa kikabila waliojulikana kwa jina la Mwami na wingi wake Abami kwa ajili ya kujidhaminia nguvu kazi waliyohitajia. Mgao huo wa kikabila, kijamii na kisiasa umeleta madhara makubwa nchini Rwanda tangu mwaka 1920 hadi leo hii na mpaka leo bado kuna chembechembe za hisia hizo za kiuadui. Mgao huo uliwafanya Wahutu ambao ni wengi kuwaona ndugu zao Watutsi kuwa ni vibaraka wa wakoloni. Ndio maana, mwaka 1959, Wahutu waliamua kuanzisha vita dhidi ya Watutsi na Wabelgiji. Huo ukawa mwanzo wa uhasama mbaya baina ya makabila hayo ndugu na ambao ulipata nguvu baada ya Rwanda kupata uhuru wake kutoka kwa mkoloni Mbelgiji mwaka 1962. Tutaendelea na mada hii katika sehemu tano ya makala mfululizo huu.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)