Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 10 Novemba 2014 15:25

Mauaji ya Kimbari (2)

Mauaji ya Kimbari (2)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Karibuni wasikilizaji wapenzi katika mfululizo wa makala hizi fupi fupi zinazochambua istilahi ya mauaji ya kimbari, historia na madhara yake. Hii ni sehemu ya pili ya mfululizo huu ambapo leo na baada ya kuelezea historia fupi ya kuingia istilahi hiyo katika msamiati wa kisiasa baada ya Vita vya Pili vya Dunia, leo tutaangalia vigezo vinavyotumiwa na Umoja wa Mataifa kubainisha maana ya mauaji ya kimbari na tutakhitimisha sehemu ya leo ya makala hii kwa kutoa mifano ya mauaji ya kimbari yaliyotokea ulimwenguni. Karibuni.

******

Umoja wa Mataifa unazingatia vigezo kadhaa vikuu katika kuanisha neno genocide yaani mauaji ya kimbari. Kuua idadi ya watu kutoka kundi moja la watu, kuwadhuru vibaya kimwili na kiroho watu wa kundi hilo, kuharibu kwa makusudi maisha ya watu wa kundi hilo kwa ajili ya kuwaangamiza wote au baadhi ya watu wa kundi hilo, kuweka sheria za kuzuia kuzaana na kuongezeka idadi ya watu wa kundi hilo na mwishowe kuwahamisha kwa nguvu watoto wa kundi hilo na kuwapeleka katika kundi jingine la watu ni miongoni mwa vielelezo vinavyotumiwa na Umoja wa Mataifa kuainisha uangamizaji wa mbari na kizazi yaani genocide. Hivyo moja ya misingi na vielelezo vikuu vya uhalifu wa uangamizaji wa kizazi ni kwamba wahanga wa uangamizaji huo huwa wanatoka katika kundi moja maalumu la watu.

Vile vile miongoni mwa sifa kuu za uangamizaji wa kizazi ni kwamba hazihusiani tu na kuua watu kwa maelfu, bali inahusiana na malengo ya watendaji wa jinai hizo, yaani kulilenga kundi fulani la watu kwa nia ya kuliangamiza. Kuwafanya watu wa kundi hilo kuwa katika hatari ya kuuawa, kuhukumiwa kidhulma, kuporwa mali zao, kunyanyaswa, kufukuzwa katika makazi yao ya jadi na hatimaye kuuliwa kwa halaiki. Historia inaonesha kuwa, makundi ya kitaifa ni mepesi sana kuwa wahanga wa uhalifu huo. Makundi hayo hasa yale ya wachache, mara nyingi yanahesabiwa kuwa ni ya watu duni na yanaonekana ni ya watu baki hata ndani ya jamii na ardhi yao wenyewe. Kwanza watu hao wanapachikwa majina mabaya na kudaiwa kuwa ni hatari kubwa kwa nchi yao na hatimaye hufanywa shabaha ya unyanyasaji na ukandamizaji.

Licha ya kwamba baada ya Vita vya Pili vya Dunia jinai hiyo ilianza kuhesabiwa kuwa ni jinai kubwa zaidi kimataifa, lakini cha kusikikitisha ni kwamba walimwengu mara nyingi wameendeleea kushuhudia jinai hiyo ikitokea katika kona mbalimbali za dunia. Mwishoni mwa muongo wa sabiini, walimwengu walishuhudia mauji ya kimbari yaliyofanywa na jeshi jekundu huko Cambodia. Walimwengu walishuhudia pia mauaji ya kimbari yaliyofanywa na Wahutu dhidi ya Watutsi na dhidi ya Wahutu wenye misimamo ya wastani nchini Rwanda katika muongo wa 90, mauaji yaliyofanywa na Saddam dhidi ya Wakurdi na Mashia nchini Iraq katika miongo ya 80 na 90, mauji ya kimbari yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina huko Sabra na Shatila pamoja na mauaji ya kimbari ya hivi karibuni huko Ghaza, kuuliwa kwa umati Waislamu wa Bosnia Herzegovina, mauaji ya umati yanayofanywa na mabudha dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya huko Myanmar na mauaji mengineyo. Hiyo ni sehemu ndogo tu ya jinai kubwa zinazofanyika kwa jina la siasa za mauaji ya kimbari katika maeneo mbalimbali duniani. Tutaendelea mbele na makala hii katika sehemu ya tatu ambapo tutatupia jicho nafasi ya jamii ya kimataifa katika suala hilo, Inshaallah. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)