Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 15 Januari 2012 12:17

Madhara ya ulevi na athari zake (8)-mwisho

Madhara ya ulevi na athari zake (8)-mwisho

Kama wewe mpenzi msikilizaji ulikuwa mfuatiliaji wa vipindi hivi vya madhara ya ulevi na athari zake bila sHaka unakumbuka tulisema kuwa, utumiaji ulevi una taathira mbaya za kimwili na kiroho kwa mtumiaji, kiasi kwamba, baadhi ya madhara na athari zake haziwezi kufidika. Hii leo utumiaji ulevi umegeuka katika baadhi ya jamii na kuwa tatizo kubwa na kila siku madhara yake katika jamii hizo yanazidi kuongezeka na kutishia mustakabali wa jamii husika. Watalaamu wengi wanaamini kuwa, kuna mambo na sababu nyingi zinazowafanya baadhi ya wanajamii hasa katika ulimwengu wa Magharibi kumili katika ulevi na utumiaji pombe. Mtafiti mmoja wa Kimarekani anayejulikana kwa jina la Horton baada ya kufanya utafiti katika muongo wa 1940 alifikia natija hii kwamba, kadiri kiwango cha mvurugiko na hali ya kutetereka katika jamii kitakavyokuwa kingi basi ndivyo utumiaji wa pombe unavyoongezeka kwa kiango hicho hicho. Anasema kuwa, katika utafiti huo inaeleweka wazi kwamba, endapo thamani na utamaduni unaotawala katika jamii utakuwa ni utamaduni na thamani ambazo zinashajiisha watu kutumiaji ulevi, bila shaka jambo hilo litakuwa na taathira kubwa katika kuongeza kiwango cha utumiaji ulevi katika jamii hiyo.
Wataalamu wa mambo wanataja sababu kuu mbili za kimsingi ambazo anasema zinachangia watu kuelekea katika utumiaji ulevi, sababu ambazo wamezigawa katika makundi mawili yaani sababu za ndani na za nje.
Wanasema kuwa, sababu za ndani ni msononeko, matatizo ya kisaikolojia, hali ya wasi wasi na kutofungamana na misingi ya dini na ya kiakhlaqi. Sababu za nje ni kama vile umasikini, hali mbaya ya kijamii na kiuchumi, kutokuweko uthabiti wa kiutamaduni, kusambaratika maisha ya familia na kujihusisha wanajamii na mambo machafu pamoja na ufuska. Majimui ya sababu hizi ni mambo yanayotajwa kuwa yanaongeza uwezekano wa kumili upande wa utumiaji madawa ya kulevya na ulevi.
Wapenzi Wasikilizaji kama ambavyo vitu vinavyosababisha kuelekea upande wa utumiaji ulevi vinagawanywa mara mbili, yaani sababu za ndani na za nje, tiba ya hilo pia inapaswa kugawanywa katika sehemu kuu mbili yaani tiba ya nje na ya ndani. Kuimarisha imani ya dini hupelekea thamani za kimaanawi ziimarike katika mahusiano ya kijamii na hivyo watu kuwa na maadili yanayotakiwa. Utafiti uliofanywa unaonyesha kwamba, kushikamana na mafundisho ya dini ni sababu kuu yenye taathira muhimu katika usalama na uzima wa kinafsi na kisaikolojia. Kwani kushikamana na mafundisho ya dini huyafanya maisha kupata maana yake halisi. Hapana shaka kuwa, kuwa na imani thabiti juu ya Mwenyezi Mungu ni kinga muhimu ya kuwafanya wanaadamu wasikengeuke na kwenda katika njia isiyo sahihi. Hatua ya mwanadamu ya kurekebisha mahusiano yake na Mwenyezi Mungu humfanya afikie matumaini ya kweli katika maisha na kwa wenzo huo huweza kutatua matatizo yake mengi ya kibinafsi, kijamii na kifamilia.
Kwa muktadha huo, mwanaadamu huwa hana haja tena ya kutumia ulevi na madawa ya kulevya kwa ajili ya kufikia katika ladha na malengo ya uongo na ya muda mfupi, akijidanganya kwamba, kwa njia hiyo amepata utulivu na kusahau matatizo yanayomkabili. Kwani utulivu wa kweli na wa kudumu unapatikana katika kivuli cha mahaba na mapenzi ya Mwenyezi Mungu.
Ni katika mazingira kama hayo tunaona kuwa, furaha ya kiroho huchukua nafasi ya msononeko na kujiinamia; na nishati hii humkinga mwanaadamu na kupotoka na hali ya kukengeuka. Huu ndio ule mfumo wa udhibiti wa ndani ambao una nguvu zaidi ya mfumo wa udhibiti wa nje.
Kwa mtazamo wa dini tukufu ya Kiislamu ni kuwa, udhibiti wa nje hautoshi kukabiliana na ufisadi na madhambi ya watu, bali kuna haja ya kuweko udhibiti wa ndani ambao kimsingi ni imani na mafundisho sahihi ya dini tukufu ya Kiislamu. Hivyo tunaweza kusema kuwa, kufungamana na mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu ni kinga imara ya kumzuia mtu na upotofu pamoja na kufanya mambo machafu yakiwemo masuala ya ulevi na utumiaji madawa ya kulevya. Ndio maana pindi ngome hii inapovunjwa na kuharibiwa hujitokeza njia ya kudhihiri anuwai kwa anuwai ya ufisadi na mambo machafu kama utumiaji wa madawa ya kulevya na ulevi.
Mwisho tunaashiria hapa kuwa, Mwenyezi Mungu mwenye huruma amemuumba mwanaadamu na vilivyomo na kumleta hapa duniani ili anufaike na vilivyomo kwa njia sahihi na kwa mujibu wa maamrisho na mafundisho ya dini.
Kama tulivyosema katika vipindi vyetu vilivyopita ni kuwa, moja ya madhara makubwa ya utumiaji ulevi ni mfarakano katika familia, maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi, unene kupita kiasi, utapiamlo hasi, mimba kuharibika na kisukari. Baadhi ya wataalamu wanasema kuwa, utumiaji ulevi una mahara ya aina mbili. Kwanza ni kuathirika kwa mishipa ya fahamu mwilini kote kwa kupunguzwa uwezo wa kufanya kazi kama inavyotakiwa; na pili ni kuungua baadhi ya ogani za mwili hasa tumbo pindi mtu anapokunywa pombe. Ni kwa kuzingatia uhakika huo ndio maana mafundisho ya Kiislamu yanamshajiisha mwanaadamu kurekebisha mwenendo wake, kufuata mafundisho ya dini sambamba na kufanya amali njema huku akijiepusha na mambo machafu kama ulevi na kadhalika.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …