Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 10 Novemba 2014 15:28

Mauaji ya Kimbari (3)

Mauaji ya Kimbari (3)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Karibuni wasikilizaji wapenzi katika sehemu hii ya tatu ya mfululizo wa makala hizi fupi fupi zinazochambua istilahi ya mauaji ya kimbari, historia na madhara yake. Katika sehemu ya pili ya mfululizo huu tuliangalia kwa muhtasari vigezo vinavyotumiwa na Umoja wa Mataifa kubainisha maana ya mauaji ya kimbari na tukakhitimisha sehemu hiyo ya pili kwa kutoa mifano michache ya mauaji ya kimbari yaliyotokea ulimwenguni. Amma leo na katika sehemu hii ya makala tutatupia jicho nafasi ya jamii ya kimataifa katika suala zima la Genocide yaani Mauaji ya Kimbari. Tutaangalia pia tofauti baina ya Mauaji ya Kimbari na jinai dhidi ya binadamu. Karibuni.

******

Wapenzi wasikilizaji, hadi mwanzoni mwa muongo wa 1990, jamii ya kimataifa ilikuwa haijachukua hatua zinazotakiwa kukabiliana na jinai hiyo ya Mauaji ya Kimbari kutokana na muundo wa kisiasa wa jamii hiyo. Lakini yalipotokea mauaji makubwa ya kimbari katika muongo wa 1990 hususan katika Yugoslavia ya zamani na Rwanda, Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama lililazimika kuanzisha juhudi kwa nguvu kubwa ili kupambana na jinai hiyo ikiwa ni pamoja na kuanzisha mahakama maalumu za kimataifa za kuwafuatilia watenda jinai hizo. Hadi wakati huo, mauji ya kimbari yalikuwa yakihesabiwa kuwa ni uhalifu tu dhidi ya binadamu lakini mauaji makubwa ya kimbari yaliyotokea kwenye miaka ya 90 yalitia nguvu nia ya kutofautisha waziwazi baina ya jinai dhidi ya binadamu na mauaji ya kimbari na kila moja kufanywa uhalifu unaojitegemea na adhabu zake nazo kuainishwa kwa kujitegemea. Kama tulivyoashiria huko nyuma, mambo yanayoingizwa katika orodha ya uhalifu wa mauaji ya kimbari ni kama vile kuingiza pigo kubwa katika usalama wa kimwili na kiroho wa watu wa kundi moja maalumu, kuchukua hatua za kuzuia kuzaana na kuongezeka idadi ya watu wa kundi fulani na kuwalazimisha watoto wa kundi fulani kutengana na kundi hilo na kuwahamishia kwa nguvu sehemu nyingine. Jinai za mauaji ya kimbari zinaweza kufanyika wakati wa vita na wakati wa amani. Kundi hilo la uhalifu linaweza kutendwa na viongozi serikalini au watu wasioko serikalini iwe ni wakati wa amani au wakati wa suluhu au wakati wa ugomvi, au kwa sura ya kimataifa au isiyo ya kimataifa. Kwa mujibu wa mtazamo wa jamii ya kimataifa, tofauti baina ya Mauaji ya Kimbari na jinai dhidi ya binadamu ni kwamba, huku sifa za Mauaji ya Kimbari zikiwa ni hizo tulizozitaja hapo juu, miongoni mwa sifa za jinai dhidi ya binadamu ni kwamba jinai hizo zinatendwa kwa kutumia shambulio kubwa, lililofanywa kwa makusudi na kupangwa tangu zamani dhidi ya jamii yoyote ile ya raia, isiyo ya wanajeshi kwa ajili ya kufanikisha na kutekeleza siasa za serikali au taasisi fulani.

Jamii ya kimataifa imeainisha mifano kadhaa ya jinai dhidi ya binadamu ikiwa ni pamoja na kufanya mauaji, kuwafanya watu watumwa, kuwanyanyasa, kuwadhalilisha kijinsia, utumwa wa kijinsia, kulazimisha watu kufanya ukahaba na uchafu wa kimaadili, ubaguzi wa rangi na wa kizazi pamoja na kumfunga au kumfanyia mtu unyanyasaji mkubwa wa kimwili tofauti na misingi mikuu ya sheria za kimataifa. Hivyo masuala matatu makuu, yaani shambulio dhidi ya jamii ya raia, ukubwa na shambulio au kufanywa kwake kwa makusudi na kwa mpangilio maalumu ni mambo ya lazima katika kuarifisha jinai dhidi ya binadamu. Jinai dhidi ya binadamu pia zinaweza kufanywa wakati wa amani na wakati wa vita na mzozo wa kutumia silaha. Ugomvi huo unaweza kuwa wa kimataifa au usio wa kimataifa na pia jinai hizo zinaweza kufanywa na serikali na pia na watu walioko nje ya serikali.

Muda umeisha wa kipindi hiki, tukutane katika kipindi kijacho tukijaaliwa. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)